Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Amina atamani SUK ivunjwe

Kada aliyegombea urais kwa tiketi ya CCM, Balozi Amina Salum Ali 

Muktasari:

Balozi Amina pia amesema uamuzi wa CUF kususia uchaguzi wa marudio visiwani humo utasababisha mpasuko mkubwa zaidi na kumtaka katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kufikiria upya na kubadili msimamo huo kwa faida ya Wazanzibari wote.

Kada aliyegombea urais kwa tiketi ya CCM, Amina Salum Ali amesema mgogoro wa kisiasa Zanzibar hautakwisha hata baada ya Uchaguzi wa marudio kwa kuwa ni wa kihistoria na baadhi ya viongozi hawana nia ya dhati ya kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani humo.

Balozi Amina pia amesema uamuzi wa CUF kususia uchaguzi wa marudio visiwani humo utasababisha mpasuko mkubwa zaidi na kumtaka katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kufikiria upya na kubadili msimamo huo kwa faida ya Wazanzibari wote.

Zanzibar imekuwa ikikumbwa na mgogoro wa kisiasa kila inapoingia kwenye Uchaguzi Mkuu kuanzia mwaka 1995 baada ya vyama vya upinzani kuruhusiwa, na vurugu za mwaka 2005 zililazimisha CUF na CCM kuingia kwenye mazungumzo yaliyozaa SUK.

Lakini dalili za SUK kuendelea sasa zinaonekana kufifia baada ya CUF kupinga uamuzi wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa, wawakilishi na madiwani visiwani humo Oktoba 28, mwaka jana na kutangaza uchaguzi mpya Machi 20, ambao chama hicho kikuu cha upinzani kimesema hakitashiriki.

Balozi Amina anaona kuyumba kwa Serikali hiyo ya umoja wa kitaifa kunatokana na Maalim Seif kutotambua kuwa maridhiano hutokana na kupata kitu fulani na wakati huohuo kukubali kupoteza kingine.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwishoni mwa juma, balozi huyo alisema siasa za Zanzibar zitaendelea kuwa za vuta nikuvute mpaka Maalim Seif atakapotambua maana ya maelewano kuwa ni “nipe nikupe”.

Alikuwa akijibu swali lililotaka aeleze kama anaamini kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu Zanzibar kunaweza kuwa suluhu ya mgogoro wa kisiasa.

“Kurudia uchaguzi ni sawa, lakini kuisha kwa matatizo ya kisiasa Zanzibar si kweli,” alisema balozi huyo wa zamani wa Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa.

“Watu wanapaswa kuelewa vizuri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilipatikana vipi na watambue kuwa Maalim Seif ndiye tatizo. Tukianzia hapo tunaweza kupata suluhu ya kudumu ya mgogogo wa Zanzibar.”

Upatikanaji wa SMZ

Akiwa ameongozana na makada wengine watatu wa CCM; Mohammed Hijja (balozi mdogo wa Tanzania India), Abdallah Rashid (aliyemtambulisha kuwa ni mshauri wake wa masuala ya siasa) na Fatuma Maghimbi, Balozi Amina alisema historia ya mgogoro wa Zanzibar ilianza baada ya mapinduzi ya mwaka 1964.

“Mapinduzi yaliwagawa Wazanzibari, kulikuwa na kundi lilibaki Zanzibar na jingine liliondoka kwenda kuishi nje ya nchi. Hilo (kundi) lililoondoka ndilo linalotaka uongozi kwa nguvu zote,” alisema.

“Pale (Zanzibar) kuna siasa za ndani na siasa za nje ya nchi. Zile siasa zinazoanzia nje ya nchi ndiyo zinazoivuruga Zanzibar. Kwa maana hiyo suala hapo si kurudia uchaguzi tu ni kuangalia mambo yote hayo na kuona namna gani yanaweza kudhibitiwa.”

Mgogoro huo ulifikia hatua mbaya mwaka 2000 wakati kulipotokea machafuko yaliyosababisha watu kadhaa kuuawa na wengine kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya.

Mazungumzo ya kutatua mgogoro huo hayakuweza kuzaa matunda licha ya kushirikisha magwiji wa usuluhishi kutoka nje ya nchi.

Mazungumzo yaliyozaa matunda ni ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Mara zote, mazungumzo hayo yamekuwa yakimuhusisha Maalim Seif na wagombea urais kwa tiketi ya CCM; Dk Amani Abeid Karume (mwaka 2000), na Dk Ali Mohamed Shein, ambaye ni rais wa sasa wa Zanzibar.

Tayari viongozi hao wameshakutana mara tisa, lakini hawajaweza kufikia mwafaka.

SUK ivunjwe

Amina alisema wazo la kuwa na SUK lilionekana mwanzoni kuwa lingekuwa mwafaka wa kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar, lakini hali imekuwa tofauti baada ya CUF kushindwa kuelewa dhana ya maelewano.

Alisema angetamani kuona SUK ikivunjwa na kuwa na mfumo mwingine mpya utakaoweza kuleta viongozi wa kuipeleka Zanzibar katika hatima yake ya maendeleo.

“Mimi natamani SUK ingevunjwa na tuwe na mfumo mwingine wa kuongoza Serikali kwa sababu mfumo huo una matatizo. Maalim Seif hajaelewa dhana ya maelewano na hivyo yuko serikalini siyo kwa ajili ya maendeleo bali kupeleleza Serikali ya CCM inafanya nini ili aikosoe. Sasa huo ni unafiki,”alisema.

Alibainisha kuwa mijadala ya mwafaka inapaswa kuheshimiwa na pande zote kwa kuwa ni utaratibu wa nipe nikupe, lakini inapotokea upande mmoja unataka kupokea tu bila kutoa, inakuwa shida.

Alipoulizwa anadhani kwa nini CUF wanaivizia CCM serikalini, alijibu: “Tatizo siyo CUF, ni Maalim Seif.” Alieleza kuwa mazingira yanaonyesha kuwa katibu mkuu huyo wa CUF ana maslahi binafsi na siyo ya Wazanzibari.

Hata hivyo, alikiri kuwa ni vigumu kuvunja muundo wa SUK kwa kuwa kunahitajika mchakato mrefu utakaoshirikisha hata kura za maoni kutoka kwa wananchi.

Amshauri Seif

“Mimi namshauri Seif kujua kuwa katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, afahamu kuwa Tanzania itajengwa na Watanzania na kwa upande wa Zanzibar, Wazanzibari wanataka maendeleo,” alisema.

“Seif analalamika wakati yuko serikalini, anakutana na mwenzake (Dk Shein) wanakula haluwa na kufurahi pamoja, lakini akitoka nje, anageuka. Tutafika wapi kwa siasa za namna hii?”

Amina alisema Zanzibar ilikuwa na bahati kumpata Dk Shein ambaye Maalim Seif angeweza kumtumia kufanya mambo anayotaka, lakini ameshindwa kugundua fursa hiyo na kuanza kujivuruga.

“Chini ya Dk Shein, Zanzibar imepata fursa nzuri ya kufikia maelewano. Shein anawawakilisha Wazanzibari wote na anajua siasa za Zanzibar ni mstahamilivu, ni mwenye busara, msomi na mpenda maendeleo,” alisema Balozi Amina na kuongeza kuwa:

“Hivyo huu ulikuwa wakati mzuri kwa Seif kushirikiana wafanye anachotaka kwa ajili ya maendeleo ya Wazanzibari.”

Alisema kitendo cha CUF kususia uchaguzi wa marudio kitaongeza mpasuko wa kisiasa badala ya kuupunguza, hivyo ni vyema Seif akaliangalia hilo vizuri na kubadili msimamo huo kwa faida ya Wazanzibari wote.

“Uchaguzi huu wa marudio ndio utakuwa kipimo cha kuonyesha nani anakubalika Zanzibar sasa Seif akisusa maana yake nini?” alihoji.

Seif anatishia nyau

Naye balozi mdogo wa Tanzania nchini India ambaye alikuwa na Balozi Amina alisema haamini kama Maalim Seif anaweza kususia uchaguzi huo wa marudio kwa sababu ya hulka yake ya kutaka maslashi binafsi.

“Sioni Seif akisusia uchaguzi huo kwa sababu kuu nne; moja simuoni akimpa fursa mpinzani wake Hamad Rashid Mohamed kuchukua nafasi yake ya umakamu wa kwanza wa Rais. Pia kwa kutoshiriki uchaguzi huo, atahojiwa na wafadhili wa chama chake ambao bila shaka watadai pesa zao,” alisema.

“Vilevile kuna suala la maslahi binafsi ya mafuta ambalo Seif atahojiwa kama atakuwa nje ya mfumo wa Serikali, mwisho hivi ni nani asiyemjua Maalim Seif kama ni mroho wa madaraka?”