Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Kilaini aeleza mamilioni ya Escrow yalivyomtesa

Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, alipowasili mkoani Kagera Julai 2013. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Askofu Msaidizi mstaafu Methodius Kilaini ameelezea jinsi sakata la mabilioni ya Escrow lilivyomtesa na kulazimika kurudisha mgao wake serikalini.

Dar es Salaam.  Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini amezungumzia mgawo wa mamilioni ya shilingi kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, aliyopewa na Mfanyabiashara James Rugemalira akisema ulimsumbua na hakuna mtu aliyetaka kumsikiliza wakati huo.

Sakata hilo lilikuwa moja ya mambo yaliyotikisa wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete ambapo vigogo wa Serikali, majaji, viongozi wa dini na wafanyabiasha walitajwa kwenye mgawo huo wa Sh306 bilioni zilizochotwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Askofu Kilaini pia alitajwa, baadaye alikiri kupokea Sh80.5 milioni kutoka kwa Rugemalira, mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engeering. Kilaini alitajwa kwenye Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyosomwa bungeni 2014 kuwa ni miongoni mwa viongozi wa dini na watu wengine waliopokea mabilioni hayo.

"Ilinipa hali ngumu wakati ule sababu hakuna mtu aliyetaka kusikiliza, waliona watafute kitu cha kuongea ili wapate kitu cha kugonga, sisi tulikuwa tunagongwa," anaanza kueleza Askofu Kilaini katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Ahamisi iliyopita.

"Lakini tunaona baadaye hata Rugemalira alitoka (mahabusu) sababu hawakupata kitu cha kumshtaki, yeye alinipa pesa zile kwa kuwa alikuwa akisaidia watu, aliniambia Askofu nimepata hizi naona zisaidie watoto na vikundi mbalimbali na alikuwa akifanya hivyo mara kwa mara, ilikuwa ni kazi nzuri na mimi nikakubali,” amesema.

"Ila walivyoanza kupiga, wanasema mkubwa wakikudhalilisha chutuma, ndiyo maana wakati ule nilichutuma lakini ilifika mahala nikasema kazi ninayoifanya ni nzuri kuliko hizo pesa, nikawarudishia serikalini, angalau mambo yakapoa,” amesema.

Anasema hakuzigusa pesa zile na alipoingia Rais wa awamu ya tano, John Magufuli zikaleta shida, akazirejesha serikalini.

"Nilichutama wakati ule, watu walishangaa Kilaini haongei, niliona kama ningejitetea ingeleta shida kwa jamii, kwa kuwa usitegemee kila mara watu watakuelewa, itafika mahali hawakuelewi hata kama ndani ya dhamira uko sawa, hata kama una haki ,lakini ukifanya kitu watu wakakwazika kiache,” amesema.

Amesema, "ndiyo sababu hata zile pesa, sawa ziliingizwa kwangu na zilikuwa ni za mfanyabiashara, lakini nikaona niziache, tena aliniingizia kama surprise (bila kumtaarifu).

“Niliziona, baadaye nikamuuliza ni za nini akasema ni za kazi zetu za kusaidia vijana na vikundi.”

"Sikuwa nimemuomba, alikuwa akisaidia watu na kwa kuwa aliijua akaunti yangu akaziingiza, sikuona shida kwa kuwa zilikuwa zake, nilipomuuliza zimetoka wapi?

Kikwete chaguo la Mungu

Moja ya kauli za Askofu Kilaini zilizokuwa gumzo ni ya “Rais Jakaya Kikwete ni chaguo la Mungu, ambayo anasema haikueleweka vizuri kwa umma.

Ilikuwa mwaka 2005 baada ya Kikwete kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa awamu ya nne wa Tanzania.

Kilaini akiwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alitoa kauli hiyo akimtaja Rais Kikwete kuwa chaguo la Mungu.

Wapo waliomwelewa na wengine waliikosoa kauli hiyo, ingawa alisimamia hoja yake kwamba kiongozi yeyote anayechaguliwa na watu anakuwa amesimamishwa na Mungu.

Katika mahojiano hayo Askofu Kilaini anafafanua kauli hiyo na kueleza jinsi alivyomfahamu Kikwete hata kabla hajawa Rais.

"Nilipomuona kwa mara ya kwanza, nilimuona ni mtu mzuri asiyekuwa na kinyongo, hataki kumtesa mtu, anataka kusaidia na yuko tayari kusikiliza.

"Alipokuwa Rais, nilisema ni chaguo la Mungu kwa sababu hiyo, japokuwa kila mara walinisema sana, maneno yalikuwa ni mengi kuhusu kauli hiyo, lakini nawaambia ni mara chache kukutana na kiongozi wa aina hiyo,” amesema.

Askofu Kilaini amesema, "Nilimfahamu akiwa bado ni Waziri wa Mambo ya Nje. Nilienda Zanzibar nikiwa katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, nilikuwa sijazoea kulala hotelini kama padri.

"Nilijisikia mpweke siku hiyo nikiwa pale hotelini ambako walikuwepo pia wabunge wengi na mawaziri wakawa wanapitapita hata wa kumsalimu humuoni.  Yeye (Kikwete) akanifuata na kuanza kunisemesha hadi nikawa sawa,” amesema.

"Pale hotelini kulikuwa na watu wengi, wengine ni Wakatoliki, lakini ni yeye (Kikwete) alikuja kuniona, hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza nafahamiana naye, nikaona huyu ni mtu mzuri,” amesema.

Anakumbuka utani wa Rais Kikwete siku hiyo, baada ya eneo hilo kuanza mambo ya kidunia.

Akaniambia, "Padri hapa si pa kwako tena, nenda kapumzike."

Anasema aliondoka kwenda chumbani kwake akawaacha waendelee na mambo ya kidunia, na kuanzia pale ndipo akawa karibu na waziri huyo, hata alipokuja kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya nne waliendelea kuwa karibu.

Ushauri kwa Salma

Askofu Kilaini anasema, wakati Kikwete anaingia kwenye mchakato wa kuwania urais, alimfuata akamweleza, akampa baraka zote na aliposhinda, mkewe Salma Kikwete alimfuata kuzungumza naye masuala mbalimbali na alikuwa mara kwa mara akimfuata kwa ushauri.

Askofu huyu alisema mara kwa mara alipokuwa akisikia kitu cha tofauti kuhusu Rais Kikwete, alienda kwake kuonana naye na kumuuliza.

“Alikuwa akiniambia ukweli wake, anasema kwenye hili Baba Askofu, liko hivi na hivi, hakuwahi kukasirika ukimweleza ukweli. Lakini wapo viongozi wengine ukimweleza anakasirika, yeye hapana.

“Na hii ni moja ya sababu zilizochangia nimuone ni chaguo la Mungu, japokuwa watu walinipiga vita ile mbaya ila nikasema siku moja mtamkumbuka," alisema.

Kauli kuwa Rais Kikwete ni chaguo la Mungu, Askofu Kilaini aliitoa kwenye hotuba wakati wa mahafali ya Chuo Kikuu cha Mt. Joseph. Alimualika kuwa Kikwete mgeni rasmi akakubali na alishiriki. Hadi leo hata baada ya Rais Kikwete kustaafu, Askofu Kilaini ambaye naye amestaafu uaskofu wiki iliyopita, anasema bado wawili hao wanawasiliana.


Mpigapicha, mwandishi wa vitabu

Askofu Kilaini, pia ni mpigapicha aliyewahi kufanya kazi hiyo ikiwamo kuwa na studio ya kusafisha picha.

"Nilipoenda Roma mara ya kwanza nilipenda mambo ya picha, niliporudi Tanzania nilianzisha studio. Mbali na kupigapicha nilikuwa nazisafisha, niliipenda kazi hii, japokuwa baadaye ilikuwa ngumu kuifanya.

Anasema mwaka 1990 wakati wa ujio wa Baba Mtakatifu nchini, alikuwa Roma, Askofu Mayala alihakikisha anarudi mapema Mwanza kuwa kiongozi wa kikosi cha kuchukua video na picha za ziara hiyo.

"Nikiwa padri nilikuwa napiga picha watu, nikienda mahala wanaomba niwapige picha nafanya hivyo, wao wanalipia gharama za kuosha, nilikuwa pia mpenzi wa kompyuta, niliipata yangu ya kwanza 1989. Mwaka uliofuata nilipokuja Baraza la Maaskofu, watu walidhania ni kitu cha ajabu nikafanya juu chini kuhakikisha zinakuwapo,” anasema.

Anasema pia anapenda uandishi. Ameandika makala na vitabu, huku kitabu chake cha kwanza kikiwa cha Historia ya Kanisa Kagera (Bukoba na Rulenge).

Alivyotekwa kwenye ndege, saa 54 bila kula

Miaka 1981 na 1982 inabaki kwenye kumbukumbu ya Askofu Kilaini, anayesema alipata ajali ya gari na kupasuka fuvu na wakati akielekea kwenye matibabu Roma, ndege aliyopanda ikatekwa nyara.

"Ilikuwa Novemba 15, 1981 nilipopata ajali ya gari eneo la Pasiansi, Mwanza, nikiwa na viongozi wengine wa kiroho tukielekea uwanja wa ndege kwenda Dar es Salaam kwenye mkutano,” anaeleza.

"Tulipelekwa hospitali ya Bugando nikiwa sijitambui, baada ya wiki moja ndipo nilipata fahamu na kujua niko wapi, baada ya uchunguzi daktari aliniambia kichwa kimepasuka kama akitoa ngozi ya juu, basi kule ndani ataokota vimfupa vya fuvu la kichwa.

"Nilikaa Bugando kwa mwezi mmoja kisha nikahamishiwa KCMC na baadaye nikatakiwa kwenda Roma kwa matibabu zaidi,” anasimulia.

"Siku ya safari, Februari 27, 1982 tulitekwa, tulikaa kwenye ndege saa 54 bila kula,” anaeleza.

Anasema walikuwa kwenye ndege ya ATC kutoka Mwanza kwenda Dar es Saalam ambapo alitarajia kupanda ndege nyingine kwenda Roma, ndege hiyo haikuweza kufika Dar es Saalam badala yake ilitekwa ikiwa njiani na kupelekwa Nairobi, Kenya, ikaelekea Jeddah, kisha Athens, Ugiriki.

"Kwenye maeneo hayo ilitua tu na kuweka mafuta sehemu nyingine ikinyimwa ruhusa, walitaka kwenda Libya wakakataa, Roma wakakataa, Marekani nako wakakataa, watekaji walikuwa watano, wawili kutoka Zanzibar na wengine Tanzania Bara.

Alisema baadaye walipelekwa Uingereza, walipofika London, Waziri Mkuu wa Uingereza enzi hizo akiwa Margaret Thatcher alitoa amri kwamba ndege iachiwe iingie lakini kwa vyovyote isiruhusiwe kuondoka.

Alisema maongezi ya kina yalifanyika kati ya Serikali ya Uingereza na watekaji hao na hapo ndipo waliporuhusiwa kuteremka kwenye ndege na kupata huduma.

"Serikali ya Tanzania ilitaka watu wake kurudi nchini, mimi nilikuwa na vyeti vya daktari, pasipoti na vitambulisho vingine vilivyoonyesha nakwenda Roma kwenye matibabu, nikaruhusiwa kuendelea na safari.

""Nilikuwa nimevaa vizuri, watekaji wakanionyesha mtutu na kunihoji naenda wapi, walifanya tukio lile wakidai Nyerere ajiuzulu, tulikuja kugundua baadaye wale walikuwa na chama chao, mmoja mwenyekiti, katibu na wengine, walikuwa pia na familia zao wakitarajia tukio lile liwape maisha," anasema.