Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Kilaini asimulia familia ilivyokataa awe padri

Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini.

Muktasari:

  • Askofu Methodius Kilaini ameeleza maisha ya miaka 51 ya upadri na 23 ya uaskofu hadi alipostaafu akiwa na umri wa miaka 75, akitaja alivyoingia kwa mbinde na nafasi ya Hayati Kardinali Laurean Rugambwa kwenye maisha yake.

Dar es Salaam. ”Nililelewa na babu ambaye hakuwa Mkatoliki, alikuwa na wake wanne, bibi yangu akiwa ndiye mke mkubwa. Babu alitaka nioe na kuendeleza familia, alinipa shamba na nyumba niishi na mke wangu na watoto baada ya kuoa.”

 Hii ni simulizi ya Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, aliyoitoa katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwishoni mwa wiki, ikiwa ni siku nane tangu Papa Francisco, kiongozi wa kanisa hilo duniani, aliridhie ombi lake la kustaafu baada ya kufikisha umri wa miaka 75.

Papa Francisco aliliridhia ombi la Askofu Kilaini kustaafu Januari 27 mwaka huu kwa mujibu wa sheria za Kanisa, akiwa amehudumu kwa miaka 23 ya uaskofu na 51 ya upadri.

“Sheria ya kanisa inataka ukifika miaka 75 uombe kustaafu, usikae hapo na ukaonekana king’ang’anizi. Hivyo nimestaafu kwa sheria za kanisa, ingawa sijastaafu ukuhani, nitaendelea kuhubiri na kutangaza ufalme wa Mungu. Nilichostaafu ni kwenye uamuzi wa kiutawala na kiuongozi,” anasema Askofu Kilaini mwenye miaka 75

Askofu huyo aliyepewa daraja takatifu la upadri jijini Roma, Machi 18, 1972 na Kardinali Agnelo Rossi kama padri wa Jimbo la Bukoba, mkoani Kagera.

Katika mahojiano hayo, Askofu Kilaini anaeleza safari yake ya miaka 51 ya upadri ilivyokuwa ngumu, kwamba akiwa anasoma sekondari mawazo yalikuwa ni mengi, kipindi hicho alikuwa ni kijana msomi ambaye familia ilitamani aje kuwa mhandisi au daktari.

“Nilipohitimu darasa la 12 (kidato cha nne), kwenye mtihani wa ‘cambridge’ tulikuwa watu watatu tuliopata daraja la kwanza, wenzangu walikwenda nje ya nchi, wakati huo ndipo nilifanya uamuzi mgumu wa kubaki nchini nikaenda seminari ya Ntungamo.

Kwenye Seminari ya Ntungamo katika Jimbo la Bukoba alijifunza falsafa kwa muda wa mwaka mmoja. Akiwa hapo alifanya mambo ya dini, pia akifanya kazi nyingine za kawaida.

“Nilisema huwezi kujua, hivyo nikawa nafanya vyote, waliponituma Roma ni kama Roho Mtakatifu alinishukia, nikasema Mungu ameniita nimtumikie.

“Sijui nisingetumwa Roma ingekuaje? Kabla sijaondoka nilikuwa nafanya vitu vya kanisa na vingine, nilikuwa naandika Oxford wananitumia masomo, lakini nilipokwenda Roma, yote yakaisha,” anasema.


Familia yapinga awe padri

Akiwa mwenye tabasamu wakati wote wa mahojiano, Askofu Kilaini anasema alipoingia kwenye upadri, familia yake haikutarajia na haikutaka.

“Waliamini nitarudi na kuishi maisha mengine kama vijana wengine. Nimekuwa padri nikiwa kijana wa miaka 23 tu, mama yangu, bibi zangu na babu yangu ambaye hakuwa Mkatoliki wakati huo, hawakupenda.

“Isipokuwa bibi yangu mzaa baba, huyu sikujua yuko upande gani, maana hakuwa anaongea chochote, alikaa kimya tu, yeye ndiye alinilea na kunipeleka kanisani nikiwa mdogo.

“Wazazi wangu walikwenda Moshi kikazi, nikabaki na bibi yangu huyo mzaa baba, ambaye alikuwa ni mke mkubwa kwa babu, alibatizwa na alikuwa ni Mkatoliki.

Anasema, “baba yeye alipenda niwe padri, lakini mama, bibi zangu wengine na babu hawakutaka. Babu alifariki dunia akiwa amenirithisha shamba na nyumba, aliniambia ukioa ukae humu, alikuwa hajaamini (hajabatizwa), tena wakati huo nilishakuwa padri tayari, yeye aliamini ipo siku nitarudi kwenye maisha ya kawaida (ya useja).

Mfahamu Askofu Kilaini

Askofu Kilaini anasema babu yake alijifunza kwa Wajerumani, alikuwa na shamba kubwa na mifugo mingi, “hivyo alitaka mimi nirithi niviendeleze, aliona nikiwa padri nani atarithi.

“Bibi mzaa mama mara kwa mara alikuwa akiniita na kuniambia ‘mama yako hapendi kabisa uwe padri’, wao walitaka niwe mhandisi au daktari, nijenge nyumba na nipate familia.

“Walitamani hivyo kwa kuwa nilikuwa mtoto wa kwanza wa kiume na babu yangu alizaa watoto wote wa kike, isipokuwa baba yangu ambaye mimi nilikuwa kijana wake mkubwa, lakini ndoto yangu ilikuwa ni kufanya kazi ya Mungu,” anasema.

Anasema baadaye mama yake alikuja kupenda (kukubali), ingawa mara kadhaa walikuwa wakimuuliza kama haiwezekani akarudi kwenye maisha ya kawaida nje ya upadri.

Anasema yeye alianza kupenda upadri akiwa kijana mdogo wa miaka 10.

“Babu yangu alikuwa akifahamu lugha ya Kijerumani, wakati ule niko mdogo, Wamisionari walikuwa wakija nyumbani kwetu, nilipowaona kwa mara ya kwanza niliwapenda, nikasema na mimi nataka kuwa kama wao.

Akiwa na miaka 11, anasema aliingia seminari, licha ya umri wake mdogo alipenda mambo ya kiroho na upadri baada ya kuwaona wamisionari na mapadri wengine wa Afrika.

“Huenda ningepata ushawishi nikatoka, lakini nilipotumwa Roma, nikajikuta kwenye kazi ya Mungu moja kwa moja na sijawahi kujutia, katika maisha yangu yote nimejaribu niwezavyo niishi kwenye upadri, licha ya shida na madhaifu yangu tangu 1972.


Pamoja na misukusuko, changamoto na mafanikio katika kipindi chote, anasema kikubwa anachojivunia ni uhusiano wake na watu na mwenyezi Mungu.

“Ukimpenda Mungu, utawapenda watu, hiki ndicho kikubwa ninachojivunia katika miaka yangu 51 kwenye upadri,” anasema Askofu Kilaini

Anasema, kipindi chote hicho amefanya kazi na watu mbalimbali hadi wa dini zingine, akiamini wote ni watu wa Mungu.

“Ilikuwa miaka 51 isiyo ya mchezo, nimefurahia, licha ya mapungufu yangu ambayo najua ninayo, lakini nimekwenda vizuri,” anasema.


Achagua azikwe Bukoba

Desemba 5, 2009 Papa Benedikto VI, alimhamisha Askofu Kilaini kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwenda jimbo la nyumbani la Bukoba kuendelea na wadhifa wake wa askofu msaidizi.

Huku ndiko amestaafia na ndiko amechagua kuzikwa baada ya maisha yake duniani.

Kikawaida Askofu anapofariki dunia, huzikwa kanisani alipochagua katika maeneo alikotumikia, Kilaini ambaye ametumikia Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Bukoba kwa nyakati tofauti, anasema yeye kaburi lake litakuwa Bukoba.

“Iwe ni kanisani au mahali popote pale, kwangu ni Bukoba, nitazikwa huku wakati ukifika.

“Tena hili sikuwa nimelisema kabla, lakini kupitia gazeti la Mwananchi, ni rasmi, wakati wangu ukifika wa kuchukuliwa, nizikwe Bukoba,” anasema.


Mapokezi yamponya kiharusi

Akikumbuka alipohamishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba mwaka 2009, anasema ni kipindi ambacho alikuwa ametoka kwenye matibabu nchini India.

“Nilipata kiharusi, nilikwenda India kutibiwa mwezi mzima, niliporudi mdomo ulikuwa bado umepinda, ndicho kipindi ambacho nilihamishiwa Bukoba.

“Hali haikuwa nzuri. Wakati huo niliona nitashindwa kuimudu Dar es Salaam ambalo ni jimbo linalohitaji nguvu zaidi, nilipoletwa Bukoba ilikuwa ni kama kupumzika,” anasema.

“Mapokezi waliyonipa Bukoba, hadi kiharusi kikapona. Kuanzia mpakani walikuja kwa maandamano kunipokea, nilijisikia nimekuja nyumbani kweli,” anasema kiongozi huyo.

Anasema akiwa Bukoba alikuta kazi ya kumalizika ukarabati wa Kanisa Kuu la Jimbo ukiendelea na yeye kwa kushirikiana na rafiki wake wengine wa Dar es Salaam nao waliwachangia likaisha haraka.”

Mbali ya kusimamia ukamilishaji wa kanisa hilo, Askofu Kilaini kama alivyosaidia kuanzisha Television Tumaini akiwa Dar es Salaam, kwa upande wa Bukoba amesaidia vilevile kuanzisha Radio Mbiu akishirikiana na Radio Maria.


Alivyovutiwa na Kardinali Rugambwa

Askofu Kilaini anamtaja, Hayati Kardinali Laurean Rugambwa, kama mtu aliyefanikisha safari yake ya kuwa padri, akimtaja kama kiongozi ambaye alijishusha kwa kila mtu na hakutaka maisha ya juu.

“Hata alipougua, yeye kama kardinali angeweza kusema nipelekeni Roma au Ulaya nikatibiwe, alikataa vyote na kuugulia nyumbani kwake pale Osterbay, jijini Dar es Salaam.

“Alikataa, alisema ‘hapana, mimi nimefika umri wangu na muda wangu umeisha, kuugua kwangu ni sawa, mimi nitakaa hapa, daktari atakuwa anakuja kunitizama hapa’,” anasema.

“(Rugambwa) alifia nyumbani kwake akiwa mgonjwa, hakufia Marekani wala Ulaya, alikubali kwamba umri umefika, hakuna sababu ya kuangaisha watu kwamba nipeleke huku wala huku.”

“Nilikwenda nikawa namuona anapotea polepole, akaniambia niombee siku zimefika, alimpenda sana Mama Maria, ilipofika mwezi wa nane nilidhania atakufa tarehe 15 siku ya Bikra Maria, ikapita.

“Ilipofika Desemba 8, 1997 ambayo nayo ni Sikukuu ya Bikra Maria ndipo alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85. Siku hiyo asubuhi ‘watoto wake’ wa Shirika la Watawa Masisita Wadogo wa Mtakatifu Fransisco alilolianzisha, siku hiyo walikuwa na sherehe ya kufanya nadhiri.

“Aliacha wakazifanya, ilipokwisha siku hiyo usiku saa 4 ndipo akafariki dunia kwa utulivu, alikuwa mtu wa Mungu aliyesali sana, mimi naamini yuko mbinguni ananiombea,” anasema.

Simulizi milima, mabonde ya Askofu Kilaini

Askofu Kilaini anasema, unapomwongelea Kardinali Laurean Rugambwa unamgusa (yeye) kwa kuwa ni mtoto wake na alimlea na ndiye alimtuma Roma kujifunza upadri.

“Hadi anafariki nilikuwa naye, alinipa wosia wake alivyokuwa anatuacha, vitu vichache alivyokuwa navyo alisema nivigawe ninavyoona.

“Nilivyokwenda kwenye nyumba yake, nikasema nigawe nguo zake kwa ndugu zake kama kumbukumbu kwa kuwa wasingeweza kuchukua kanzu la ukardinari wala nguo zake za misa, nikasema nichukue mashati na suruali zake niwape ndugu zake angalau wamkumbuke,” anasema.

“Cha kushangaza sikukuta nguo nzuri ya kumpa mtu, zilikuwa kuukuu, sababu hela alizopata alikuwa akisaidia watu, ilinishangaza na kunifundisha sana, huyu mtu mkubwa mwenye pesa nyingi lakini yeye mwenyewe hakujijali sana, alikuwa ni mtu wa kujali wengine.”

Anasema, Kardinal Rugambwa alipokuwa askofu pale Bukoba, walimpa kasehemu kadogo, wazungu wote wakaondoka na kumuacha.

“Alipambana hadi Papa alipomuona na kumteua kuwa kardinali, tena si kardinali tu, bali kardinali wa kwanza Mwafrika, leo hii mtu akiwa kardinal tunashangilia.

Askofu Kilaini anasema, “Kardinali Rugambwa alipokwenda Marekani, wale Wamarekani weusi wakati huo walikuwa hawajaruhusiwa kupiga kura, walipomuona huyo kardinari mweusi walimbeba, kule Ujerumani walitaka kuona huyu ni mtu wa aina gani.

“Walimfurahia na kumuuliza tukupe zawadi gani, yeye akachagua kujenga shule ya sekondari ya wasichana, ndipo ikajengwa hii ya Rugambwa, hata baada ya kuitaifisha, tunashukuru bado inaitwa Rugambwa,” anasema.

Shule hiyo ya kidato cha kwanza hadi cha sita ilianzishwa mwaka 1965, imejengwa katika Kijiji cha Kitendaguro, Bukoba. Ikichukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwemo wenye mahitaji maalumu.

Anasema hata alipokuwa Dar es Salaam, si Wakristo tu, hadi madhehenu mengine walimuunga mkono, hakuna aliyesema hapana yeye akisema. Hata kwenye ujumbe kwa Serikali walitaka awaongoze, alijishusha kwa kila mmoja bila kujali ni mtu wa aina gani.

Akizungumza alivyokutana kwa mara ya kwanza na kardinal huyo, Askofu Kilaini anasema alikuwa akimuona tu wakati huo yeye akiwa darasa la tano au la sita.

“Alipokuja Ntungamo (Seminari Kuu), nilikwenda kutumikia misa kwenye nyumba yake. Hapo ndipo nilifahamiana naye, nakumbuka tulikuwa wawili ndipo baadaye akatutuma Roma kwenda kujifunza, hata niliporudi kutoka kuchukua Shahada ya Uzamivu, alinipa pesa nichape kitabu change (tasinifu),” anasema.

Anasema Kardinal Rugambwa aliyezaliwa Kijiji cha Bukongo-Kamachumu, Bukoba Julai 12, 1912 na kupewa upadri Desemba 12, 1943 alikuwa mtu mkubwa, mnyenyekevu ambaye alikuwa akizungumza na kila mtu, bila kujali hali yake kipesa.

Desemba 13, 1951 aliteuliwa kuwa Askofu na Vikarieti ya Kitume ya Kagera Kusini. Alipewa daraja takatifu hilo Februari 10, 1952 na Askofu David Mathew. Eneo alilokabidhiwa likafanywa kuwa Jimbo la Rutabo Machi 1953 na Juni 21, 1960 likabadilishiwa jina kuwa Jimbo Katoliki la Bukoba.

Papa Yohane XXIII alimteua kuwa Kardinali Machi 28, 1960 akimkabidhi usimamizi wa Parokia ya San Francesco d'Assisi a Ripa Grande mjini Roma. Alikuwa Kardinali wa kwanza asiye Mzungu na Mwafrika. Alishiriki Mtaguso wa pili wa Vatikano na mikutano mitatu ya uchaguzi wa Papa (1963, 1978 na 1978 tena).

Desemba 19, 1968, alihamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam aliloliongoza hadi alipojiuzulu kutokana na uzee Julai 22, 1992.

“Mwaka 1962 hadi 1965 kipindi ambacho maaskofu wote wa ulimwengu walipokwenda Roma yeye peke yake ndiye alipewa kuzungumza, alikuwa mtu mkubwa, si mkubwa tu bali mnyenyekevu sana, Rais (mstaafu Benjamin) Mkapa aliwahi kusema alimshangaa alipomkuta akizungumza na watu wa chini kabisa,” anasema Askofu Kilaini.

Akihitimisha kumzungumzia Kardinali Rugambwa, Askofu Kilaini anasema, “nimestaafu hivi sasa, nafikiri nimepata muda wa kumtangaza na kufanya ajulikane kwa watu, kwani ni kama tulimsahau kidogo huyu mwana mtukuka wa Tanzania.”


Ujumbe kwa wanandoa

Kiongozi huyo wa kiroho anasema katika miaka 51 ya upadri na 23 ya uaskofu kuna mambo mengi amekutana nayo ikiwemo migogoro na kuwa “kukosekana uaminifu kwenye ndoa likiongoza”.

“Mgogoro ulioongoza ni kukosa uaminifu, huu haukuwa kwa kina baba tu, hadi kina mama, tofauti yao kina mama wanakwenda chinichini na kina baba wanakwenda kifuakifua.

“Inapokuja kubumbuluka (kujulikana) inafikia hatua hadi kina baba wanahoji watoto hawa hakuna wa kwangu, kweli?

“Hiki ndicho kitu kikubwa kinachoongoza kuvunjika kwa ndoa, uaminifu ukikosekana kwenye ndoa ni hatari, hata Mwenyezi Mungu aliumba ndoa ya watu wawili, wenzetu Waislamu wanakwenda hadi wanne, hata wenyewe ukienda nje ya ndoa ni balaa,” anasema.

Anasema kingine ambacho alikisuluhisha mara nyingi ni watu kuwa wagumu kusamehe wanapokosewa na wake au waume zao.

“Kusamehe kulikosekana, mtu anasema huyu alifanya hiki simtaki, hata akitubu, wengi walikuwa hawasamehi, nawahasa watu kujifunza kusamehe, sote ni wadhambi na msamahaa ni muhimu,” anasema.

Jambo la tatu ambalo, Askofu huyo anasema alilichukia kuliko na ataendelea kulichukia ni marafiki kuingilia ndoa.

“Huu nao ulikuwa ni mgogoro ulioongoza kwa wanandoa na kusababisha kutoelewana, marafiki kuwaletea maneno, mengine ya uongo na kuzichonganisha ndoa nyingi.

“Hii ilikuwa pia kwa mmojawapo kwenye ndoa kuwa na vikundi fulani na kuiga tabia za watu wa kikundi hicho ambazo si nzuri.

“Hili niliseme wazi, hakuna watu nawachukia kama marafiki wabaya ambao hawawatakii mema wanandoa. Kila mara niliwapiga vita watu wa aina hii, hakuna watu nawachukia kama wachonganishi wa ndoa hawa ni mashetani,” alisema.

Anasema, mtu anapokuja kukwambia vibaya juu ya mume au mke wako, huyo hakutakii mema, akibainisha yule anayewatakia mema ni anayewaita wote wawili na kuwasema mkiwa pamoja, na sio yale maneno maneno ya uchonganishi ambayo alikutana nayo kwenye usuluhishi wa ndoa nyingi.

Akizungumzia mwenendo wa ndoa kwa miaka ya karibuni na ongezeko la talaka, Askofu huyo anasema nyingi za sasa zina shida.

“Bado tunaendelea kupiga kelele na kutoa mafunzo, ndoa ndiyo kiini cha maisha ikienda vibaya huwezi kuwa na jumuiya nzuri, itakuwa nzuri kama matayarisho yake yatakuwa mazuri, si kwa watu kuokotana.

Amesema, kuna watu kabla hawajaamua kukaa pamoja walishapata mtoto, hivyo wanakosa cha kufanya wengi wao huwa wanakwenda kwenda tu kwa kuwa hajui amuache au la.

“Kabla hajapata mtoto mkubaliane, mpendane na kisha muoane, lakini siku hizi wapo wanaooana bila kuoana, wako pamoja lakini si kimawazo wala kimaisha.

“Nawashauri, kabla ya kuingia kwenye ndoa, miezi mitatu, waje pamoja wasikilize mawaidha ya ndoa, ukiyasikia kabla yatakuingia kwa kuwa yanawatayarisha, lakini ukiyasikia baada ya ndoa utakuwa unaona kama yanamsema mwenzako,” anasema.

Anasema ni mbaya ndoa kuvunjika, mbaya zaidi mkiwa na watoto, ni bora ufukuzwe kazi utapata nyingine, si ndoa ivunjike tena mkiwa na watoto.


Huyu ndiye Askofu Kilaini

Baada ya Seminari Ku Ntungamo, mwaka 1968-1972 Askofu Kilaini alijiunga Chuo Kikuu cha Urbaniana ambako alipata Shahada ya kwanza (B.A) na ya pili (STL) katika somo la Thiolojia.

Alipewa upadrisho jijini Roma mwaka 1972 na Kardinali Agnelo Rossi baada ya kupata Shahada ya Pili ya teolojia huko Roma. Baada ya kurudi nyumbani Bukoba, alifanya kazi parokiani, baadaye alikuwa mhazini msaidizi wa jimbo la Bukoba.

Kati ya mwaka 1978 hadi 1985 alifundisha Historia ya Kanisa katika Seminari Kuu ya Ntungamo. Mwaka 1985 alirudi Roma na kupata Shahada ya Udaktari wa tauhidi katika Historia ya Kanisa kutoka Chuo cha Gregoriana mwaka 1990.

Mwaka 1990 hadi 2000 alikuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Desemba 22, 1999, Papa Yohane Paulo II, alimteuwa kuwa Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam na aliwekwa wakfu Machi 18, 2000 na Kardinali Polycarp Pengo.

Desemba 5, 2009, Papa Benedikto XVI alimhamisha kutoka Jimbo kuuM wa Jimbo la Bukoba. Oktoba 1, 2022, Papa Francisko alimteuwa kuwa ni Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Bukoba, utume ambao ulifikia ukomo wake Januari 27, 2024.

Akiwa Dar es Salaam, anakumbukwa kwa kuratibu majengo mengi yaliyopo makao makuu ya maaskofu Kurasini na kuongeza viwanja vya kanisa.

Vile vile alishiriki kuleta maelewano kati ya viongozi wa dini mbalimbali. Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Tume ya Kikristo ya huduma za jamii mwaka 1992 (CSSC), vilevile wa Tume ya amani ya viongozi wa dini mwaka 1994.

Kule Bukoba alisaidia kukamilisha Ukarabati wa Kanisa Kuu la jimbo na kuratibu kuhamisha mwili wa Laurean Kardinali Rugambwa uliokuwa umehidhiwa kwa muda katika Kanisa la Kashozi. Alisaidia vilevile kuanzisha Radio Mbiu akishirikiana na Radio Maria.