Asilimia 90 wagonjwa wa kifafa hawafuati tiba hospitalini

Muktasari:
- Wakati jamii kubwa ikiwa na imani potofu kuwahusu wagonjwa wanaoanguka wataalamu wa mishipa ya fahamu nchini wamesema asilimia 90 ya wagonjwa hao hawafiki hospitalini kutibiwa na wengi huishia kwa waganga na nyumba za ibada ilhali matatizo hayo hutibika kisayansi.
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema asilimia 75 ya wagonjwa wanaougua kifafa nchini wanaishia kwenda kutafuta tiba kwa waganga wa kienyeji, asilimia 15 wakienda kuombewa katika nyumba za ibada na asilimia 10 pekee hufika hospitalini.
Hata hivyo wameeleza kuwa matatizo hayo yanatibika iwapo mgonjwa atawahi kufika katika vituo vya kutolea tiba kwa wakati.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 8, 2024 Daktari bingwa wa mishipa ya fahamu na uti wa mgongo na ubongo, Patience Njenje amesema mgonjwa anapowahishwa hospitali katika hatua za awali za ugonjwa uwezekano wa kupona ni mkubwa.
Amesema Tanzania inakadiriwa na wagonjwa milioni moja wa kifafa huku wilaya ya Mahenge ikiwa na idadi kubwa ya wagonjwa ikifuatiwa na wilaya ya Haidom.
“Kifafa kinapona, lakini mgonjwa wa kifafa kila anapokuwa anapata degedege mara kwa mara inaharibu mishipa akifika kwetu tayari kumbukumbu inakua ipo chini, ameathirika kwa kiasi kikubwa,” amesema Dk Njenje na kuongeza;
“Asilimia kubwa hufichwa hasa watoto. Asilimia 75 ya wagonjwa huenda kuwaona waganga wa jadi na wengine huenda kuwaona viongozi wa kiroho, si kitu kibaya kutafuta msaada nyumba za ibada ila utaratibu huo ufuatwe baada ya kuhudhuria kwa wataalamu wa afya.”
Hata hivyo amesema baada ya mgonjwa kuathirika kwa asilimia 5 mpaka 10 ndipo huweza kupata matibabu hospitalini.
Dk Njenje ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Kifafa Tanzania (TEA) amesema maadhimisho ya siku ya kifafa yanatarajiwa kufanyika Februari 13 mwaka huu yakiwa na kaulimbiu #TokomezaUnyanyapaa.
Ametaja chanzo cha ugonjwa huo kuwa ni homa wakati wa utoto, uzazi pingamizi na kwa watu wazima mara nyingi husababishwa na minyoo, uvimbe Kwenye ubongo na baadhi hutokana na ajali kichwani au upungufu wa kinga.
Dk Njenje ametaja dalili za kifafa kuwa ni pamoja na kifafa cha kupoteza fahamu ambacho mgonjwa anaweza kaza na kuchezesha viungo vya mwili na kutoa sauti.
Alitaja dalili ya kifafa cha kutopoteza fahamu ambacho wengi wa wanajamii hawana ujuzi nacho mgonjwa kuwa na kiungo kimoja au msuli kuwa unatikisika wenyewe.