Ajali ya Precision itaendelea kukumbukwa 

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 ikitolewa kwenye maji.

Dar es Salaam. Mhariri wa Mafunzo wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rashid Kejo amesema ajali ya ndege ya Precision Air ni moja ya matukio yaliyotikisa mwaka 2022 na hayatasahaulika.

Kejo amebainisha hayo leo Jumatano, Desemba 28,2022 wakati akichangia kwenye mjadala wa Twitter Space unaoandaliwa na MCL ukiwa na mada “mwaka 2022 ulikuwaje kwa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii.”

Ajali hiyo iliyoua watu 19 na 24 kuokolewa, ilitokea Novemba 6, 2022 kwa ndege hiyo iliyokuwa inatoka jijini Dar es Salaam kutumbukia Ziwa Victoria, takribani mita 500 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Mkoa wa Kagera.

Akizungumzia ajali hiyo, Kejo amesema mambo mengi yaliibuka ikiwemo hili la kijana shujaa Majaliwa ambaye alisaidia katika uokoaji wa watu katika ndege hiyo.

"Ajali ya ndege ya Precision Air ni jambo ambalo litaendelea kukumbukwa kwani Tanzania haijawahi kupata ajali ya ndege kubwa kiasi kile ulikuwa ni mshtuko mkubwa.

"Lakini hasa baada ya ajali yaliyotokea, waliibuka mashujaa wengine, kukaibika mjadala wa Majaliwa hivyo ni tukio ambalo miaka nenda tutaendelea kulikumbuka kwa sababu pia yapo mengi ambayo tunapaswa kujifunza kupitia tukio lile," amesema Kejo.

Kejo amebainisha jambo jingine kuwa ni mkutano wa siku ya uhuru wa vyombo vya habari ambao kwa mara ya kwanza ulihudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine wa sekta ya habari kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

"Mkutano wa siku wa vyombo vya habari duniani kwa mara ya kwanza katika historia kwa mara ya kwanza ulihudhuriaa na Rais Samia Suluhu Hassan na kushirikisha wadau mbalimbali wa habari kutoka maeneo tofauti duniani," amesema.