Bima ya marubani Precision Air yalipwa

Muktasari:

  • Kampuni ya Bima ya Alliance Life Assurance tayari imeshalipa malipo ya bima ya maisha marubani wawili waliofariki katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba mkoani Kagera.

Dar es Salaam. Kampuni ya Bima ya Alliance Life Assurance tayari imeshalipa malipo ya bima ya maisha marubani wawili waliofariki katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba mkoani Kagera.


Ajali hiyo iliyotokea iliyotokea Novemba 6, mwaka huu saa 2:53 asubuhi ilisababisha vifo vya watu 19 wakiwemo marubani hao.


Ndege hiyo ilianguka katika Ziwa Victoria takribani mita 100 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, mkoani Kagera ikiwa na watu 43 waliokuwa wakitoa jijini Dar es Salaam, kati yao 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.


Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 9, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa Alliance Life, Byford Mutimusakwa amethibitisha kufanyika kwa malipo hayo bila kuweka bayana kiasi cha malipo hayo.

Amesema wameshakabidhi hundi ya mafao hayo kwa kampuni ya Precision Air na kueleza kuwa fedha hizo zitakwenda kusaidia familia za marubani hao.


Kwa upande wake Meneja Masoko na Mauzo wa Alliance Life, Josephine Mfikwa amesema kuwa wamelipa malipo ya bima ya maisha marubani hao kwa kuwa shirika walilokuwa wakifanya kazi limewakatia bima hiyo wafanyakazi wake.


“Precision Air wamekuwa ni wateja wetu wa muda mrefu kwa kuwa wamewakatia bima wafanyakazi wao katika kampuni yetu, kwa wateja wetu ikitokea mfanyakazi amefariki tunaanza kwa kulipa bima ya mazishi kisha baadae tunamaliza kwa fao la bima ya maisha,” anasema.

Mfikwa amesema wamekabidhi malipo hayo kwa shirika la Precision Air kwa kuwa kampuni hiyo ndiyo iliyokata bima hiyo kwa wafanyakazi wake kisha wao watafanya mchakato wa kuwasilisha kwa familia husika.


“Wakati mwingine mwajiri anaweza kutoa idhini ya fedha hizo kuwasilishwa moja kwa moja kwa wanafamilia baada ya kujiridhisha,” anasema.


Kwa upande wake Meneja Masoko na Mauzo wa Shirika la Ndege la Precision Air, Hillary Mremi amethibisha kufanyika kwa malipo hayo na kueleza kuwa mchakato wa kuwasilisha kwa familia za marubani hao umeanza.

Ameongeza kuwa amesema mchakato wa malipo ya fidia kwa familia zilizoathiriwa na ajali hiyo bado unaendelea.

Awali akizungumza na waandishi wa habari  Jumatatu ya Novemba 14, mwaka huu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Patrick Mwanri alisema mchakato huo utakaokuwa kati ya familia za waliothirika na shirika hilo na utafanyika kwa umakini mkubwa.


Hata hivyo, wiki kadhaa zilizopita Mwenyekiti wa Chama cha Kampuni za Bima, Khamis Suleiman aliiambia Mwananchi kuwa inapotokea ajali ya ndege bima inatakiwa kumlipa mwathirika Sh300 milioni.