Aendesha gari likiwa linawaka moto, wananchi wauzima

Wakazi wa mji mdogo wa Sirari Wilaya ya Tarime mpakani mwa Tanzania na Kenya wakishuhudia Fuso lililosheheni bidhaa likiteketea kwa moto. Picha na Mpiga Picha Maalum
Musoma. Gari aina ya Fuso lililopakia bidhaa mbalimbali limenusurika kuteketea kwa moto ambao chanzo chake hakijafahamika huku tukio la kushangaza zaidi likiwa ni dereva ambaye jina lake halijafahamika kuliendesha gari hilo likiwa linawaka moto hadi kwenye uwanja umbali wa takribani kilomita moja.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano Septemba 20, 2023 wakati gari hilo likiwa limeegeshwa eneo la mpaka wa Sirari Wilaya ya Tarime.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na akiahidi kutoa taarifa za kina baada ya kupokea taarifa kutoka kwa maofisa wake waliokuwa eneo la tukio.
"Nimepokea taarifa za awali kuhusu tukio hilo na tayari maofisa wangu wako eneo la tukio...,nitatoa taarifa zaidi baadaye. Ninachoweza kwa sasa ni kuthibitisha kuwa ni kweli tukio hilo lipo," amesema Magere.
Mashuhuda
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamemsifu dereva wa gari hilo kwa ujasiri wa kuliondoa kwa kasi gari hilo likiwa linawaka moto kutoka katika maegesho eneo la mpakani hadi uwanja wa michezo wa Sirari maarufu kama uwanja wa Tarafa, umbali wa takriban kilometa moja kutoka kituo cha forodha Sirari.
"Nilikuwa nimesimama pembeni mwa barabara kuu ya Sirari - Tarime, nikaona Fuso linaloteketea kwa moto likikimbizwa kwa kasi kutoka upande wa forodha kuelekea Tarime. Ghafla, gari lilikata kona kuingia uwanja wa Tarafa. Tulipokimbilia huko, tukakuta gari linaendeshwa kuzunguka uwanjani huku moto ukiendelea kuwaka," amesema Johnson Marwa, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo
Shuhuda mwingine, Elizabeth Masagati amesema waliofika kutoa msaada walipiga kelele kumtaka kushuka ili kuokoa maisha yake baada ya kuona moto unazidi.
"Tunamshukuru Mungu alisikiliza ushauri na kuteremka huku wananchi wakitumia maji, mchanga na vifaa vvingine kuuzima moto," amesema Elizabeth
Juhudi za wananchi hao ambao baadhi walionyesha ujasiri kwa kupanda juu ya gari ambako hakukuwa na moto na kuanza kurusha mizigo chini huku ikidaiwa ipo iliyoibiwa.
Dereva wa gari hilo ambaye muda wote alikuwa akizunguka huku na kule akilia, hakuweza kuzungumzia tukio hilo kutokana hamaki na taharuki aliyokuwa nayo.