Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Adha ya mvua inavyotesa wakazi wa Dar, mikoani

Muktasari:

  • Mvua zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini zimesababisha adha kubwa kwa wananchi, ikiwamo barabara kufungwa, usafiri kuwa mgumu na gharama kupanda.

Dar/mikoani. Barabara hazipitiki, kazini na hata shuleni hakuendeki. Huu ndio uhalisia wa hali ilivyo katika baadhi ya maeneo nchini, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mfululizo.

Mbali na uharibifu wa miundombinu, kuongezeka kwa gharama za usafiri kutoka eneo moja kwenda jingine na msongamano barabarani ni miongoni mwa changamoto, huku baadhi ya maeneo wakineemeka kwa mazao kustawi.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa madhara kuongezeka kwa kuwa mvua hizo zitaendelea hadi Mei mwaka huu, kama inavyoelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Meneja Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla, amesema mvua zinazoendelea Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar ni za siku mbili mfululizo kuanzia Aprili 28.

"Katika mikoa ya Ukanda wa Pwani inayohusika Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Mafia, visiwa vya Unguja na Pemba, na mikoa ya Lindi na Mtwara kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa.

“Watu wachukue tahadhari. Katika hizi siku mbili (Aprili 28 na 29) kutakuwa na mvua hizo, na Aprili 30 kutakuwa na upungufu wa mvua kubwa katika maeneo hayo," amesema.

Katika mikoa ya Iringa, Pwani na visiwa vya Zanzibar, mvua hizo zimesababisha baadhi ya maeneo kujaa maji na uharibifu wa miundombinu ya barabara na kuleta adha kwa wananchi.


Hali ilivyo

Katika Jiji la Dar es Salaam, mvua zimekwaza mtihani wa darasa la nne kwa baadhi ya wanafunzi waliokwama njiani, kutokana na maji kujaa katika njia wanazopita kwenda shuleni.

Ule usemi wa kufa kufaana umeakisi uhalisia katika mvua hizo, baada ya baadhi ya madereva bodaboda kupandisha nauli mara mbili ya zile walizokuwa wakitoza awali.

Hatua ya kupandisha nauli hizo imetokana na kupungua kwa vyombo vya usafiri, hivyo inamlazimu raia kutumia gharama kubwa, vinginevyo akubali shughuli zake zikwame.

Eneo maarufu kuathiriwa na mvua, Jangwani jijini Dar es Salaam, lilijaa maji kiasi cha usafiri wa umma kuzuiwa kupita tangu saa 3 asubuhi.

Kwa sababu ya hali hiyo, mabasi yaendayo haraka yalilazimika kukatisha safari zake kutoka Mbezi, Kimara, Morocco na kuishia Magomeni Mapipa badala ya Gerezani na Kivukoni.

Kwa upande wa mabasi hayo yaliyotoka Gerezani na Kivukoni, yaliishia Fire, na baada ya hapo abiria alitakiwa kutafuta njia mbadala ya kusafiri anakoelekea.

Bajaji na bodaboda ndivyo vyombo vya usafiri pekee vilivyotumika zaidi mjini, lakini nao walitumia hali ya kuhitajika kwao kama fursa ya kupandisha nauli.

"Nimepanda bodaboda Sh5,000, tena hiyo mnakaa mishikaki (abiria wawili), kila mmoja analipa Sh5,000. Kutoka Mapipa hadi Gerezani bodaboda wanalipisha Sh10,000 kwa abiria wawili," amesema Agripa Amir, mfanyakazi wa moja ya maduka Kariakoo.

Kwa upande wa Jemima Juma, anayeishi Kimara, Dar es Salaam, amesema nauli ya kwenda Kivukoni haikufanikisha safari yake kwa kuwa basi la mwendokasi lililazimika kukatisha safari baada ya maji kujaa.

"Mvua ikinyesha Dar kwa siku ni shida kwenye eneo hili. Kama huna nauli ya ziada, ni changamoto kufika kazini. Kwa sisi tunaopaswa kupita Jangwani ili tufike kazini, mvua kwetu si neema bali kero," amesema.

Nauli ya Sh10,000 iliwatoka Samwel Baraka na wenzake, katika usafiri wa bajaji kutoka Magomeni Mapipa hadi Gerezani.

"Eneo lilikuwa na maji yanayokaribia kufika magotini, lakini bajaji ilipita. Lakini ndiyo hivyo, lazima utumie fedha zaidi ya nauli iliyokuwa kwenye hesabu," amesema.


Daraja la Mto Mzinga lafurika

Daraja la Mto Mzinga, Dar es Salaam, lilijaa maji, huku wakazi wa eneo hilo wakiomba mamlaka kuchukua hatua za haraka kabla ya kutokea maafa zaidi.

Gazeti la Mwananchi lililokuwa eneo hilo lilishuhudia baadhi ya wakazi wakivuka kwa Sh500 hadi Sh2,000 kwa kubebwa mgongoni, huku wenye vyombo vya usafiri wakilazimika kuviacha.

Hakukuwa na uwezekano wa daladala kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Hussein Hamidu, anayefanya kazi ya kuvusha watu eneo hilo, amesema wanafunzi huwavusha bure, huku watu wazima akiwatoza fedha tofauti kulingana na namna anavyomuangalia usoni.

"Hapa unamwangalia mtu. Kuna ambaye unaona hata ukimtajia Sh5,000 ataitoa, lakini kuna wale wa Sh500 na Sh1,000 ambao ndiyo wengi tunawavusha," amesema Hamidu.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Shabani Nassoro, amesema changamoto ya eneo hilo kujaa maji inatokana na udogo wa madaraja.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Zingiziwa, Oliver Osward, amesema hali hiyo inawapa mazingira magumu kufundisha, kwa kuwa wanafunzi wengi hawahudhurii shuleni.

Meshack Nemes, mkazi wa Mtaa wa Ngobedi, amesema amelazimika kuacha gari na kuwavusha watoto wake wanaosoma Chanika Mjini kwa kuwa wana mtihani wa darasa la nne.

"Ingekuwa sio mtihani, nisingewapeleka shule. Hata mimi kazini siendi, na imebidi niache gari nivushwe hapa, kisha nikachukue bodaboda upande wa pili ili kuwasindikiza watoto hadi shule."

Wakati hali ikiwa hivyo Dar es Salaam, katika Mkoa wa Iringa mvua zimeendelea kunyesha kwa wastani, hali inayowaneemesha wakulima kutokana na mazao yao kustawi.


Visiwani Zanzibar

Mvua hizo zinaendelea visiwani Zanzibar tangu jana, Aprili 28 hadi leo, Aprili 29, 2025, zikisababisha usafiri wa umma kuwa mgumu katika baadhi ya maeneo.

Maji yakiwa yametanda eneo la Kariakoo Mjini Unguja kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kisiwani Zanzibar

Licha ya mvua hizo kutosababisha madhara, changamoto kubwa inayojitokeza ni baadhi ya maeneo kujaa maji na wananchi kunyeshewa wakielekea katika shughuli zao.

"Nimelowa mwili mzima nikiwa naenda kazini, maana hata usafiri wa daladala umekuwa shida," amesema Hamrat Chande, mkazi wa Kwerekwe Unguja.


Pwani

Katika Mkoa wa Pwani, mvua hizo zimesababisha kujaa maji kwa baadhi ya mitaa na barabara, ikiwemo ya Msangani kutokea kwa Mfipa.

Mbali na kujaa maji, mvua hizo pia zimesababisha uharibifu wa barabara hiyo na hofu ni kukatika kwa mawasiliano ya barabara hiyo.

"Kimebaki kipande kama nusu ndipo watu wanapita pembeni. Kila mvua zinaponyesha, eneo hilo linameguka," amesema mkazi mmoja.

Jitwae Masatu amesema mvua zinazoendelea zimeharibu miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo na kusababisha gharama za usafiri, hasa wa bodaboda, kuongezeka kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000.


Imeandikwa na Nasra Abdallah na Imani Makongoro (Dar), Christina Thobias (Iringa) na Jesse Mikofu (Zanzibar)