Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TMA yatoa tahadhari wavuvi, wananchi mwambao Ziwa Nyasa

Muktasari:

  • Imeelezwa hii ni wiki ya mwisho kwa mwezi Aprili, huku mvua zikitarajiwa kukatika mwanzoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Mei, huku maeneo ya vijito na mabondeni kutajwa kuwa katika hatari.

Mbeya. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), imetoa tahadhari kwa wavuvi na wananchi waishio mwambao mwa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela mkoani hapa, kufuatia kuwepo kwa vipindi vya mvua za radi na upepo mkali unaoweza kuleta madhara majini.

Pia, imewataka wananchi kutojikinga mvua katika maeneo ya wazi na miti mirefu ili kukwepa athari ya kupigwa na radi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 25, 2025, Meneja wa TMA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elius Lipiki amesema kwa sasa msimu wa mvua uko wiki ya mwisho ya mwezi Aprili zikitarajiwa kukatika mwanzoni mwa Mei, 2025.

"Maeneo Ukanda wa Ziwa Nyasa kutakuwa na vipindi vya mvua za radi na upepo mkali, tuwatake wavuvi na wananchi waishio maeneo vijiji vya pembezoni kuchukua tahadhari kubwa," amesema Lipiki.

Amesema TMA   inaendelea kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari wakiwepo wavuvi pindi wanapoingia majini kwa ajili ya shughuli za uvuvi.

"Nisisitize sana kwa wavuvi kuna uwepo wa mvua za radi ambazo sio salama sana katika shughuli za uvuvi kwani husababisha kuwepo kwa upepo na mawimbi makali majini," amesema.

Wakati huo huo, Lipiki amewataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa za kila wakati na akiwatahadharisha wavuvi kuachana na imani potofu za kutumia njia asili kudhibiti mawimbi na upepo wawapo majini.

Kwa wanaoishi maeneo ya mabondeni amewataka kuchukua tahadhari kufuatia vijito vya maji kuwa kwenye hatari ya kuleta madhara hususani kwa ndani ya mita 60.

"Kuna maeneo mengine hakutakuwa na athari kwani tayari udongo umefyonza maji mengi, lakini maeneo ya mabondeni na kwenye vijito ni miongoni mwa maeneo hatarishi," amesema.


Mvuvi katika mwambao mwa ziwa nyasa eneo la Matema, Festo Wille amesema msimu huu hali ni tete kwani kumekuwa na vipindi vya mvua nyingi ambazo zimesababisha samaki na dagaa kupatikana kwa shida.

"Mwaka huu wa historia kwetu wavuvi kwani dagaa wamepotea na hata samaki wanaopatikana hawaeleweki kabisa na ukiwapata lazima uingie maeneo ya ndani sana ya ziwa," amesema.

Wille amesema kutokana na changamoto hiyo wanaiomba Serikali kuwapa mikopo ya zana za kisasa za uvuvi ili kuwezesha kuondokana na vipindi vigumu walivyopitia.

Mfanyabiashara wa samaki aina ya mbasa, Neema Aloyce amesema kutokana na upatikanaji wake kuwa mgumu wamekuwa wakiuza kati ya Sh15,000 mpaka Sh30,000 kulingana na ukubwa.