Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

42 mbaroni kwa tuhuma za uhalifu Tanga

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 18, 2025. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Kati ya watuhumiwa waliokamatwa, watano wanatuhumiwa kumvamia na kumpora simu mwalimu mmoja wa shule ya sekondari ya jijini Tanga na kumjeruhi.

Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewakamata watu 42 katika operesheni maalumu ya kukabiliana na wahalifu, wanaohusishwa na makosa mbalimbali ya jinai katika maeneo tofauti ya mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu watuhumiwa hao, leo Juni 18, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema watuhumiwa 29 wamekamatwa kwa makosa ya jinai, unyang’anyi wa kutumia nguvu, uharibifu wa mali na mashambulio ya mwili dhidi ya raia.

Amesema sambamba na ukamataji huo, jumla ya pikipiki 28 zimekamatwa, ambapo tisa kati ya hizo hazina namba za usajili, na zinashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kubaini uhalali wa umiliki wake na iwapo zinahusishwa na matukio ya uhalifu.

Lakini pia Polisi wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita waliopatikana na bangi ikiwamo misokoto 47, kete 15, na bunda moja la bangi huku watuhumiwa wengine sita walikamatwa wakiwa na mabunda mawili ya mirungi.

Vilevile, mtuhumiwa mmoja amekamatwa akiwa na mafuta yanayodhaniwa kuwa ya wizi, zikiwemo lita 415 za petroli na l 40 za dizeli.

Kamanda Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina dhidi ya watuhumiwa wote waliokamatwa, na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu, kwa lengo la kuimarisha usalama na amani mkoani Tanga.

Mkazi wa Mtaa wa Lucas, kata ya Sahare, ambaye ni dereva bodaboda, Abubakar Salim amesema yeye ni miongoni mwa waliovamiwa na  vibaka hao wakati akimshusha abiria Jumapili Juni 15, 2025 na wakati akijihami, walimpiga mawe.

Amesema watu hao ubabe virungu, mawe na mapanga na wakikuta raia eneo lolote, hutoa amri ya kutaka wapewe simu na vitu vingine ulivyonavyo na ukikaidi kufanya hivyo ndiyo wataanza kukushambulia.

Kwa upande wake, Fatuma Mhidini amesema kutokana na hali hiyo, inawabidi kujifungia saa 1 jioni kutokana na hofu dhidi ya vijana hao, hivyo kuomba Jeshi la Polisi kuongeza ulinzi zaidi kwenye mitaa yao.

Jeshi la Polisi Mkoa Tanga Oktoba 2021 liliwakamata vijana 117 wanaojiita ‘ibilisi’ kwa tuhuma ya kufanya matukio ya uhalifu katika operesheni iliyofanyika mkoani humo, kwa kushirikiana na wananchi.