Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askari Magereza mbaroni akituhumiwa kumlawiti mtoto wa nduguye

Muktasari:

  • Askari huyo alikamatwa Juni 14, mwaka huu katika Kijiji Cha Rauya, wilayani Moshi baada ya familia kubaini mtoto ametendewa kitendo hicho cha kikatili.

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia askari wa Jeshi la Magereza (jina linahifadhiwa kwa sasa) kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 13, katika moja ya shule zilizopo eneo la Marangu, wilayani Moshi.

Askari huyo alikamatwa Juni 14, 2025, katika Kijiji cha Rauya, wilayani Moshi, baada ya familia ya mtoto huyo kubaini kuwa alikuwa ametendewa kitendo hicho cha kikatili.

Inadaiwa kuwa mtoto huyo, ambaye ni ndugu wa mtuhumiwa, alifanyiwa kitendo hicho Juni 5, 2025 katika shamba la migomba, karibu na nyumbani kwa mtuhumiwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kueleza kuwa taratibu za kinidhamu na kijeshi dhidi yake zinaendelea na zikishakamilika, hatua kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria.

 “Mtuhumiwa amekamatwa taratibu za kitumishi/kijeshi zinaendelea na zitakapokamilika hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake," amesema Mtagwa.

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Rauya, Modest Minja amedai kuwa tukio hilo ni la kusikitisha na linapaswa kulaaniwa vikali.

Minja amedai mtuhumiwa anadaiwa kumuingilia mtoto huyo kwa nguvu, huku akimtishia kumuua endapo angejaribu kumpinga au kutoa taarifa.

Alidai kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho, mtoto huyo alimweleza dada yake, ambaye naye aliwaarifu wazazi wao. Wazazi walimchukua mtoto hadi kituo cha polisi kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.

Baada ya tukio hilo kuripotiwa katika Kituo cha Polisi Himo, walipewa fomu ya matibabu (PF3) na kumpeleka mtoto katika Kituo cha Afya Himo kwa uchunguzi wa kitabibu, ambapo ilibainika kuwa mtoto huyo amelawitiwa.

"Nilipigiwa simu Kituo cha Polisi Himo wakinitaka niende eneo ambalo mtoto huyo alifanyiwa kitendo hicho cha kikatili kwani walitaka pia kufanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa.

"Tuliingia kwenye ukaguzi tukapekua na mwisho wa siku mtoto akaonyesha nguo ambazo mtuhumiwa alikuwa amevaa wakati akimfanyia hicho kitendo, ambapo mtoto alidai kafanyiwa kitendo hicho kwenye migomba karibu na nyumbani kwa mtuhumiwa," alidai Minja.

Minja alidai kuwa "Mtuhumiwa alimwambia huyu mtoto atampa Sh10,000 na pipi kama atamkubalia, kijana alikataa na alipokataa alimwambia atamuua, ndipo huyo mtoto akakubali na fedha hakupewa," ameeleza mwenyekiti huyo.

Aama wa mtoto huyo amevitaka vyombo vya dola kuchukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa, akieleza kuwa kitendo hicho ni cha kikatili na hakipaswi kufumbiwa macho.

"Huyu baba anatuangamizia vijana wetu. Kesho au keshokutwa tutakapokuwa hatupo, watoto wengine watazaliwaje, nao wataishi kwa hofu kama hii? Kama mzazi, tukio hili limeniacha na maumivu makubwa sana," mama huyo ameeleza.

Baba wa mtoto huyo amesema baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, alipatwa na mshtuko mkubwa na kujikuta hajui la kufanya, hasa ikizingatiwa kuwa mtuhumiwa ni ndugu wa familia.

"Huyu ni mtumishi wa Serikali, mimi ni mkulima wa kawaida nitaongea nini? Baada ya kutoka kanisani na kupewa taarifa hizi, hata chai niliyokuwa nakunywa niliiacha. Maana huyu aliyefanya kitendo hiki ni ndugu yangu wa damu kabisa," alisema baba huyo.