Prime
'Mauaji haya yawe mwisho Tanzania'

Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema Taifa, Ally Mohamed Kibao anayedaiwa kutekwa na kuuawa.
Muktasari:
- Wadau na wapenda haki nchini wamepaza sauti wakitaka Rais kuunda tume ya kijaji kuchunguza na kukomesha matukio ya mauaji.
Dar es Salaam. Mauaji ya aliyekuwa kada wa Chadema, Ally Kibao aliyezikwa leo jijini Tanga, yameibua watu mbalimbali, wanaosema matukio hayo yawe mwisho kutokea nchini.
Wamesema licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza mamlaka za uchunguzi zichunguze matukio ya mauaji, uchunguzi huo usihusishe vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa wadau hao wa masuala ya haki, tume maalumu inapaswa kuundwa na mkuu huyo wa nchi itakayohusisha vyombo mbalimbali vya kijamii na kwamba pamoja na matukio hayo, tume itakayoundwa ilichunguze pia Jeshi la Polisi.
Rais Samia alielekeza kufanywa kwa uchunguzi huo, juzi kupitia mitandao yake ya kijamii alipoandika akisikitishwa na tukio la kuuawa kwa Kibao aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi.
"Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” aliandika Rais Samia katika mitandao yake hiyo.
Mzizi wa maelekezo hayo ya mkuu huyo wa nchi ni tukio la kukamatwa kwa Kibao na baadaye kukutwa ameuawa Ununio jijini Dar es Salaam.
Taarifa za uchunguzi kutoka Hospitali ya Mwananyamala, zilibaini kifo chake kilitokana na kipigo na kumwagiwa tindikani usoni.
Mbali na tukio la Kibao, uchunguzi unaozungumzwa na Rais Samia unatarajiwa kuhusisha matukio lukuki, likiwemo la kupotea, kutoweka na kutekwa kwa waandishi wa habari, wanasiasa na wanaharakati nchini.
Agosti mwaka huu, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoa orodha ya watu 83 kiliodai walitekwa, kutoweka na hata kuuawa, jambo lililoiibua Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kusema imeanza uchunguzi.
Uchunguzi huru
Uchunguzi utakaofanywa na chombo huru ndiyo wito ulioonekana kutolewa na wadau wengi kama njia ya kupata jawabu la mwisho la matukio hayo. Ubalozi wa Marekani na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ni miongoni mwa wadau waliotoa wito huo.
Akizungumzia na Mwananchi, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi alisema uchunguzi huo haupaswi kufanya na Jeshi la Polisi kwa kuwa lenyewe ndilo linalotuhumiwa.
Badala yake, alitaka viongozi wa juu wa jeshi hilo wawekwe chini ya uchunguzi, utakaofanywa na tume maalumu itakayoundwa na Rais Samia.
“Tunasema polisi wasichunguze kwa sababu wenyewe ndiyo watuhumiwa namba moja. Mara zote waathirika wametoa ushuhuda wakilitaja jeshi hilo au mazingira yanayolihusisha na matukio hayo,” alisema.
Hata hivyo, Julai 2024, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camlius Wambura alisema polisi hawahusiki na utekaji wa watu au kupotea kwa watu kunakofanywa na watu wasiojulikana.
Kwa mtazamo wa Mwabukusi, tume hiyo itakayoundwa na mkuu wa nchi, inapaswa kuwa na mwakilishi kutoka TLS, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Wawakilishi wengine kwa mujibu wa Mwabukusi ni wanasheria kutoka sekta ya umma, Usalama wa Taifa, huku mwenyekiti wa kamisheni hiyo akiwa kuwa jaji mstaafu wa Mahakama.
“Hao watu watakaoteuliwa wasiteuliwe kwa majina, bali kila taasisi ielekezwe kupeleka jina la mwakilishi wake,” alieleza.
Katika pendekezo lake hilo, Mwabukusi alitaka tume hiyo ipewe siku 60 kutekeleza jukumu hilo la uchunguzi kisha ikabidhi ripoti yake.
Wakati uchunguzi ukiendelea, rais huyo wa wanasheria Tanganyika alisema Serikali itoe tamko la dharura la kutoruhusiwa askari yeyote au kikundi chochote kwenda kukamata mtu bila hati ya mahakama au kiongozi wa serikali za mitaa.
“Kama mtu yupo kwenye chombo cha usafiri, abiria na dereva waruhusiwe kumpeleka mtu huyo kwa pamoja hadi katika kituo cha polisi kilichopo karibu naye,” alisema.
Mtazamo wa wadau wa haki
Mtazamo wa Mwabukusi, haukutofautiana na mwanazuoni wa sheria, Profesa Gamaliel Mgongo-Fimbo aliyetaka kuundwa kwa tume ya kijaji itakayofanya uchunguzi wa jumla.
“Inawezekana wakati polisi wanafanya uchunguzi kuhusu tukio la Kibao, kukawa na chombo kingine cha uchunguzi kwa sababu kuna wanaohisi kwamba watendaji wa mambo haya ni polisi,” alisema Profesa Fimbo.
Hata hivyo, alisema mwenye mamlaka ya uundaji wa tume hiyo ni mkuu wa nchi na kwa utashi wake ndiyo anateua wajumbe na viongozi wa tume husika.
Alisema pamoja na kuundwa kwa tume hiyo, anachotilia shaka ni kuwekwa hadharani kwa ripoti itakayobainika kwa kuwa historia inaonyesha ripoti nyingi zilifichwa.
Kuhusu tukio la Kibao, alitaka uchunguzi utakaofanywa na Polisi uhusishe kuangalia ilikuwaje, hizo gari zilizotumika ni za aina gani.
“Wale walioingia kwenye basi wachunguzwe wote waliokuwepo waliona nini. Alikaa kiti gani na nani na waliokuwepo walisikia nini kutoka kwa aliyekuja na pingu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda alipendekeza kuundwa kwa tume hiyo ya kijaji kwa ajili ya kuchunguza matukio ya utekaji na mauaji.
“Mheshimiwa Rais, Taifa linahitaji tume ya kijaji kuchunguza matukio yote ya utekaji na mauaji,” aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter).
Walichokisema Marekani, TEF
Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Marekani ulisisitiza uchunguzi huru na wa uwazi dhidi ya tukio hilo na mengineyo ya utekaji.
“Mauaji na kupotea kwa watu, kukamatwa na kupigwa havipaswi kuwa na nafasi katika demokrasia,” ilielezwa katika tamko hilo.
Kwa mujibu wa tamko hilo, vitendo hivyo vinadhoofisha haki za kikatiba.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alitoa taarifa ya kulaani tukio la Kibao na kutaka kuundwa kwa tume ya majaji kuchunguza wimbi la utekaji na mauaji.
“Tunamuomba Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aunde tume ya majaji kuchunguza wimbi la utekaji na mauaji, ambalo lilianza kwa mtu mmoja mmoja sehemu mbalimbali nchini, likahamia kwa watoto na sasa watu wanashushwa kwenye magari ya abiria na kuuawa,” alisema.
Jukwaa hilo limekwenda mbali na kusema:“Tunaomba uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika ngazi zote, ujitafakari iwapo unastahili kuendelea kuwapo, wakati tuhuma hizi nzito za watu kutekwa zikiendelea kusikika sehemu mbalimbali nchini.
“Tunao mfano hai wa alichofanya Mzee Ali Hassan Mwinyi mwaka 1976 kwa nia ya kuleta uwajibikaji wafungwa walipouawa kwa kuteswa wakiwa gerezani mkoani Shinyanga.’’
Jaji Werema awapa jukumu wanahabari
Aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisema kabla ya uchunguzi mwingine, vyombo vya habari vinapaswa kuhakikisha vinafanya habari za uchunguzi kubaini mzizi wa tatizo.
“Wanahabari wanapaswa kufanya habari za uchunguzi kubaini sababu za tatizo, kama huyu niliyesikia kwamba amechukuliwa akiwa kwenye basi, uchunguzi wa wanahabari uje na jawabu la kwanini basi lilimwachia abiria wake kwa watu wasiojitambulisha,” alieleza.
Jaji Werema ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema zaidi ya hivyo ni vema wananchi wasubiri uchunguzi ufanyike kama ilivyoelekezwa na Rais Samia kisha itajulikana kinachofuata.
Wito wa kuundwa kwa tume ya kijaji, ulitolewa pia na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo- Bara, Issihaka Mchinjita alisema ni muhimu Rais Samia akaunda tume ya kijaji kuchunguza matukio hayo.
Akiwa katika maziko ya Kibao mkoani Tanga, Mchinjita alisema sababu ya kuundwa kwa tume hiyo, ni kukosekana imani kwa vyombo vya ulinzi na usalama kama vinaweza kuwa sahihi kuchunguza matukio hayo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye aliungana na wadau wengine kutaka tume ya kijaji ichunguze matukio hayo na vyombo vya dola kwa ujumla.
“Wote tumesikia kauli ya Rais jana, lakini kauli ya Rais ambayo inaelekeza vyombo vile vile ambavyo ni watuhumiwa namba moja wakajichunguze wenyewe tunaona hiyo haiwezekani hii nchi haitarekebika.
“Rai ya waombolezaji katika msiba huu, kamwambie Rais yeye pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuunda tume ya kijaji ya kimahakama, ambayo inaweza ikachunguza matukio yote haya na mengine mengi yaliyojificha,” alisema.
Alieleza ni imani yake kuwa, hiyo ndiyo njia pekee itakayowezesha kukomesha vitendo hivyo.
“Sisi ambao tuna ushahidi tutakuwa tayari kueleza mbele ya tume hii,” alisema.