Kikwete ndani ya Sabasaba

Rais Mtaafu Jakaya Kikwete akiwa katika maonyesho ya Sabasaba leo Juli 6, 2023
Muktasari:
- Akiwa kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu na mstaafu, Rais wa awamu ya nne ametembelea maonyesho ya sabasaba huku ujio wake ukikonga mioyo ya watu wengi.
Dar es Salaam. Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete amesimamisha maonyesho ya 47 ya biashara ya Kimatifa ya Dar es Salaam (DITF) baada ya watembeleaji kutumia muda wao mwingi kumshangaa kila alipopita.
Kikwete ambaye alifika katika viwanja hivyo majira ya mchana, aifanya ziara yake katika mabanda mbalimbali ikiwemo lile linalomilikiwa na Anna Mkapa ambaye ni mke wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Akiendelea na ziara yake ndani ya uwanja huo pia alipita katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo yeye ni mkuu wa chuo.
Kila alipoingia katika banda na watu kugundua kuwa yupo ndani walimsubiri nje na alipotoka baadhi walinyenyua simu zao kumpiga picha.
Kutokana na hilo Kikwete alilazimika kupunga mkono kila wakati kuwasalia Wananchi huku akiambatanisha na salamu ya 'Hamjambo'
Kikwete anakuwa kiongozi mkubwa wa kwanza mstaafu kutembelea maonyesho haya tangu yalipofunguliwa rasmi Juni 28, 2023.
Hii si mara ya kwanza yeye kuwapo katika maonyesho haya bali amekuwa na desturi ya kuyatembelea karibu kila mwaka.
Katika ziara anayofanya ndani ya viwanja hivi aliambatana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis.
Aipopata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa Habari, Kikwete alisema maonyesho hayo yameendelea kuimarika kila mwaka na kupendeza.
Amesema maonyesho hayo ya Kimataifa ni fursa ya Tanzania kutangaza kile kilichopo kwa ajili ya kukiuza ndani na nje ya nchi kwani mtu unapozalisha lengo lake huwa ni kupata soko
"Maonyesho haya yanatoa futsa ya soko, ukiwa unatengeneza batiki ukija hapa watu watapita na kuvutiwa wengine watanunua kabisa wengine utaingia nao mkataba uwatengenezee waje kununua nyingi zaidi," alisema Kikwete.
Alisema upande wa Tanzania, waonyeshaji kutoka nje wanapokuja kushiriki, huwa wanasoma fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
"Wanaangalia nini nchini kinapendwa kina soko na wanakwenda kuzalisha kitu ambacho nchini hakizalishwi," alisema Kikwete.