Hivi ndivyo unavyopaswa kuoga

Dar es Salaam. Unafahamu njia sahihi ya kuoga?
Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi, Dk Albane Bosman wa Masaki, Dar es Salaam anasema wakati wa kuoga, mtu aanze kuulowesha mwili na kuupaka sabuni mwili kisha kusuunza maji mwilini.
Anasema kutokana na sababu za kimazingira, inashauriwa kuoga kwa maji machache.
Dk Bosman anasema ni muhimu maji unayotumia wakati wa kuoga yawe na nyuzi joto 37, karibu sawa na kiwango cha joto la mwili.
Kwa afya ya nywele, anasema angalau zisafishwe kwa sabuni maalumu (Shampoo) kila baada ya siku mbili hadi tatu.
Anashauri kama ngozi yako ni ya kawaida, basi tumia sabuni za kawaida zisizo na kemikali au usitumie kabisa sabuni.
“Epuka sabuni za kemikali zenye kukausha sana ngozi, matumizi ya sabuni hizo hayashauriwi kama ngozi haina maambukizi,” anasema Dk Bosman .
Pia, anasema hata ngozi ikiwa na maambukizi haishauriwi kutumia sabuni zenye kemikali.
“Kwa mfano mtu mwenye tatizo la fangasi, sabuni hizo (zenye kemikali) hazina msaada wowote kwao kwa sababu zinawaathiri bakteria salama wanaoilinda ngozi na kuufanya mwili uathiriwe na antibiotiki,” anasema Dk Bosman.
“Bakteria hao wakiondolewa mwilini wanaathiri mfumo wa kinga za mwili, mifumo ya kinga inahitaji kiasi fulani cha msisimko na vijidudu vya kawaida, uchafu na vijidudu vingine vilivyo kwenye mazingira kulinda kinga mwili na kumbukumbu ya kinga mwilini.”
Anasema kuoga mara kwa mara kunaondoa uwezo wa kinga ya mwili kufanya kazi.
Dk Bosman anasema mtu anapaswa kuoga mara moja kwa siku kwa kutumia sabuni na kama atalazimika kuoga kwa mara nyingine asitumie sabuni bali maji pekee ili kuondoa uchafu mwilini.
“Unaweza kuulinda mwili wako zaidi na mambukizi kwa kutumia sabuni isiyo na kemikali kuliko kutumia sabuni zenye kemikali,” anasema mtaalamu huyo wa afya.
“Katika vituo vya afya tunatumia sabuni zisizo na kemikali kuosha mikono na sanitaiza ambayo haina athari kubwa kwenye ngozi na huondoa bakteria.”
Dk Bosman anasema kuoga kwa kujisugua hasa maji yakiwa ya moto kunaondoa bakteria salama ambao hulinda ngozi, jambo linalochangia ngozi kukakamaa, kuwasha au kuwa kavu.
“ozi kavu, iliyokakamaa na yenye michubuko husababisha ngozi kupata maambukizi ya bakteria na mzio (aleji),” anasema Dk Bosman.
Mtaalamu mwingine wa afya, Dk Daniel Magomele anasema wakati unaoga, yapo mambo unapaswa kuyaepuka.
“Usitumie maji (wakati wa kuoga) ambayo ni ya moto sana. Huenda yakaathiri ngozi, mtu anapotumia mara kwa mara maji ya moto wakati wa kuoga anaifanya ngozi kuwa kavu,” anasema Dk Magomele.
Anashauri wakati wa kuoga hupaswi kuacha kuosha uso na muhimu kutumia bidhaa zinazotengezwa kwa ajili ya kuogea.
Dk Magomele anasema dodoki la kuogea linapaswa kuhifadhiwa kwenye eneo safi, kavu na lenye mwanga kwa sababu vifaa hivyo vina uwezo wa kuzalisha bakteria.
Akizungumzia muda ambao mtu anapaswa kuoga, Dk Magomele anasema kwa nchi za Marekani, watu wanatumia dakika nane.
“Kuoga kuanzia dakika tano hadi 10 ni muda sahihi unaoweza kutumia kuoga bafuni na si kukaa zaidi ya hapo,” anasema Dk Magomele.
Namna watu wanavyofanya
Baadhi ya watu wanaoga mara tatu kwa siku hasa maeneo yenye joto kama Dar es Salaam, wengine wanaoga mara mbili, utaratibu unaoelezwa unaweza kuleta madhara.
Hata hivyo, wapo wanaomaliza siku nzima bila kuoga na wengine hukaa siku kadhaa bila kusafisha miili yao.
Kundi hili linatajwa kuwa kwenye hatari pia ya kupata magonjwa ya ngozi yanayosababishwa na joto na uchafu.
Vilevile, watu wanaooga kila siku pia hutofautiana muda wanaoutumia kuoga, wengine wanatumia muda mrefu na wengine mchache katika kufanya usafi wa miili yao.
“Binafsi huwa natumia dakika mbili hadi tatu, sina mambo mengi nikiingia bafuni,” anasema Baraka Baraza wa Dar es Salaam.
“Nikiingia bafuni najimwagia maji, sabuni mwilini, najisuuza nimemaliza, siku nitakayotumia muda mrefu kuoga ni dakika tano, lakini mara nyingi natumia dakika tatu au mbili,” anasema.
Raphael Masatu, mkazi wa Musoma, yuko tofauti kidogo, anapoingia kuoga muda mfupi anaotumia ni dakika 30 na anatumia si chini ya ndoo mbili kubwa za maji.
“Huwa naoga mara moja kwa siku, ratiba yangu ni asubuhi lakini nahakikisha nimejisugua kikamilifu, ninapokuwa bafuni hata familia yangu inafahamu, hivyo hakuna anayekuja kunigongea niharakishe,” anasema Masatu.
Anaamini kuoga ni jamo linalohitaji nafasi na utulivu kama ilivyo kwenye matendo mengine ikiwamo wakati wa kula.
“Huo ndiyo utaratibu wangu, hata nilipokuwa bado mtumishi, sasa hivi nimestaafu, lakini wakati nahitajika kuwahi kazini, nililazimika kuamka mapema na kutumia muda wa kunitosha kuoga ili kujiandaa kwenda kazini,” anasema.
Gladness John wa Morogoro, anasema kuoga kwake si kipaumbele sana, japo anaoga mara moja kwa siku na hana kanuni maalumu ya kumwongoza kuoga.
“Huwa naoga kwa kuwa tunapaswa kuoga, lakini kuna siku napitisha dash (siku inapita bila kuoga), kutegemea na hali ya hewa na ratiba zangu,” anasema Gladness.
Wema Stephano wa Dar es Salaam anaoga mara mbili na wakati mwingine mara tatu kwa siku kutegemea na mazingira na ratiba zake.
“Kama nakwenda kazini, nitaoga asubuhi kabla ya kutoka nyumbani na jioni ninaporudi, lakini nikiwa nyumbani kuna wakati nalazimika kuoga na mchana pia kutokana na joto. Kama hali ya hewa ikiwa ya baridi, nitaoga mara mbili, asubuhi na jioni, utaratibu wangu siku zote nikiwa bafuni naanza kuoga miguu, kisha ndipo nakuja kichwani na maeneo mengine ya mwili.”
Mambo ya kuzingatia
Dk Happyness Biyengo anasema wakati wa kuoga mtu anapaswa kuepuka kuoga kwa muda mrefu kwa kuwa kufanya hivyo ni kuondoa mafuta kwenye ngozi, anashauri muda wa kukaa bafuni usizidi dakika 10.
“Usioge maji ya moto sana, usitumia sabuni za kuua bakteria au kuchubua na hakikisha unaoga vema kwenye maeneo ya kwapani na sehemu za mapajani,” anaeleza.
Kuoga maji ya baridi, moto
Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya Healthline ya Marekani, baadhi ya seli za mafuta kama vile mafuta ya kahawia, zinaweza kutengeneza joto mwilini kwa kuchoma mafuta wakati wa kuoga maji ya baridi.
Kutumia maji ya baridi huenda usiwe sahihi kama mwili unapitia hali ya baridi kwa sababu kutumia maji hayo kunaweza kuufanya mwili kuchukua muda mrefu kupata joto.
Pia, kwa mtu ambaye anaumwa au mwenye msongo wa mawazo si sahihi kutumia maji ya baridi wakati wa kuoga.
Tovuti hiyo ya afya inabainisha kwamba kuoga maji ya moto kunaifanya ngozi kukauka, kuwa na muwasho na kuharibu seli aina ya keratin iliyochini ya ngozi ya mwanadamu.
Pia, kuoga kwa maji ya moto kunaongeza shinikizo la damu, kama mtu ana shinikizo la damu au ugonjwa wa moyo na mishipa, kuoga maji ya moto kunaweza kumfanya kuwa kwenye hali mbaya zaidi.
Hatua za kuoga
Mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Dk Innocent Tesha anasema kuoga kwa usahihi kunapaswa kuanzia kichwani hadi miguuni kwa kusugua vizuri sehemu zote zenye mikunjo kama kwapani, sehemu za siri na maungio ya miguuni.
Anasema wakati wa kuoga unatakiwa kutumia maji ya uvuguvugu japokuwa maji ya baridi na ya moto yana faida na hasara.
“Faida za kuoga maji ya baridi ni kuupoza mwili, kuchangamsha mwili, kupunguza maumivu ya misuli na uzito. Madhara yake humfanya mtu akose au apungukiwe na usingizi,” anasema Dk Tesha.Kuhusu maji ya moto, Dk Tesha anasema husaidia kupata usingizi, hupunguza hali ya mafua, kikohozi, kufungua mapafu na hulainisha misuli.