Wananchi waomba ulinzi wa polisi hofu ikitanda Islamabad
Islamabad. Baadhi ya familia katika mji wa Islamabad nchini Pakistan zimeomba ulinzi wa polisi kutokana na kushamiri kwa matukio ya uvamizi yanayohusishwa na sababu mbalimbali ikiwemo visasi.
Miongoni mwa familia hizo ni ya, Arthur Anthony, mwenye umri wa miaka 70 mmiliki wa hoteli iliyopo eneo la Dhoke Noor Chowk nchini Pakistan ambaye amejeruhiwa kwa risasi katika tukio lililozidisha hofu miongoni mwa wananchi.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimeripoti kuwa matukio ya raia kushambuliwa yanahusishwa na masuala mbalimbali ikiwemo visasi.
Katika maelezo yake, Anthony amesema hoteli yake ilikuwa na wateja wengi na kuna wakati alifuatwa na mtu aliyemlazimisha kuiuza lakini alikataa na kubainisha kuwa huenda suala hilo ndio chanzo cha yeye kupigwa risasi.
Akinukuriwa na vyombo vya habari, amesema kutokana na shinikizo hilo, aliamua kuiuza hoteli hiyo kwa Rupia 90,000 lakini mtoto wa aliyemuuzia hoteli hiyo alilalamika kuwa baba yake anataka kuuziwa hoteli hiyo kwa gharama kubwa.
‘’Siku ya tukio mfanyakazi wa hoteli alifika nyumbani kwangu kunieleza kuwa natakiwa kufika hotelini kwangu kuifunga. Nilipofika yaliibuka mabishano makali kati yangu na aliyetaka kununua hoteli..., wakati tukiendelea na mabishano alitokea kijana mmoja akiwa na pikipiki na amefunika uso na alinipiga risasi,’’ amesema Anthony.
Anthony amesema wakati akiendelea na matibabu hospitali, baadhi ya wafanyakazi wake walimtembelea kumjulia hali na kumueleza kuwa kuna matukio yanatokea eneo hilo yakihusishwa na sababu mbalimbali, watu kadhaa wamejeruhiwa.
Amesema kutokana na kushamiri kwa matukio hayo, familia yake iliomba msaada wa polisi kukomesha matukio mbalimbali yanayoendelea katika mji huo.