Ujumbe wa Papa Francis kwa vijana wa kizazi kipya

Muktasari:
- Hayati Papa Francis Januari 8, 2025 alirekodi ujumbe kwa ajili ya vijana kwenye simu ya Luca Drusian aliyekuwapo katika Hosteli ya Mtakatifu Martha.
Vatican. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano inayowawezesha watu wengi kuwasiliana.
Hata hivyo, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamekuwa chanzo cha kusambaratika kwa mawasiliano katika familia na jamii kwa ujumla.
Padri Richard Mjigwa katika andiko lililochapishwa na mtandao wa Vatican News Aprili 28, 2025 amesema badala ya kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, hakuna tena utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana, watu wamezama katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kiasi hata cha kushindwa kuguswa na mateso na mahangaiko ya wengine.
Katika hilo, amesema kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kuhudumiana katika huruma na upendo. Majadiliano ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa daraja la watu kukutana.

Ni katika muktadha wa kuwataka vijana kujifunza utamaduni wa kusikiliza ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani duniani, Januari 8, 2025 hayati Papa Francis alirekodi ujumbe kwenye simu ya Luca Drusian aliyekuwapo katika Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya.
Hayati Papa Francis aliwaambia vijana kwamba: “Kati ya mambo msingi katika maisha ni watu kujifunza utamaduni wa kusikiliza kwa kumwachia nafasi jirani yako azungumze kabla ya kumkatisha, lengo ni kufahamu kikamilifu ujumbe anaotaka kukupatia.”
Luca Drusian anajihusisha na ujenzi wa maabara ya utamaduni wa kusikiliza, mradi unaowahusisha vijana wa kizazi kipya na wazee, lengo likiwa ni kujenga utamaduni utakaowasaidia kutambua uzuri wa kusikilizwa, kusikiliza na hatimaye kusikia.
Papa Francis katika ujumbe huo alisikika akisema leo hii watu wengi hawana utamaduni wa kusikiliza kiasi kwamba wanapenda kuingilia na kuwakatiza watu wengine wasiendelee kuzungumza, jambo hili ni hatari kwa muktadha wa ujenzi wa utamaduni wa kisikiliza.
Kwa namna ya kipekee aliwataka vijana wa kizazi kipya wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini.