Kardinali Becciu ajiondoa rasmi kwenye uchaguzi wa Papa mpya

Muktasari:
- Kardinali Giovanni Angelo Becciu ametangaza uamuzi huo kwa kuthibitisha kwamba licha ya kuamini hana hatia yoyote, ameamua kutii utashi wa Kanisa.
Vatican. Mwadhama Kardinali Giovanni Angelo Becciu wa Sardegna hatashiriki katika mkutano wa uchaguzi wa Papa mpya (Conclave) unaotarajiwa kuanza Jumatano, Mei 7, 2025, huko Vatican.
Kardinali Becciu ametangaza uamuzi huo kwa kuthibitisha kwamba licha ya kuamini hana hatia yoyote, ameamua kutii utashi wa Baba Mtakatifu Francis kwa ajili ya masilahi ya Kanisa.
“Nikiwa na moyo wa wema wa Kanisa, ambalo nimelitumikia na nitaendelea kulitumikia kwa uaminifu na upendo, pamoja na kuchangia ushirika na utulivu wa mkutano wa uchaguzi, nimeamua kutii, kama nilivyofanya siku zote, mapenzi ya Baba Mtakatifu Francis ya kutoingia kwenye mkutano wa uchaguzi wa Papa mpya, huku nikiendelea kusadiki kwamba sina hatia,” amesema Kardinali huyo kupitia taarifa.

Hatua ya Becciu kujiondoa inakuja wakati Kanisa Katoliki likijiandaa kwa mkutano muhimu wa uchaguzi wa kiongozi mpya wa Kanisa hilo baada ya nafasi hiyo kuwa wazi. Uamuzi wake unatajwa kama jaribio la kulinda mshikamano na utulivu katika kipindi hiki nyeti kwa Kanisa.
Baada ya kifo cha Papa Francis mnamo Aprili 21, 2025, Kanisa Katoliki linaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa papa mpya kupitia mchakato wa conclave, ambao utaanza rasmi Mei 7, 2025, katika Kanisa la Sistine, Vatican.
Tuhuma dhidi ya Becciu
Kardinali Becciu amewahi kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya Vatican, akihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Naibu wa Masuala ya Ndani wa Vatican (Sostituto) katika Sekretarieti ya Jimbo. Aliteuliwa kuwa Kardinali mwaka 2018 na Papa Francis.

Hata hivyo, aliingia hatiani mwaka 2020 baada ya kuhusishwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za Kanisa, hususan ununuzi tata wa jengo la kifahari jijini London kwa kutumia fedha za misaada kutoka kwa waumini.
Tuhuma hizo zilimlazimu Papa Francis kumwondoa Becciu katika wadhifa wake wa Mkuu wa Idara ya Watakatifu na pia kumpokonya haki ya kushiriki katika mikutano ya uchaguzi wa Papa.
Becciu amekuwa akikanusha tuhuma hizo mara kwa mara na kusisitiza kuwa hana hatia, akieleza kuwa amekuwa mhanga wa mazingira na maamuzi ya kisiasa ndani ya Vatican.

Mwaka 2021, alifikishwa mahakamani pamoja na washtakiwa wengine kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha, udanganyifu na rushwa, lakini kesi hiyo imekuwa ikiendelea huku baadhi ya mashitaka yakiondolewa au kuwekewa masharti mapya.
Kwa uamuzi huu wa sasa, Becciu anakuwa Kardinali wa kwanza wa ngazi ya juu kujiondoa rasmi kwenye Conclave kwa hiari, ikiwa ni hatua isiyo ya kawaida katika historia ya Kanisa Katoliki.
Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa Vatcan News