Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Israel yazidi kushambulia Iran, Trump ataka ijisalimishe

Dar es Salaam. Maelfu ya watu wameanza kukimbia kutoka Tehran na miji mingine mikuu nchini Iran, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Hatua hiyo inakuja wakati Iran na Israel zikiendelea kushambuliana kwa makombora licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuitaka Iran ijisalimishe bila masharti.

Jeshi la Israel limeripoti kwamba mafungu mawili ya makombora kutoka Iran yalirushwa kuelekea Israel katika saa mbili za mwanzo za alfajiri ya leo. Milipuko ilisikika juu ya anga la Tel Aviv.

Israel iliwataka wakazi wa maeneo ya Kusini-Magharibi mwa Tehran wahame haraka ili kuruhusu mashambulizi ya anga dhidi ya kambi za kijeshi za Iran.

Maelfu ya watu wameonekana wakikimbia kutoka mji mkuu na miji mingine mikubwa, huku barabara zikifurika magari na baadhi ya njia kufungwa, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Iran.

Shirika la habari la Mehr, ambalo kwa sehemu ni la serikali, limearifu kwamba kulitokea mapigano kati ya vikosi vya usalama na watu wasiojulikana wenye silaha katika jiji la Rey, kusini mwa Tehran, na kuongeza kuwa washambuliaji hao huenda wana uhusiano na Israel na walikuwa na lengo la kufanya mashambulizi ya kigaidi katika maeneo yenye watu wengi.

Tovuti za habari za Iran zinaripoti pia kuwa Israel ilikuwa inashambulia chuo kikuu kinachohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mashariki mwa Iran

Pia kituo cha makombora ya masafa marefu cha Khojir kilicho karibu na Tehran, ambacho pia kililengwa na mashambulizi ya Israel mwezi uliopita.

Ofisa mmoja wa jeshi la Israel alisema kwamba ndege 50 za kivita zilishambulia maeneo 20 jijini Tehran usiku kucha, ikiwa ni pamoja na maeneo ya kuzalisha malighafi, vipuri na mifumo ya kutengeneza makombora.

Ofisi ya Mkurugenzi wa ujasusi wa kitaifa wa Marekani imesema kuwa Iran ina idadi kubwa zaidi ya makombora ya masafa marefu Mashariki ya Kati.

Iran kwa upande wake imesisitiza kuwa makombora hayo ni silaha muhimu ya kuzuia na kujibu mashambulizi kutoka Marekani, Israel na mahasimu wengine wa ukanda huo.

Jana Jumanne Juni 17,2025, Rais Trump alionya kupitia mitandao ya kijamii kwamba uvumilivu wa Marekani unakaribia kufikia mwisho.

Alisema hana mpango wa kumuua Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei kwa sasa, lakini kauli zake zilionesha mwelekeo mkali zaidi dhidi ya Iran, huku akitafakari iwapo aongeze ushiriki wa Marekani katika vita hiyo.

“Tunajua wapi haswa huyo anayejiita kiongozi mkuu amejificha,” aliandika katika mtandao wa Truth Social. “Hatutamtoa ‘kuua’ angalau si kwa sasa ... uvumilivu wetu unakaribia kufikia mwisho.”

Dakika tatu baadaye, Trump aliandika: “Jisalimishe bila masharti!”

Kauli za Trump mara nyingine huwa zinakinzana au hazieleweki kuhusu mzozo huu kati ya Israel ambaye ni mshirika wake wa karibu na Iran, hasimu wake wa muda mrefu zimezidisha sintofahamu.

Kauli zake za hadharani zimekuwa zikisita kati ya vitisho vya kijeshi na ishara za kidiplomasia, jambo ambalo si geni kwa rais huyu mwenye mtazamo wa pekee kuhusu siasa za nje.

Chanzo kimoja kilicho karibu na majadiliano ya ndani kimesema kuwa Trump na timu yake wanachunguza uwezekano wa kushirikiana bega kwa bega na Israel katika mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Ofisa mmoja wa Ikulu ya White House alieleza kuwa Juni 17,2025, Trump alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Aidha, alikutana kwa dakika 90 na Baraza la Usalama la Kitaifa kujadili mzozo huo, ingawa maelezo ya kikao hicho hayakuwekwa wazi mara moja.

Maofisa watatu wa Marekani waliiambia Reuters kuwa nchi hiyo inapeleka ndege zaidi za kivita katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza muda wa kuwapo kwa ndege nyingine zilizotangulia.

Hadi sasa, Marekani imekuwa ikichukua hatua za moja kwa moja tu kama kusaidia kuzuia makombora yaliyokuwa yakiilenga Israel.

Chanzo chenye taarifa za kiintelijensia ya Marekani kilisema kuwa Iran imehamisha baadhi ya mitambo ya kurushia makombora ya masafa marefu, ingawa haikuwa wazi kama inalenga vikosi vya Marekani au Israel.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, akizungumza kwenye mkutano wa kilele wa mataifa saba tajiri zaidi duniani (G7), unaofanyika Canada ambao Trump aliondoka ghafla akisema hakuna dalili kuwa Marekani inajiandaa kuingia vitani moja kwa moja.

Nguvu za kanda zadhoofika

Wasimamizi wakuu wa masuala ya kijeshi na usalama wa Khamenei (Kiongozi Mkuu wa Iran),  wameripotiwa kuuawa na mashambulizi ya Israel, jambo lililovuruga duru ya karibu ya ushauri wake na kuongeza hatari ya makosa ya kimkakati, hiyo imesemwa pia na watu watano walio karibu na mchakato wa uamuzi wake.

Mashambulizi hayo, ambayo ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa viongozi wa Iran tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, yamefanya mamlaka ya usalama wa mitandao nchini humo kuzuia maofisa kutumia simu na vifaa vya mawasiliano, kwa mujibu wa shirika la habari la Fars.

Tangu kundi la Hamas linaloungwa mkono na Iran liliposhambulia Israel Oktoba 7, 2023 na kusababisha vita vya Gaza, ushawishi wa Khamenei katika ukanda umepungua sana, huku Israel ikishambulia vikali vikundi vinavyoungwa mkono na Iran, kuanzia Hamas huko Gaza hadi Hezbollah nchini Lebanon, waasi wa Houthi Yemen na makundi ya wanamgambo nchini Iraq. Hata mshirika wake wa karibu Rais wa Syria, Bashar al-Assad ameshindwa kudhibiti mamlaka yake.

Israel ilianzisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya Iran ambayo ni makubwa zaidi katika historia Ijumaa iliyopita baada ya kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa karibu kuunda silaha ya nyuklia.

Iran inakanusha madai kuwa inataka kutengeneza silaha za nyuklia na inasisitiza haki yake ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani, ikiwemo uboreshaji wa nishati, kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), wa kimataifa ambao ni mwanachama wake.

Israel ambayo si mwanachama wa mkataba huo, inaaminika kuwa taifa pekee Mashariki ya Kati lenye silaha za nyuklia japo haijawahi kuthibitisha wala kukanusha hilo.

Netanyahu amesisitiza kuwa hatarudi nyuma hadi maendeleo ya nyuklia ya Iran yatakapodhibitiwa kabisa, huku Trump akieleza kuwa mashambulizi ya Israel yanaweza kusitishwa iwapo Iran itakubali vikwazo vikali vya kiufundi dhidi ya uboreshaji wa nyuklia.

Kabla ya mashambulizi ya Israel kuanza, bodi ya magavana wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) lenye wanachama 35, kwa mara ya kwanza ndani ya karibu miaka 20, ilitangaza kuwa Iran imekiuka masharti ya mkataba wa NPT.

Shirika hilo lilieleza kuwa shambulio la Israel liligonga moja kwa moja maeneo ya chini ya ardhi katika kituo cha nyuklia cha Natanz.

Israel imesema sasa inadhibiti anga ya Iran na inatarajia kuongeza mashambulizi zaidi katika siku chache zijazo.

Hata hivyo, Israel itakuwa na kazi ngumu kulenga kwa mafanikio vituo vya nyuklia vilivyochimbwa chini ya milima kama Fordow, bila msaada wa moja kwa moja kutoka Marekani.

Maofisa wa Iran wameripoti vifo vya watu 224 wengi wao wakiwa raia huku Israel ikisema raia wake 24 wameuawa. Masoko ya mafuta duniani yameingiwa na taharuki kufuatia mashambulizi katika maeneo muhimu kama South Pars (eneo kubwa zaidi la gesi duniani). Eneo hili lipo kwenye Ghuba ya Uajemi (Persian Gulf), ambalo linamilikiwa kwa pamoja na Iran na Qatar.