Ajali za mabasi zaua 15, zajeruhi 13 Kenya

Daladala likiwa limeharibika baada ya kugongana na basi nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu 15, leo Januari 9, 2024.
Muktasari:
- Ajali iliyohusisha basi na daladala leo Jumanne asubuhi kwenye barabara kuu ya Nakuru kwenda Eldoret nchini Kenya imesababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi wengine 13.
Kenya. Watu 15 wamefariki katika ajali iliyotokea leo, Jumanne Januari 9, 2024 asubuhi kwenye barabara kuu ya Nakuru kwenda Eldoret nchini Kenya, ikihusisha basi na daladala.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Star ya nchini humo, waliofariki katika ajali hiyo ni watu wazima wanane na watoto saba wakiwemo wasichana watano.
Kwa mujibu wa Polisi nchini humo, abiria wengine 38 waliokuwa kwenye basi wamenusurika kwenye ajali hiyo huku wenzao 14 waliokuwa kwenye daladala, wamepoteza maisha.
Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia zaidi ya watu 20 katika ajali tofauti ndani ya siku mbili, kama ilivyoripotiwa na polisi.
Tukio hilo lilitokea saa 2:45 asubuhi katika eneo la Twin Bridge, ambapo basi la kampuni ya ‘Classic Kings of Congo’ limegongana na daladala ya ‘North Ways Shuttle.’
Polisi wamethibitisha kuwa watu wote waliokuwa kwenye daladala walipoteza maisha, huku abiria watatu wa waliokuwa kwenye basi, wamepata majeraha wengine kumi wakipata majeraha madogo.
Polisi walifika eneo la tukio mara moja na kusaidia kuwapeleka majeruhi katika Hospitali ya Molo huku Kamanda wa Polisi wa Bonde la Ufa, Tom Odero amesema kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea.
"Ilikuwa asubuhi nyingine ya kusikitisha ambapo tumepoteza watu 15. Wengine wamejeruhiwa na wako hospitalini,” amesema.
Pia Odero ametoa wito kwa madereva kuchukua tahadhari wawapo barabarani ili kuzuia ajali za barabarani.
Takwimu za polisi zinaonyesha zaidi ya watu 40 wamefariki katika ajali tofauti nchini humo mwaka huu pekee.