Afariki wakati wakifanya mapenzi kichakani

Muktasari:

  • Mwanamke mmoja amefariki dunia akiwa anafanya mapenzi na mwanaume anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake, umauti ulimkuta baada ya kuingia kwenye kichaka kwa ajili ya kushiriki tendo hilo huku wakiwa wamelewa.

Kenya. Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 37 anakabiliwa na mashtaka ya mauaji baada ya mpenzi wake aliyefahamika kwa jina moja la Milca (48) kufariki dunia wakati wakifanya mapenzi kichakani eneo la Mbita katika Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya.

Tukio hilo limetokea jioni ya Jumapili ya Machi 19 mwaka huu baada ya wapenzi hao waliokuwa wanarejea nyumbani kuamua kuingia kwenye kichaka eneo la Got Rateng kwa ajili ya kufanya kitendo hicho walipokuwa wametoka kunywa pombe, tovuti ya TUKO imeripoti.

Chifu wa eneo hilo amesema kuwa wawili hao  awali walikuwa wameonywa wasishiriki tendo wakiwa wamelewa lakini hawakutii, mshtakiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini humo baada ya kukiri chanzo cha kifo hicho.

Inasemekana mwanaume huyo amemrithi Milca baada ya kifo cha mume wake kama ilivyo utamadumi wa wakazi wa eneo hilo, ambapo mwanamke anaruhusiwa kurithiwa pale mumewe anapofariki.

“Baada ya kifo cha Milca alijaribu kuuzika mwili wake na ndipo tukamkamata mshtakiwa,” amesema Chifu Bernard Ouma.

Ameongeza kwa kusema, "Kuna wakati niliwaita na kuwaonya kuhusu kufanya mapenzi sehemu zisizo na staha hasa baada ya kunywa pombe, waliendelea na ninafikiri hilo linaweza kuwa chanzo cha maafa haya."

Mwili wa marehemu umepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay huku uchunguzi zaidi ukiendelea.