Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safari ya kumchagua Papa mpya yaanza, bomba la kutolea moshi lasimikwa

Muktasari:

  • Papa Francis, alifariki dunia Aprili 21, 2025 akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta, na kuzikwa Aprili 26, 2025 katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu mjini Roma, nchini Italia, takriban kilometa 5.2 kutoka Vatican.

Roma. Maofisa wa Zimamoto katika Mji wa Vatican wamesimika bomba la kutolea moshi juu ya paa la Kanisa la Sistine, ikiwa ni ishara ya hatua ya mwisho kuelekea kuanza kwa mkutano wa kumchagua Papa mpya.

“Kikosi cha zimamoto mjini Vatican tayari kimesimika bomba la moshi litakalotangaza uchaguzi wa Papa mpya,” imeeleza taarifa ya Vatican ya leo Ijumaa, Mei 2, 2025.

Bomba hilo, lililowekwa juu ya paa la kanisa, sasa linatarajiwa kuanza kutoa moshi mweusi mara mbili kwa siku kuanzia kesho Jumamosi asubuhi, kuashiria kuwa Papa mpya bado hajapatikana – isipokuwa Mei 7, 2025 ambapo uchaguzi wa kiongozi huyo wa kiroho unatarajiwa kufanyika.

Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican, moshi mweusi unaashiria kuwa kura zilizopigwa hazijafikia mwafaka wa kumpata Papa mpya. Ikitokea limeanza kutoa moshi mweupe, ni ishara kuwa mrithi wa Papa Francis amepatikana.

“Moshi utapanda asubuhi (isipokuwa Mei 7) na jioni,” wameeleza maofisa wa Vatican.

Moshi mweupe ukiinuka, inamaanisha kuwa angalau makadinali 89 wamekubaliana kuhusu nani atakayeongoza Kanisa Katoliki, wakiwa wamefikia theluthi mbili ya kura zinazohitajika.

Kikao cha uchaguzi kinatarajiwa kuanza Mei 7, mwaka huu ambapo makadinali (wapiga kura) 135 – wote wakiwa chini ya umri wa miaka 80 – watakusanyika ndani ya kanisa hilo lenye michoro ya enzi ya Renaissance, kuchagua mrithi wa Papa Francis, aliyefariki Aprili 21 akiwa na miaka 88.

“Makadinali watakusanyika katika Kanisa la Sistine Mei 7 kuanza kikao cha kumchagua Papa ajaye,” taarifa ya Vatican imeeleza.

Kikao hicho kinatarajiwa kuwa kikubwa zaidi katika historia ya kisasa ya Kanisa, kikiwa kielelezo cha upana wa ushawishi wa kimataifa na mwelekeo wa mageuzi uliowekwa na utawala wa miaka zaidi ya 11 wa Papa Francis.

Kati ya makadinali 135 wapiga kura, 108 waliteuliwa na Papa Francis, na jumla ya nchi 71 zinawakilishwa  ikionyesha Kanisa lenye utofauti zaidi kuwahi kutokea.

Ushawishi wa Papa Francis umejidhihirisha hasa katika juhudi zake za kugatua mamlaka ya Vatican, kufungua milango ya mazungumzo na jamii zilizotengwa, na kuinua nafasi ya wanawake katika uongozi wa Kanisa.

Miongoni mwa mambo yatakayokumbukwa kwa Francis ni pamoja na uteuzi wa (sista) Simona Brambilla na (sista) Raffaella Petrini katika nafasi kuu za Vatican ingawa hawatakuwa na haki ya kupiga kura katika kikao hiki  ambao umeweka mwelekeo mpya kwa uongozi wa Kanisa.

Miongoni mwa majina yanayofuatiliwa kwa karibu kuwa huenda akachaguliwa kuwa mrithi wa Francis ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin wa Italia, Katibu wa Vatican anayejulikana kwa umahiri wake wa kidiplomasia; Kardinali Matteo Zuppi, mwenye msimamo wa wastani na mpatanishi wa kimataifa; Kardinali Fridolin Ambongo Besungu (65) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC); Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson (76) kutoka Ghana; na Luis Antonio Tagle wa Ufilipino – kiongozi mwenye mvuto mkubwa anayeonekana kama sauti ya Kusini ya Dunia na ambaye aliwahi kupewa nafasi kubwa ya kuwa Papa.

Mvutano bado upo kati ya wahafidhina wanaotilia shaka mageuzi ya Francis na wanaopenda maendeleo zaidi.

Hata hivyo, wachambuzi wanapendekeza kuwa mkutano huo wa makardinali huenda ukampendelea mgombea anayeweza kuziba pengo hilo – Papa atakayedumisha dira ya Francis, huku akiwatuliza wahafidhina kuhusu uthabiti wa mafundisho ya Kanisa.

Kwa sasa, Kanisa la Sistine limefungwa rasmi.

Makadinali wataapa kutunza siri kabla ya kupiga kura chini ya mchoro wa Hukumu ya Mwisho wa Michelangelo.

Huko nje, dunia inasubiri, macho yote yakiangazia bomba dogo la moshi ambalo linaweza, wakati wowote, kutangaza kiongozi mpya wa Wakatoliki takriban bilioni 1.3 duniani.

Moshi mweupe utakaoonekana ukitokea kwenye bomba hilo utaambatana na tangazo la Habemus Papam kuashiria kuwa hatma ya uchaguzi huo imefikiwa kwa kiongozi mpya wa Wakatoliki duniani kupatikana.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.