Hali si hali Kenya, Afrika ya Kusini maelfu wakiandamana

Jeshi la Polisi nchini Kenya lna lile la Afrika Kusini limekianza kibaru akigumu cha kukabiliana na maandamano ya raia yaliyoanza jana katika mikoa yao tofauti.

Nchi hizo mbili zilikumbwa na maandamano ya kitaifa yaliyoitishwa na vyama vya upinzani kushinikiza unafuu wa maisha na hali bora ya uchumi.

Nchini Kenya, maandamano hayo yaliripotiwa katika kaunti tofauti kama vile Bungoma, Nakuru, Kisumu, Mombasa na Nairobi ambako waandamanaji walikabiliana vikali na askari polisi waliotawanywa kuwadhibiti.

Waandamanaji waliweka vizuizi barabarani pamoja na kuchoma matairi jambo lililowalazimu polisi kupiga mabomu ya machozi ili kuviondoa vizuizi hivyo huku mamia ya vijana waliojitokeza wakikamatwa.

Kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga aliyeshindwa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022, aliapa kwamba maandamano hayo yataendelea hadi Serikali itakaposikiliza madai yao.

“Ninataka Wakenya wajitokeze kwa wingi na kuonyesha kukerwa na yanayoendelea nchini mwetu,” alisema Odinga.

Alisema Wakenya wanateseka kutokana na kupanda kwa bei ya mahitaji ya msingi sambamba na kushuka kwa kasi kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani bila kusahau athari za ukame ambao umewaacha mamilioni ya watu wakikosa chakula.

Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi, Adamson Bungei alisema walipokea maombi ya maandamano mawili mwishoni mwa Jumamosi na mapema Jumapili wakati kwa kawaida taarifa ya mkutano wa hadhara inatakiwa kutolewa siku tatu kabla.

“Kwa usalama wa umma, hakuna chochote kilichotolewa,” alisema.

Barabara zilikuwa tulivu kuliko kawaida jijini Nairobi jana Jumatatu na nyingi zimefungwa kabla ya maandamano hayo kuanza huku waajiri wakiwaambia wafanyakazi wao wafanyie kazi nyumbani.


Mabomu yapigwa

Saa tisa alasiri jana, msafara wa Odinga na viongozi wa Azimio la Umoja walipigwa mabomu ya machozi lakini wafuasi wake waliendelea kusonga mbele huku wakiwarushia polisi mawe.

Akizungumza na wafuasi wake, Odinga alisema kila Jumatatu watakuwa wakiandamana nchi nzima hadi Serikali itakapotekeleza matakwa yao.

“Vita vimeanza, haitaisha mpaka Wakenya wapate haki yao. Mko tayari?” aliuliza Odinga na wananchi walioandamana waliitikia kwa pamoja “tuko tayari.”

Akiwa Mombasa, naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua alimtaka Odinga kumaliza maandamano hayo kwa sababu yanaathiri uchumi wa Kenya kwani kwa jana pekee, yamepoteza zaidi ya Ksh2 bilioni (takribani Sh70 bilioni).

Wakati Gachagua akisema hayo, kiongozi wa wachache katika Bunge la Seneti la Kenya, Stewart Madzayo na mwenzake wa Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi na wabunge kadhaa walikamatwa jana jijini Nairobi.


Hali ilivyo Afrika Kusini

Huko Afrika Kusini, polisi na wanajeshi walisambazwa mtaani kabla ya kuanza kwa maandamano baada ya Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kutoa wito wa “kulisimamisha Taifa” na kuzua hofu ya kurudiwa kwa machafuko yalisababisha vifo miaka miwili iliyopita.

Mamlaka zilisema ziko katika hali ya tahadhari kuzuia na kupambana na vitendo vyovyote vya uhalifu huku Bunge likitangaza kuwa Rais Cyril Ramaphosa aliidhinisha kutumwa kwa wanajeshi 3,474 kuwasaidia polisi.

“Tunatumaini kwamba wale ambao watakuwa wakiandamana, watafanya hivyo kwa amani, hatuna sababu ya kuwaingilia. Polisi itabidi wawe imara bila kuwa wakatili,” alisema Bheki Cele, waziri wa Mambo ya Ndani alipozungumza na waandishi wa habari jijini Johannesburg.

Takriban waandamanaji 87 walikamatwa huku barabara za jijini Pretoria na Johannesburg zikiwa kimya na magari machache tu yakipita mtaani. Maduka mengi yalifungwa na kampuni jijini Pretoria iliyaondoa magari yote yanayokuwapo kwenye madirisha ya duka lake (display) kwa hofu ya maandamano hayo.