Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wasisitiza Afrika kuunganisha nguvu kufungua fursa za nishati

Muktasari:

  • Wataalamu wa nishati wamesema ipo haja ya kuungana ili kuharakisha maendeleo na kuboresha upatikanaji wa umeme barani Afrika.

Cape Town. Wataalamu wa nishati wamesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuunganisha nguvu kama mkakati muhimu wa kukabiliana na changamoto sugu za nishati na kufungua fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Wakizungumza katika Mkutano wa Nishati Afrika (Africa Energy Forum) unaoendelea jijini Cape Town, Afrika Kusini, ambao unahudhuriwa na washiriki takriban 6,000 wakiwemo viongozi kutoka sekta mbalimbali za nishati, wamesema ipo haja ya kuungana ili kuharakisha maendeleo na kuboresha upatikanaji wa umeme.

Mkutano huo wa siku nne ulianza Jumanne Juni 17, 2025 na umewakutanisha maofisa wa Serikali kutoka mataifa mbalimbali, wawakilishi wa sekta binafsi, taasisi za kikanda na wadau wengine ili kujadili suluhisho la pamoja chini ya kaulimbiu ‘Africa United’.

Balozi wa zamani wa Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa ajili ya Muungano wa Miundombinu ya Kijani Afrika, ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Uchumi, Mipango na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Senegal, Amadou Hott, alisema mshikamano ni jambo la msingi katika kusukuma mbele ajenda ya nishati barani Afrika.

“Miradi ya pamoja ya usambazaji umeme (power pools) imefanya kazi vizuri na ni mfano bora wa ushirikiano wenye mafanikio,” amesema Hott.

Amezitaka serikali za Afrika kutumia masoko ya mitaji ya ndani, mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na taasisi za fedha za maendeleo kama njia ya kuhamasisha rasilimali za uwekezaji katika miradi ya nishati.

Aidha, amewahimiza wawekezaji kupunguza masharti ya kifedha na kuziomba serikali kuongeza bajeti za sekta ya nishati pamoja na kuruhusu marekebisho ya viwango vya bei ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Mkutano huo pia unalenga kuimarisha sauti ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa kuhusu ajenda ya nishati, hususan kuelekea vikao vya G20 ambavyo mwaka huu vitafanyika Afrika Kusini.

Waziri wa Umeme na Nishati wa Afrika Kusini, Kgosientsho Ramokgopa, amesisitiza kuwa miradi ya kikanda kama vile mifuko wa miundombinu na miradi ya pamoja ya usambazaji umeme ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea biashara baina ya nchi za Afrika.

Ametaja mradi wa kuunganisha umeme kati ya Zambia na Tanzania (Zambia–Tanzania Interconnector) kama mfano mzuri wa ushirikiano wa kikanda unaolenga kuimarisha uhakika wa nishati.

“Afrika ina rasilimali nyingi; ndiyo maana tunaamini bara hili litakuwa kinara wa nishati duniani katika siku zijazo,” alisema Ramokgopa, akisisiza uwekezaji na maboresho.

“Hatujakusanyika hapa kwa ajili ya sherehe wala hotuba tupu, bali kutafuta matokeo. Tukifanikiwa kuvutia uwekezaji sahihi na kutekeleza mageuzi ya maana, Afrika inaweza kuwa kitovu cha nishati duniani,” ameongeza.

Amesisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), huku akionya kuwa utekelezaji wa miradi ya nishati unapaswa kuakisi hali halisi ya kijamii na kiuchumi ya bara la Africa.

Kamishna wa AU anayehusika na Miundombinu na Nishati, Lerato Dorothy Mataboge, naye alisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kwa maendeleo ya haraka.

“Bara hili lazima lichukue hatua kwa pamoja kukabiliana na changamoto za nishati na maendeleo kwa ujumla,” amesema, akiahidi kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama kuhimiza mwelekeo wa pamoja katika mabadiliko ya nishati.