Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msamaha wa kodi kwenye mitungi gesi ya kupikia, ni hatua nzuri

Matumizi ya gesi ya kupikia yanaendelea kuongezeka hapa nchini, hasa kwa matumizi ya nyumbani, biashara, na maeneo mengine. Huu ni mwenendo chanya unaoashiria hatua kuelekea matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa mkaa ili kuepuka athari za kimazingira na kiafya.

Hata hivyo, changamoto inayojitokeza ni bei ya mtungi wa gesi, wengine huona bei yake kujaza tena ni kubwa kuilipia kwa mkupuo mmoja wakilinganisha na uwezo wa kipato chao, hivyo kushindwa kumudu kuendelea kutumia nishati hiyo baada ya gesi kuisha mtungini.

Katika bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 iliyosomwa hivi karibuni bungeni, miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa matanki ya kuhifadhia pamoja na mitungi ya gesi ya kupikia.

Lengo la Serikali ni kupunguza gharama ya upatikanaji wa vifaa hivyo na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa mtazamo wa haraka, hatua hii ni ya kupongeza. Kusamehe VAT kwa mitungi kwa kuwa inaweza kusaidia kufikia lengo la kushusha gharama za upatikanaji wa gesi.

Kwanza, ni muhimu kuelewa kwamba kusamehe VAT kwa bidhaa hizo ni uamuzi mzuri katika kushusha bei ya mitungi ya gesi na gharama kwa upande wa uhifadhi wa gesi hiyo.

Kwa tafsiri yangu, hatua hii inaweza kuleta ahueni ya gharama kwa wachakataji na viwanda hasa katika hatua ya awali ya mnyororo wa usambazaji gesi, kwa kuwa itawapunguzia gharama za kununua, kuagiza na kutumia vifaa vya kuhifadhia gesi.

Vilevile, hatua hiyo inaongeza uzito katika hatua ya awali ya kuondoa VAT kwenye gesi yenyewe. Kwa maneno mengine, kifaa (yaani mtungi) pamoja na gesi iliyomo ndani yake, vyote kwa sasa vina msamaha wa VAT.

Uzoefu katika mazingira yetu ya kila siku unaonesha kuwa hata wale ambao tayari wanamiliki mitungi ya gesi ya kupikia majumbani, mara nyingi huishia kurejea kutumia kuni au mkaa pindi gesi inapoisha, kutokana na ugumu wa kumudu gharama ya kujaza tena gesi hiyo.

Hata hivyo, kuna mambo kadhaa yangeweza kusaidia msamaha huo wa VAT kuweza kuleta tija nzuri zaidi;

Kwanza, ili kuharakisha upatikanaji wa gesi ya kupikia kwa bei nafuu, utekelezaji wa misamaha, upangaji bei, usimamiwe na kudhibitiwa ili kweli nafuu ifike kwa haraka kwa mtumiaji wa mwisho.

Pili, upatikanaji wa nishati safi ya kupikia si suala la bei pekee. Ni muhimu kupanua miundombinu ya usambazaji wa gesi hadi maeneo ya nje ya miji.

Kwa sasa, matumizi ya gesi yamejikita zaidi mijini. Hata bei ikishuka, kama huduma haijawafikia wengi, tija inayokusudiwa kwa kiasi fulani bado haitawagusa vizuri walengwa ambao ni wananchi.  Jambo hili linaweza kusisitizwa zaidi katika mpango wat aida wa matumizi ya nishati salama.

Tatu, elimu kwa umma ni muhimu. Baadhi ya watu bado hawatambui vizuri madhara ya kiafya na kimazingira yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa, au wengine wana hofu ya usalama wanapotumia gesi, nk. Hii inahitaji kampeni madhubuti za kuelimisha na uhamasishaji.

Kwa kumalizia, msamaha wa VAT kwa mitungi na matanki ya gesi ni hatua na chanya ya kisera. Lakini mafanikio yake yatategemea kama hatua hiyo itaambatana na sera jumuishi zitakazogusa utelekezaji wa upangaji na kudhibiti bei ya gesi kwa wazalishaji, kuboresha usambazaji wake na kutoa elimu kwa umma. Ili kusaidia nishati safi ya kupikia kupatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu, na kutumika kwa wingi na Watanzania wote.