Nafuu ya kodi kwenye mitungi ya gesi yawakosha wadau

Dar es Salaam. Pendekezo la Serikali la kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mitungi ya gesi ya kupikia imetajwa kama hatua muhimu katika kuhakikisha Watanzania wengi, hasa wasiokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, wanatumia nishati safi ya kupikia.
Juni 12, 2025 akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali ya 2025/2026 Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba alipendekeza kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye matanki na mitungi ya gesi ya kupikia yanazotambulika kwa HS Code 7311.00.10.
Msamaha huo wa VAT umewekwa pia kwenye mitambo ya kuondoa hewa ukaa yenye HS Code 8417.80.00 inayotumika katika uzalishaji wa mikaa mbadala.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu msamaha huo unalenga kupunguza gharama za upatikanaji wa bidhaa hizi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
“Licha ya kuwa hili litapunguza mapato ya Serikali kwa Sh1.9 bilioni, hatua hii itapunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambao husababisha uharibifu wa misitu na athari za kiafya kutokana na moshi unaotokana na nishati hizo,” alisema.
Akifafanua msamaha kwenye gesi ya kupia, Waziri alieleza utofauti baina ya mitungi ya kuhifadhia gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) na mitungi ya gesi ya kupikia ya Liquified Petroleum Gas (LPG) ili kuendana na ajenda ya kimataifa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Tathmini iliyofanyika imebaini kuwa, kutokana na ukuaji wa teknolojia, hakuna mitungi ya kuhifadhia gesi asilia iliyoshindiliwa kwa ajili ya kutumika kama nishati ya kupikia,”alisema Dk Mwigulu.
Alisema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia, unaolenga kuongeza matumizi ya nishati safi kufikia asilimia 80 ya kaya zote ifikapo mwaka 2034.
Novemba 1, 2022 katika kongamano la kwanza la kitaifa la nishati safi ya kupikia, Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kuanzishwa kwa kikosi kazi kitakachoshughulikia nishati safi ya kupikia ili kuanzisha safari ya kulitoa taifa kwenye matumizi ya nishati isiyofaa kupikia.
“Nitajisikia fahari ikifika 2032 Tanzania hii iwe na nishati ya kupikia kwa asilimia hizo hizo 80, 90 kama siyo zote. Huko tutafika kwa kuwa na mpango mkakati ambao utatoa motisha, ruzuku ya uwekezaji katika utafiti, teknolojia. uvumbuzi, ubunifu na uhamasishaji matumizi ya nishati safi,” alisema Rais Samia.
Takwimu zinaonyesha takribani Watanzania 22,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya upumuaji yanayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia.
Maoni ya wadau
Akizungumzia hatua hiyo, Emmy Mfikwa, mwananch anayemiliki mgahawa, amesema inalenga kupunguza gharama za mitungi ya gesi hali itakayowezesha Watanzania wengi kumudu nishati hiyo.
“Kwa namna moja au nyingine naona tunapiga hatua, tulianza kuona kampeni za kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni lakini sasa inakwenda kwenye vitendo kuondoa kodi ya ongezeko la thamani ni wazi bei zile za awali za gesi inayohusisha na mtungi zitapungua.
Kwa upande wake Rogatus Moshi ambaye ni mdau wa mazingira amesema kupunguza gharama ya mitungi ya gesi ya kupikia si tu suala la bei, bali ni uwekezaji katika ustawi wa jamii, afya ya wananchi na maendeleo endelevu ya taifa.
“Kupunguza gharama za mitungi ya gesi ya kupikia ni hatua muhimu kiuchumi, kijamii na kiafya. Bei ya juu ya gesi ya kupikia ina athari kubwa kwa kaya za kipato cha chini, ambazo ndizo nyingi katika jamii zetu.
“Gesi ya kupikia ni mbadala bora wa kuni na mkaa ambao hutumika kwa wingi, lakini husababisha uharibifu wa mazingira na athari za kiafya kutokana na moshi. Hivyo hatua za namna hii zinapaswa kuwekewa nguvu kuhakikisha utekelezaji wake unawagusa wananchi wa kawaida kabisa,” amesema Moshi.
Mtalaamu wa uchumi, Dk Gibson Kihalala amepongeza hatua hiyo na kushauri jitihada ziendelee kufanyika kuhakikisha nishati ya gesi ya kupikia inapatikana kwa gharama nafuu zaidi, ili wananchi wengi waweze kuimudu.
Amesema upatikanaji wa gesi kwa bei nafuu huongeza mahitaji na matumizi, jambo ambalo linaweza kuchochea uwekezaji zaidi katika miundombinu ya usambazaji na uzalishaji wa gesi, pamoja na kuongeza ajira katika sekta hiyo.
“Wananchi wengi hutumia sehemu kubwa ya mapato yao kwa mahitaji ya msingi kama chakula na nishati. Kwa kupunguza gharama ya gesi, familia zitakuwa na uwezo wa kuokoa fedha kwa ajili ya matumizi mengine ya msingi kama elimu na afya.
“Pia bei ya chini ya gesi itawavutia watu wengi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni, hali ambayo itasaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza ukataji wa miti.,” amesema Kihalala
Amesema katika familia nyingi, wanawake ndio wanaobeba jukumu la kupika na kwa kutumia gesi ya kupikia badala ya kuni au mkaa, huokoa muda mwingi na huweka afya zao salama.