Mambo matano yaibuliwa uchambuzi wa mapendekezo ya bajeti

Muktasari:
- Mambo hayo yamebainishwa siku moja baada Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, kuwasilisha mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni jijini Dodoma Alhamisi ya Juni 12, 2025.
Dar es Salaam. Wadau wa uchumi na kodi nchini wamechambua mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kupanua wigo pamoja na uwepo ufanisi madhubutu wa usimamizi katika kodi.
Mengine waliyoshauri ni bima ya usafiri kwa wageni wanaoingia nchini iangaliwe upya, mifumo ya utoaji risiti ili kusaidia usimamizi na kuongeza mapato pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kumsaidia mlipakodi kuweza kulipa kwa wakati bila kupata changamoto.
Wadau hao wamebainisha hayo siku moja baada Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba. Huwasilisha mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni jijini Dodoma Alhamisi ya Juni 12, 2025.
Jana Juni 13, 2025 wadau wa uchumi na kodi walichambua mapendekezo ya bajeti hiyo katika mkutano ulioandaliwa na kampuni ya Mahesabu na Ushauri wa kodi nchini ya ERNST & Young (EY), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Sekta binafsi Tanzania ( TPSF), Raphael Maganga amesema bajeti hiyo imelenga kuwa jumuishi na shirikishi hasa kwa sekta binafsi.
"Imetoa matumaini katika eneo la kulinda viwanda vya ndani kukua, ikipunguza bidhaa kutoka nje hasa katika zile bidhaa zinazozalishwa nchini," amesema.
Amesema katika kulinda viwanda vya ndani, mapendekezo hayo yatafungua fursa za ajira kwa Watanzania, "ukiagiza bidhaa kutoka nje ya nchi mnyororo wa thamani anzia huko, lakini tukizalisha hapa unaanzia hapa hapa."
Maganga ameshauri kuwa: “Kama nchi tunapaswa tuwe na wigo mpana wa kukusanya kodi, wigo huo ulikuwa mdogo sana, katika mwaka ujao wa fedha tunategemea wigo utapanuka na ukusanyaji kodi utafikia malengo."
Kuhusu tathimini ya bajeti, Wakili Freddy Rugangila amesema bajeti hiyo inajaribu kuijengea nchi uwezo wa kujitegemea yenyewe hususani nyakati hizi ambazo wahisani wa kimaendeleo wanabadilisha sera zao mbalimbali akiitolea mfano Marekani.
Rugangila ambaye ni meneja mwandamizi wa idara ya kodi wa kampuni EY amegusia namna bajeti inavyokwenda kuongeza wigo wa nchi kujitegemea.
Amesema mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko ya sheria za kodi ambayo yanaongeza wigo wa kodi kama yakitekelezwa, Taifa litapata mapato kutokana na shughuli za ndani na kuweza kugharamia wenyewe baadhi ya miradi mikubwa.
"Bajeti hii ni ya kwanza katika Dira ya Maendeleo ya 2050, tumeona vyanzo mbalimbali vimependekezwa, ikiwa katika utekelezaji inawezekana kama taifa kusonga mbele," amesema.
Amegusia moja kati ya mapendekezo yaliyopo katika sheria za kodi hususani katika sheria za usimamizi wa kodi na kushauri mifumo ya utoaji risiti uunganishwe na mifumo ya TRA ili kutasaidia usimamizi na kuongeza mapato.