Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bajeti 2025/2026 yagusa sanaa, wadau watofautiana

Muktasari:

  • Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Juni 12, 2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alieleza kuwa serikali inalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa vijana wengi wanaojihusisha na muziki, filamu, usanii wa jukwaani na mitindo, kwa kuweka mfumo shirikishi wa tozo unaozingatia hali halisi ya soko la sanaa.

Katika kile kinachoonekana kuwa neema mpya kwa sekta ya burudani nchini, Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka wa fedha 2025/2026, imeweka kipaumbele katika kuwawezesha wasanii na wadau wa sanaa kwa kupunguza ada, kufuta baadhi ya tozo na kurahisisha mazingira ya kazi kwa wabunifu wa ndani.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Juni 12, 2025, alieleza kuwa serikali inalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa vijana wengi wanaojihusisha na muziki, filamu, usanii wa jukwaani na mitindo, kwa kuweka mfumo shirikishi wa tozo unaozingatia hali halisi ya soko la sanaa.


Wasanii binafsi wapunguziwa ada

Miongoni mwa hatua kubwa ni kupunguza ada ya usajili kwa wasanii binafsi kutoka Sh20,000 hadi Sh10,000, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha urasimishaji wa kazi zao na kuwawezesha kufaidika na fursa za mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.

Ada ya Studio na DJs imebaki palepale, lebo zapewa unafuu

Lebo za muziki sasa zitalipa Sh100,000 badala ya Sh500,000 zilizokuwa zimependekezwa awali, huku studio za muziki zikiendelea kulipa ada ya Sh50,000. DJ’s pia hawajaguswa, wakibaki na ada ya Sh40,000 kwa mwaka.


Wabunifu na wapambaji sasa kurasimishwa

Kwa mara ya kwanza, serikali imeanzisha ada za usajili kwa wapambaji wa harusi, wapigapicha, wabunifu wa picha (graphic designers) pamoja na MCs na mameneja wa wasanii, kwa lengo la kutambua mchango wao katika uchumi wa ubunifu na kuwatambua rasmi kama sehemu ya sekta inayochangia mapato ya taifa.


Muziki wa kidijitali wafunguliwa mlango mpya

Kwa upande wa teknolojia, kampuni zinazotoa huduma za kusambaza muziki kidijitali (digital music platforms) zimewekewa ada ya usajili ya Sh200,000 kwa kampuni za ndani, na hadi Sh2 milioni kwa kampuni za nje ya nchi. Hii inalenga kudhibiti ushindani usio wa haki na kuongeza mapato ya ndani kupitia kazi za wasanii wa Tanzania.


Safari za wasanii kwenda nje sasa bila ada

Serikali pia imefuta ada ya Sh50,000 kwa wasanii wazawa wanaokwenda nje ya nchi kwa shughuli za sanaa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha wasanii kuchangamkia masoko ya kimataifa na kuitangaza Tanzania kupitia kazi zao.

Branding ya kazi za sanaa yapunguziwa makali

Katika hatua nyingine, ada iliyokuwa ikitozwa kwa kampuni zinazotumia kazi za wasanii katika matangazo au promosheni imefutwa kabisa, hatua ambayo inatazamiwa kuchochea ushirikiano kati ya wasanii na sekta ya biashara.


Wadau watoa ya moyoni

Akizungumzia kuhusu kurasimishwa kwa wabunifu mbalimbali wakiwemo washereheshaji , MC maarufu nchini Gara B, amesema kuwa kwa eneo hilo Serikali ni kama imechelewa kwa namna moja ama nyingine kwa sababu wao mpaka sasa wanatambulika kupitia Baraza la Sanaa la Taifa na wanalipa kodi kama ambavyo wafanyabiashara wengine wanavyofanya, “ Ni vyema Serikali ingetushirikisha na wadau wa sekta husika ili kuweza kupata kitu ambacho kitaleta manufaa kwa pande zote,” amesema Gara B.

Kwa upande wake Mwanamuziki wa kike anayekuja kwa kasi XOUH, alisema kwamba yeye anaona sawa kupunguzwa kwa ada ya wasanii binafsi kutoka 20,000 hadi 10,000 kwa mwaka  huku akisema kwamba italeta unafuu kwa wasanii kuingia kiwango hicho kwenye mambo yao mengine hasa ya uzalishaji.

Mtazamo wa tofauti kutoka kwa Mwanamuziki wa Hip Hop nchini, One The Incredible akisema kuwa kinachotakiwa si kupunguza baadhi ya gharama kwenye tasnia ya muziki kwani kinachoenda kufanyika ni kuongeza mzigo wa mamlaka husika kutatua na kuendesha kiwanda cha muziki nchini.

“Kinakachofanyika ni hatua nyingi kurudi nyuma na sio kwenda mbele, kiwanda chetu cha muziki hakina matatizo tu ya fedha ila ni matatizo ya mfumo mbovu, kwa hiyo kuweka au kupunguza gharama haisaidii kama huo mfumo hautafanyiwa kazi, lazima tupate sehemu moja inayoweza kusimamia kila kitu ambapo kila mmoja ambaye anahusika na muziki awe anapitia humo” amesema One.


Kauli ya Serikali

“Serikali inaamini kuwa kazi za wasanii si burudani tu, bali ni ajira, biashara na dira ya utambulisho wa taifa. Tunapunguza mzigo wa ada ili kuwawezesha vijana na wabunifu kutumia vipaji vyao kuinua maisha yao na pato la Taifa,” alisema Dk Nchemba