Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima Iringa wageukia teknolojia ya kukausha tumbaku kwa jua

Muktasari:

  • Wakulima hao wameeleza kuwa pamoja na changamoto ndogo za hali ya hewa, njia ya jua imethibitika kuwa ya gharama nafuu, rafiki kwa mazingira na rahisi kuitumia.

Iringa. Teknolojia mpya ya kukausha tumbaku kwa njia ya jua imeanza kuleta mapinduzi makubwa kwa wakulima wa tumbaku mkoani Iringa, ambapo sasa wakulima wanaripoti kupungua kwa gharama za uzalishaji.

Vilevile, wakulima wanaeleza kuwepo kwa ongezeko la ubora wa mazao yao huku mazingira yakinusurika kutokana na kupungua kwa matumizi ya kuni.

‎Wakizungumza na Mwananchi leo Juni 26, 2025, wakulima hao wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya gharama za ununuzi wa kuni kwa ajili ya kukaushia tumbaku pamoja na athari kwa mazingira kutokana na uharibifu wa misitu, lakini kwa sasa teknolojia hiyo mpya imeleta matumaini mapya na mwelekeo endelevu katika kilimo hicho.

‎“Hatuamini kilimo chetu kingekuwa rafiki wa mazingira hivi,” amesema mkulima, Juma Mbilinyi. Mkulima mwingine kutoka Kijiji cha Ndolela kilichopo Wilaya ya Iringa, Pius Mbinda ameeleza kwamba:

‎“Kila mwaka tulikuwa tunalazimika kununua magunia ya kuni kwa gharama kubwa, lakini sasa tunatumia nishati ya jua kukausha tumbaku zetu na gharama zimepungua sana,” amesema Mbinda.

‎Wakulima hao wameeleza na kulinganisha tofauti ya kukausha tumbaku kwa kutumia jua na njia ya mvuke na moshi, huku wakisema kuwa teknolojia ya kukaushia tumbaku kwa jua, ambayo ni njia mpya kwa maeneo yao, imeleta mapinduzi ya kweli ikilinganishwa na mbinu walizozizoea awali za kukaushia kwa mvuke na moshi.

‎Wakulima hao wameeleza kuwa pamoja na changamoto ndogo za hali ya hewa, njia ya jua imethibitika kuwa ya gharama nafuu, rafiki kwa mazingira na rahisi kuitumia.

‎“Kwanza kabisa, njia ya jua haina moshi wala hitaji la kuni na ni tofauti kabisa na njia ya moshi ambayo tulilazimika kukata miti mingi na kutumia kuni nyingi lakini sasa hivi tunatumia mabanda yenye dari maalumu, tunaweka tumbaku ndani, tunafungua hewa na jua linakausha polepole,” amesema Selina. Mbwana, mkulima wa zao la tumbaku wilayani Iringa.

‎Wakulima hao wamesema kuwa katika njia ya mvuke, ilikuwa vigumu kudhibiti joto na unyevu, jambo ambalo lilisababisha tumbaku kuharibika mara kwa mara.

‎“Mvuke ukiwa mwingi, tumbaku huloana badala ya kukauka lakini kwenye njia ya jua, joto ni la asili, tunachohitaji ni kuhakikisha tunawekewa paa lenye uwezo wa kuachia mionzi lakini kuzuia mvua hakuna gharama ya mafuta wala kuni,” amesema.

‎Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha IMU Kiwere wilayani Iringa ameeleza kwamba mafanikio ya teknolojia hiyo ni ya kushangaza kwani imewawezesha wakulima kama yeye kupata faida zaidi huku wakilinda mazingira.

‎“Tangu tuanze kutumia njia hii mpya, tumeokoa zaidi ya asilimia 60 ya gharama za kukausha na tumbaku inakaushwa haraka na kwa ubora wa hali ya juu,” amesema Mbinda huku akiongeza kuwa:

“Kwa kweli hii ni suluhisho ambalo tulilitamani kwa muda mrefu na tunaiomba serikali iendelee kuhamasisha matumizi ya teknolojia hii kwa wakulima wote nchini.”

‎Meneja wa Bodi ya Tumbaku Mkoa wa Iringa, Mohamed Kifunko ameiambia Mwananchi kuwa mfumo huo wa kukaushia zao hilo kwa njia ya jua ni suluhisho la kudumu linaloshughulikia changamoto za muda mrefu kwenye sekta ya tumbaku, huku ukilenga kuongeza tija, kulinda mazingira na kuendana na malengo ya kitaifa ya kutumia nishati safi.

‎“Wakulima wa Iringa sasa wanauza tumbaku iliyo na ubora wa juu sokoni kwa sababu teknolojia hii inasaidia kuhifadhi ladha, rangi, na uzito wa majani ya tumbaku,” amesema Meneja Kifunko na kuongeza kuwa: “Njia hii inawapa wakulima bei nzuri sokoni na ni mapinduzi ya kweli kwenye sekta hii.”

‎Naye Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Iringa, Daniel Mlay amesema kuwa tofauti na mbinu ya zamani, njia hii mpya ni salama zaidi, inahifadhi muda, inazuia ajali za moto na inatoa nafasi kwa wakulima kupanua shughuli nyingine za kilimo.

‎“Mbali na kuwa salama kwa mazingira, njia ya juu inapunguza ajali za moto, inaongeza uzalishaji kwa sababu wakulima hawatumii muda mwingi kutafuta kuni na hii inawapa nafasi ya kuwekeza muda wao kwenye shughuli zingine za kilimo,” amesema Mlay.

‎Ofisa Mlay ameongeza kuwa teknolojia hiyo pia imerahisisha usimamizi wa ubora wa mazao shambani na kutoa fursa kwa wakulima kupatiwa mafunzo ya kisasa ya uendelezaji wa kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.

‎Vilevile, wakulima wengi wanaeleza kuwa mafanikio haya yamewapa matumaini makubwa na kuona kuwa serikali iko makini kuwasaidia wakulima wadogo kwa vitendo.‎

‎Kwa sasa, Bodi ya Tumbaku kwa kushirikiana na maafisa ugani na wadau wengine inatekeleza mpango wa mafunzo kwa wakulima wengi zaidi ili kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi.