RC Ruvuma atoa maelekezo kukamilika stendi ya Lundusi

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kanali Ahmed Abbas akizindua stendi mpya ya mabasi kijiji cha Lindusi
Muktasari:
- Ujenzi wa stendi hiyo umegharimu zaidi ya Sh686.3 milioni
Songea. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuimarisha ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya stendi ya kisasa ya mabasi ya Lundusi.
Ujenzi wa stendi hiyo umegharimu zaidi ya Sh686.3 milioni. Kanali amesema maagizo hayo yanalenga kuhakikisha mradi huo unaleta tija kwa wananchi kwa kuondoa kero ya kusafiri umbali mrefu na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Agizo hilo amelitoa leo Jumatano Julai 2, 2025, wakati akiuzindua mradi huo uliofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Kanali Abbas amesema utekelezaji wa miradi ya Tasaf ni sehemu ya mkakati wa kupambana na umaskini.
Katika awamu ya pili ya utekelezaji wake, Tasaf imejikita katika kuwezesha kaya kunufaika na fursa za kiuchumi, kuongeza kipato kwa walengwa na kuboresha huduma za afya, elimu, maji safi na salama sambamba na miundombinu ya kukuza uchumi katika ngazi ya jamii.
“Mradi huu wa ujenzi wa stendi ya mabasi na maduka ya biashara ni sehemu ya miundombinu itakayosaidia kukuza uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
“Nitoe rai kwa viongozi na wananchi wote kuhakikisha miundombinu hii ya stendi ya mabasi inatunzwa ili iweze kuleta tija kwa wananchi na halmashauri kwa ujumla, kuondoa kero ya usafiri, kutoa eneo bora la kuegesha magari, sehemu za biashara ndogondogo na kuongeza kipato cha kaya na jamii,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amemshukuru pia aliyekuwa mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama kwa juhudi zake za kupambania maendeleo kwa wananchi sambamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf na timu yake ya wataalamu, kwa ufuatiliaji kwa karibu wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrak Mziray amesema mradi huo uliombwa na Kijiji cha Lundusi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea huku ikihusisha miradi mitano.
“Tunafurahi kukuarifu kwamba miradi yote mitano imekamilika na kuhakikiwa na wataalamu wa halmashauri na ipo tayari kutoa huduma kwa wananchi. Kwa sababu hiyo, Tasaf imetoa vyeti vyote vya kukamilika kwa miradi hii kulingana na taratibu na masharti ya kisekta,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Willman Ndile amesema tayari viwanja 20,000 vilivyo jirani na stendi hiyo vimepimwa na kuuzwa.
Ndile amesema stendi hiyo itawaunganisha wasafiri wanaokwenda Nyasa na nchi jirani ya Msumbiji, ambako tayari soko la mazao la kimataifa limejengwa.
Aidha, amesema wamepanga kupeleka maombi Tasaf kwa ajili ya kujenga stendi nyingine mpakani mwa Msumbiji, eneo la Mkenda.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Marry Makondo ameishukuru Serikali kwa kupeleka miradi ya maendeleo mkoani humo, akiahidi kuhakikisha miradi iliyobaki inakamilishwa kwa wakati.
Raphael Haule mwananchi wa eneo hilo, amesema stendi hiyo itarahisisha safari za kwenda mikoa mbalimbali na kutoa ajira ya biashara kwa wananchi waishio jirani.