Vodacom ilivyoingiza matrilioni katika uchumi wa Tanzania

Muktasari:
- Kwa jumla, kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh4.5 trilioni kwenye miundombinu na huduma, huku zaidi ya Sh3 trilioni zikitumika katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kupanua mtandao wake unaofikia zaidi ya asilimia 95 ya Watanzania.
Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Kampuni ya Vodacom Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Taifa na kuinua maisha ya wananchi kupitia uwekezaji wa kihistoria, huduma za kisasa, ajira na miradi ya kijamii.
Kwa jumla, kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh4.5 trilioni kwenye miundombinu na huduma, huku zaidi ya Sh3 trilioni zikitumika katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kupanua mtandao wake unaofikia zaidi ya asilimia 95 ya Watanzania.
Kampuni hiyo inaeleza kuwa uwekezaji huu umewezesha uzinduzi wa teknolojia za kisasa kama vile 4G na 5G na kupanua upatikanaji wa intaneti ya kasi hadi kwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi.
Kupitia jukwaa lake la kifedha la M-Pesa, Vodacom imetambulisha huduma bunifu kama Songesha, M-Koba, malipo ya wafanyabiashara, pamoja na huduma za kijamii kama Nipige Tafu na kumgawia mwingine bando (Share the Bundle with your loved ones). Huduma hizi zimesaidia kurahisisha maisha ya Watanzania na kuwawezesha kifedha.
Kwa upande wa ajira, Vodacom imesaidia zaidi ya watu 270,000 kupata kipato kila siku kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, wakiwemo mawakala wa M-Pesa, wasambazaji na baadhi ya watoa huduma.
Idadi hiyo haijawaweka waajiriwa wa kampuni nyingine zinazotoa huduma kama za minara, usafi wa majengo, kampuni za magari ambazo zimepewa mikataba na Vodacom. Hilo limeongeza mchango wake katika kupunguza ukosefu wa ajira na kukuza uchumi wa ndani.
“Kwa miaka minane mfululizo, Vodacom imetambuliwa kama mwajiri bora na kwa miaka 13 hakujawahi kuripotiwa kifo cha mfanyakazi kazini,” alisema Vivienne Penessis, Mkurugenzi wa Raslimali Watu katika kampuni hiyo.
Kupitia Taasisi yake ya Vodacom Foundation, kampuni hiyo imetekeleza miradi kadhaa ya kijamii kwa ushirikiano na taasisi kama Vodafone Foundation, CCBRT, USAID na Serikali.
Miradi ya mfano ni pamoja na m-mama inayopunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga kwa kutoa usafiri wa dharura, pamoja na e-Fahamu, jukwaa la elimu mtandaoni linalowafikia maelfu ya wanafunzi bila gharama kwa wateja wa Vodacom. Miradi hiyo imesaidia kuboresha maisha ya zaidi ya watu milioni 10 nchini.
Kwa sasa, Vodacom inatawala soko la huduma za simu asilimia 31.9 ya wateja wote na ni miongoni mwa kampuni zilizo mstari wa mbele katika usalama wa mtandao, ikitunukiwa cheti cha kuwa "Data Processor and Controller" chini ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022.
Mafanikio haya yanatokana na uwekezaji wa kudumu katika 'mtandao, ubunifu' na teknolojia salama na kukuza vipaji vya vijana katika usalama wa mtandao hivyo kuifanya kampuni hiyo kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wa Taifa.