Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vodacom Plc yatuzwa kwa kuimarisha ulinzi taarifa binafsi za wateja

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa kampuni ya huduma za mawasiliano ya Vodacom Plc, Athuman Mlinga (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Katibu wa Chama cha kitaaluma cha kimataifa cha Ukaguzi na Udhibiti wa Mifumo ya Habari (Isaca), Rosevita Majani wakati mkutano wa chama hicho jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Kampuni ya huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc imetambuliwa kuwa moja ya taasisi za mawasiliano zinazozingatia ulinzi wa taarifa binafsi za wateja na kuahidi kuendelea kuimarisha mifumo yake.

Arusha. Kampuni ya huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc imetambuliwa kuwa moja ya taasisi za mawasiliano zinazozingatia ulinzi wa taarifa binafsi za wateja,  na mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Akikabidhi tuzo hiyo leo Junia 12, 2025 wakati wa mkutano wa kila mwaka wa chama cha kitaaluma cha kimataifa cha Ukaguzi na Udhibiti wa Mifumo ya Habari (Isaca) jijini hapa, Rais wa chama hicho, Peter Kisa Baziwe amesema kampuni ya Vodacom imejizatiti kwa kuweka wataalamu wa kuhakiki mfumo mara kwa mara kama upo salama.

Amesema wapo wataalamu wengi wenye uwezo wa kufahamu na kutengeneza mifumo lakini sio wote wanaweza kuilinda isishambuliwe na watu wenye nia ya kuchukua taarifa muhimu kwa ajili ya kuzitumia kwa malengo yasiyo mazuri.

“Niwapongeze Vodacom kwa kuwa mbele ya jambo hili muhimu, nasi wataalamu tutaendelea kuhakikisha taarifa binafsi zinalindwa kwa masilahi mapana ya nchi yetu, taasisi zetu na familia zetu kwa sababu dunia imebadilika kulingana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano,”amesema Baziwe.

Ameongeza kuwa chama hicho kitaendelea kuwajengea uwezo wanachama wake kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na kutoogopa changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo, bali kuzielewa na kuendelea kuzitumia kutokana na kuwa na manufaa mapana.

Mkurugenzi wa Tehama kutoka Vodacom, Athuman Mlinga akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo amesema wanashirikiana na Isaca kutoa ujumbe muhimu unaozingatia ulinzi wa taarifa binafsi za wateja na usalama wa kimtandao.

“Vodacom ikiwa taasisi inayotoa huduma za mawasiliano ipo mstari wa mbele kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi za wateja na usalama wa kimtandao unapewa kipaumbele, tumeendelea kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndaki ya Tehama kuwajengea umahiri katika usalama wa mitandao,”amesema Mlinga

Mlinga amefafanua kuwa Vodacom itaendelea kuwekeza kwenye maendeleo ya kidijitali nchini na kujenga mazingira wezeshi ya kuweka mifumo ya mitandao imara inayotumia teknolojia za kisasa, ili kuhakikisha wakati wowote wanaenda kwa kasi kutumia mifumo ya kiteknolojia.

Aidha ameongeza kuwa suala la usalama wa taarifa za wateja ni moja ya vipaumbele kutokana na kampuni kuchakata taarifa nyingi za wateja wao na kuwa mifumo yao kila mara inajengwa katika mazingira yanayojali na kuthamini ulinzi wa taarifa binafsi, na kuzuia aina yeyote ya udukuzi.