Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vodacom yajivunia haya safari ya miaka 25 Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Phillip Besiimire akizungumza wakati wa madhimisho ya kutimiza miaka 25 ya kampuni ya Vodacom nchini katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Kampuni ya  kwa mara ya kwanza iliingia nchini mwaka 2000, tangu wakati huo imekuwa ikiongoza kwa kutawala soko la idadi ya wateja wa simu pamoja na wale wa huduma za miamala.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesema inajivunia ubunifu katika huduma za mawasiliano nchini tangu kuanzishwa kwake miaka 25 iliyopita.

Katika safari hiyo ya miaka 25 sasa Vodacom imesema inajivunia ufikiaji wa wananchi katika huduma za miamala zilizoanza mwaka 2008, sambamba na huduma za intaneti ya kasi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 10, 2025 wakati hafla ya kampuni hiyo kusherehekea miaka 25 tangu kuanza kwake kwa huduma nchini Tanzania, makao makuu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire amesema wataendelea kuwaunganisha Watanzania katika nyanja za mawasiliano, fedha na dijitali kama walivyofanya miaka 25 iliyopita.

“Vodacom tumekuwa tukiunganisha watu kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila mwaka kwa miaka 25.  Tumeunganisha watu katika biashara na wadau mbalimbali kwenye jamii.  Tumeisogeza nchi mbele, na tumekuwa sehemu ya safari,” amesema Besiimire.

Mkurugenzi wa M-Pesa Tanzania, Epimack Mbeteni amesema kwa sasa matumizi ya huduma za kifedha kidijitali yanakuwa kuanzia kutoa na kuweka fedha hadi kuwekeza kidijitali.

“Hadi kufikia mwaka huu 2025, tayari huduma za kifedha kidijitali zimefikia asilimia 76. Hata hivyo, katika miaka 25 iliyopita ujumuishaji wa huduma za kifedha ilikua chini ya asilimia 9, wakati kwa sasa ni karibu asilimia 76,” amesema.

"Katika hili Vodacom inajivunia kuchangia kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwake huduma hizi mwaka 2008. Awali, ilikuwa ni kutoa na kuweka lakini hivi sasa kuna kuwekeza, kukopa na kufungua akaunti kidijitali," amesema mkurugenzi huyo.

Aidha, amesema Vodacom  itaendelea kuwafikia Watanzania zaidi huku katika mbio za Butiama mwaka huu itatumia fursa hiyo kupima na kutibu Watanzania bure.

Mbali na mafanikio hayo, Vodacom imesema kwa mwaka jana kampuni hiyo yenye wateja milioni 28, imetoa mikopo ya zaidi ya Sh2.5 trilioni kwa Watanzania.

Brigita Shirima, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom amesema wamezindua kampeni ya ‘Tupo nawe tena na tena’ kusherehekea miaka 25 ya kampuni hiyo kwa ajili ya kuwafikia zaidi wateja na watoa huduma.

"Tunaendelea kutoa uelewa wa Watanzania wa namna ya huduma zetu ili waelewe zaidi," amesema Shirima.

Akizungumzia ujumuishwaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania, Mchumi Oscar Mkude amesema huduma hizo zinatanua huduma hizo hasa katika kundi ambalo halijafikiwa na huduma za kibenki ikiwamo vijijini.

"Ni kweli, huduma za fedha za kidijitali zinakua sana hapa nchini,  zimetanua huduma za kifedha hasa kwa kundi ambalo halijafikiwa na huduma za kibenki huko hususani vijijini, watu wanaweza kuhifadhi pesa zao kiurahisi hata bila akaunti za benki, wanaweza kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi," amesema Mkude.

Dk Mwinuka Lutengano, mchumi kutoka UDOM amesema kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) hatua kubwa imepigwa hususani matumizi ya mifumo ya kidijitali kufanya miamala ya aina mbalimbali.

“Imani na uelewa imeongezeka eneo hili, wananchi wengi sasa wanamiliki simu za mkononi. Mzunguko wa kifedha unaendelea kuongezeka kidijitali, muda unapungua wa miamala na ufanisi unakua kwenye biashara na mwisho tija na faida vinapatikana,” amesema Dk Lutengano.

Amesema matumizi mazuri ya teknolojia ni fursa nzuri na kubwa ya kurahisisha mambo si tu kwa wanunuzi na wafanyabiashara ila pia kwa Serikali katika kutambua na kupata mapato ya tozo na kikodi.

Ameongeza kuwa, kwa sasa huduma za Tehama si kitu kigeni kuona watu wananunua bidhaa au kupata huduma kama za usafiri na usafirishaji kwa njia hizi. Huko siku zijazo itakuwa ngumu kwa shughuli za kiuchumi kuzitenga na maendeleo haya ya kidijitali.