Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kuanza kuunganisha magari ya umeme na gesi

Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya GF Automobile, Mehboob Karmali (kulia) kama ishara ya uzinduzi wa gari mpya ya Mahindra Scorpio uliofanyika jijini Dar es salaam

Muktasari:

  • Uunganishaji wa magari ya umeme na gesi ni moja ya hatua ya kukabiliana na hewa ukaa unayosababisha mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikihamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo katika vyombo vya moto ambayo ni moja ya hatua ya kukabiliana na hewa ukaa, Tanzania ipo mbioni kuanza kufanya uunganishaji wa magari ya umeme na gesi.

Uunganishaji wa magari haya sasa utafanya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kupata urahisi wa kununua magari tofauti na sasa wanapolazimika kuagiza kutoka bara lingine.

Hili linaanza kufanyika wakati ambao pia Tanzania imeanza kushuhudia kupungua kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi huku matumizi ya gesi asilia yakitajwa na wadau kuwa moja ya sababu.

Hayo yameelezwa usiku wa jana Jumamosi, Juni 21, 2025 na Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey wakati akizindua gari ya Mahdra Scopion uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Dey amesema Tanzania iko katika hatua za mwisho kutengeneza magari yanayotumia umeme na gesi nchini kupitia kiwanda cha kampuni ya GF kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

“Kutokana na mahusiano mazuri ya kibiashara yaliyopo baina yetu na Serikali ya Tanzania umesababisha India kuleta wawekezaji wengi hali inayoendeleza mahusiano mazuri yaliofanywa na waasisi wa mataifa hayo mawili,” amesema Dey.

Balozi huyo amesema kuanzia mwakani magari hayo yatakuwa yakitengenezwa nchini katika kiwanda cha GF Kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Magari yanayotumia gesi katika uendeshaji yametajwa kuwa moja ya sababu ya kushuka kwa fedha zilizotumika kuagiza mafuta nje ya nchi kati ya mwaka 2022 na 2024 zimepungua kutoka Sh9.57 trilioni hadi Sh7.62 trilioni mtawaliwa.

Ripoti ya Hali ya Uchumi ya Tanzania 2024, inaonyesha mafuta yalitumia Sh7.62 trilioni katika mwaka 2024 pekee ikiwa ni pungufu kutoka Sh9.574 trilioni mwaka 2022 na Sh8.04 trilioni mwaka 2023.

Hata hivyo, huenda fedha zilizotumika zilipungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kwani ripoti hii inaonyesha kati ya mwaka 2023 na 2024 bei za jumla za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zilipungua kwa wastani wa asilimia 9.5, 6.2 na 9.8.

Mbali na fedha zilizotumika kuagiza mafuta lia bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2025/2026 inaonyesha hadi Aprili, 2025 vituo tisa vya kujazia gesi asilia kwenye magari (CNG) vilikuwa vimekamilika na vinatoa huduma ikilinganishwa na vituo viwili vilivyokuwapo mwaka 2020/21.

Pia mtandao wa usambazaji wa gesi asilia nchini umeongezeka kutoka kilomita 102.54 mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 Aprili 2025 ambao umewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57.

Pia zaidi ya vyombo vya moto 15,000 vinatumia gesi asilia (CNG), hivyo kupunguza mahitaji ya petroli na dizeli katika uendeshaji wa vyombo vya moto nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya GF, Mehboob Karmali amesema baadaye watazindua gari za umeme na gesi zitakazotengenezwa nchini Tanzania kupitia kiwanda kilichopo Kibaha.

“Tutaanza na magari madogo ya mizigo (pickup- double cabin) maalumu kwa shughuli za kilimo na wajasiriamali wadogo hasa mashambani,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi za umma na Serikali kwa jumla kujenga tabia ya kununua bidhaa kutoka viwanda vya ndani ili kuvilinda, kuongeza pato la Taifa na kuokoa pesa ambayo ingetumika kuagiza bidhaa nje ya nchi.