Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibarua kinachomsubiri Dk Kimambo Muhimbili

Dar es Salaam. Gharama kubwa za huduma za matibabu, miundombinu na teknolojia ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa na wadau kuwa yanapaswa kushughulikiwa na mengine kuendelezwa na uongozi mpya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, MNH.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwamo Dk Delilah Kimambo kuwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), akichukua nafasi ya Profesa Mohammed Janabi ambaye alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Dk Kimambo ambaye ameteuliwa kushika nafasi hiyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Juni 16, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka awali, kabla ya uteuzi huo alikuwa akifanya kazi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Wadau mbalimbali wamempongeza Dk Kimambo kwa uteuzi huo, wakiangazia alivyoonyesha umahiri wake akiwa JKCI, huku wakitaja mambo kadha wa kadha yanayohitajika kushughulikiwa Muhimbili.

Mtaalamu wa masuala ya bima kutoka ACISP, Dk Anselmi Anselmi amesema Muhimbili ni hospitali kuu ya Taifa na imefanyiwa mabadiliko makubwa sana na Profesa Janabi na kufikia kushindana na hospitali kubwa za binafsi katika ubora wa huduma.

Ametaja changamoto kubwa ambayo atakutana nayo na wadau wa bima ni gharama za matibabu, dawa na vifaa tiba kwa ujumla, pamoja na kwamba Muhimbili wamejitahidi kuboresha kiwango cha huduma gharama za huduma zimepanda kwa kiasi kikubwa.

“Tulitegemea gharama zake zingekuwa nafuu. Kinachojitokeza gharama zinakimbizana na hospitali binafsi na wakati mwingine zinakuwa juu zaidi, inaleta ugumu na inapunguza Watanzania wengi kuzifikia huduma za afya,” amesema.

Amesema kama gharama zikiwa juu bima inabidi kuweka ukomo wa matibabu, hivyo inawaongezea kazi waendeshaji wa mifuko na kupunguza huduma kwa wanachama.

“Ana jukumu la kutazama upya gharama na kuangalia namna anaweza kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD) kuona namna gani anaweza kumsaidia Mtanzania wa kawaida.”

Dk Anselmi ametaja eneo la pili kuwa ni miundombinu, majengo na vitende kazi, akisema kumekuwa na jitihada ya kuleta vifaa vipya vya kisasa zaidi kutokana na ajenda ya tiba utalii, akitaja ni fursa kubwa kama nchi kuboresha matibabu yake ya ubobevu ili kukua zaidi eneo hilo.

Akisema hata matarajio ya fedha za kigeni zitakazoingia, zikafanye maboresho maeneo ya huduma za afya, ikiwemo kuongeza watoa tiba wabobevu suala alilotaja ni la kulitazama kimkakati.

“Kwenye bima tumekuwa tukipambana na tiba mtandao kama njia mojawapo ya utoaji wa huduma za matibabu, unafuu na uharaka wa huduma kwa wananchi, wataalamu wanatuambia inapunguza gharama za matibabu kwa wastani wa asilimia 35 mpaka 65,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphfta), Dk Egina Makwabe amesema wana imani na Dk Kimambo kutokana na uwezo wake, akitaja ukubwa wa viatu vya Profesa Janabi lakini anaamini ataweza kuvivaa vizuri.

“Sekta binafsi tunaamini kutakuwa na ushirikiano mzuri kama uliokuwepo mwanzo, suala la rufaa za wagonjwa wakitoka hospitali binafsi wasilazimike tena kupata barua kutoka hospitali za umma ni kitu muhimu lazima kiendelezwe.

“Profesa Janabi alishaanza kulifanyia kazi, lipo katika hatua nzuri kwa hiyo naamini ataliendeleza zaidi, pia alikuwa na maono makubwa ya kuitanua hospitali kuweka huduma nyingi nadhani ataendeleza vizuri tu,” amesema Dk Makwabe.

Aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshala amesema Dk Kimambo ana kazi kubwa ya kuifanya Muhimbili kuwa hospitali ya kisasa inayoweza kuhudumia wagonjwa wa aina zote.

“Bado tuna changamoto kupeleka wagonjwa nje, sehemu iliyobaki ana kazi ya kuhakikisha idadi inapungua zaidi, hali nyingine kuwafanya wafanyakazi kuwa na moyo wa kujitoa kama wauguzi wawe wanaowapa faraja wagonjwa,” amesema.

Katika hatua nyingine Wakili Nshala amegusia Bonde la Msimbazi, akisema kwa sehemu kubwa ina mazalia ya mbu na ni eneo ambalo linasogea na hospitali inaingia kwenye ule mto, hivyo lazima kujenga utaratibu mzuri kulimudu kutokana na hatari ya mazalia hayo.

Dk Delilah Kimambo ni nani?

Akimwelezea Dk Delilah Kimambo, Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo JKCI, Tatizo Waane amesema ni kiongozi muadilifu, makini, hodari, mcha Mungu kwani katika kipindi alichokaa katika taasisi hiyo amefanikisha kuleta mageuzi mbalimbali.

Amesema aliongoza Kitengo cha tiba shirikishi ambayo ni pamoja na dawa, maabara na mitambo ya utambuzi wa magonjwa ya moyo na magonjwa mbalimbali.

Dk Waane amesema katika kipindi chake, kitengo kimekuwa na maendeleo makubwa mojawapo ikiwa ni ongezeko la idadi ya wagonjwa wanaowahudumia, aina za uchunguzi na matibabu wanayofanya katika taasisi.

“Kwa kuwa alisomea masuala ya dawa na upatikanaji wake, pamoja na kwamba ni kazi ya taasisi, na kazi ya Mkurugenzi Mtendaji, amekuwa akisimamia na inakuwa ni zaidi ya asilimia 95 kiwango ambacho kinakubalika sehemu zote za hospitali nchini na kimataifa,” amesema.

Ameongeza kuwa anaamini ataitendea haki nafasi hiyo, hasa kwa kuwa amekuwa kiongozi tangu taasisi ya moyo ilipoanzishwa hivyo ana uzoefu wa kutosha sambamba na kupewa majukumu mengine katika taasisi amekuwa ni mwenyekiti mikutano ya kitaifa ya magonjwa ya moyo kwa miaka mitatu mfululizo.

Wasifu

Katika uzoefu wake wa kazi, akiwa Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na uangalizi wa wazee, ameshika nafasi mbalimbali akiwa JKCI, kama Mkurugenzi wa idara nyeti ya kliniki.

Akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Kliniki, JKCI amesimamia rasilimali watu na vifaa katika vitengo vya famasia, uhandisi wa vifaa tiba, huduma za uchunguzi wa picha, uchunguzi wa moyo bila upasuaji, maabara ya uchunguzi wa kisayansi na ya patholojia, na huduma za ustawi wa jamii.

Kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2022 akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni alisimamia mchakato wa zabuni wa taasisi kuhakikisha unakwenda vizuri. Kupitisha mapendekezo ya kitengo cha ununuzi na kuidhinisha mikataba.

Kipindi cha mwaka 2016 mpaka sasa Dk Kimambo ameendelea kuwa daktari bingwa akiwahudumia wagonjwa wa nje na wa ndani kwa wodi za kawaida, ICU na CCU.

Novemba 2011 mpaka Mei 2012 alifanya kazi katika kituo cha Christian Medical Centre - Vellore, Tamil Nadu, India kama daktari wa Idara ya moyo kama sehemu ya mafunzo ya ubingwa wa magonjwa ya moyo.

Machi hadi Septemba mwaka 2011 alikuwa katika mafunzo kwa vitendo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland huko Bergen, Norway kama daktari anayebobea katika magonjwa ya moyo akijifunza mambo mbalimbali ikiwemo kusaidia maabara za upasuaji wa moyo na upandikizaji wa betri za moyo ‘pacemaker’.

Mwaka 2016 mpaka sasa amekuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI na Mkurugenzi wa huduma za kliniki na Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni.

Pia Dk Kimambo amewahi kufanya kazi hospitali ya Taifa Muhimbili kuanzia mwaka 2013 katika idara ya magonjwa ya moyo kama daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kabla hajahamishiwa JKCI Aprili 2016.

Dk Kimambo amewahi kufanya kazi katika Hospitali ya Ligula – Mtwara kuanzia Desemba 2004 hadi Aprili 2012 kama Daktari wa Mkoa na Mratibu wa Mpango wa UKIMWI kwa niaba ya Clinton Foundation na alihamishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Pia amewahi kufanya kazi katika idara ya magonjwa ya ndani kama sehemu ya mafunzo Muhimbili kati ya mwaka 2010 hadi 2012.

Alifanya kazi kama daktari mtarajiwa katika Hospitali ya Bugando kwa kipindi cha mwaka mmoja 2003 – 2004.

Alipata shahada ya udaktari wa tiba katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam kati ya mwaka 2003 - 2007

Shahada ya uzamili katika tiba (MMed) aliipata katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam kwa mwaka 2007 hadi 2010.

Dk Kimambo pia alipata shahada ya uzamili ya sayansi katika tiba za moyo (MSc Cardiology) kati ya mwaka 2010 hadi 2013 kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam.

Mwaka 2021 hadi 2023 alitunukiwa shahada ya uzamili ya uangalizi wa wazee (MSc Care of Elderly) kutoka katika Chuo Kikuu cha Wales Trinity Saint David, kilichopo nchini Uingereza.