Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huyu ndiye Dk Delilah Kimambo, Mkurugenzi mpya wa Muhimbili

Muktasari:

  • Licha ya kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Dk Delilah Kimambo ni miongoni mwa madaktari bingwa wa uangalizi wa wazee ambao ni wachache barani Afrika.  shahada ya uzamili katika nafasi hiyo adimu alitunukiwa mwaka 2023 katika Chuo Kikuu cha Wales Trinity Saint David, kilichopo nchini Uingereza.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya  uteuzi wa viongozi mbalimbali ikiwemo Dk Delilah Kimambo kuwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Mwananchi imekusogezea wasifu wake.

Dk Kimambo anachukua nafasi Profesa Mohammed Janabi ambaye alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Mei 18 na kula kiapo Mei 28,2025.

Dk Delilah ambaye ameteuliwa kushika nafasi hiyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Juni 16, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka awali alikuwa akifanya kazi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Katika uzoefu wake wa kazi, akiwa Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na uangalizi wa wazee, ameshika nafasi mbalimbali akiwa JKCI, kama Mkurugenzi wa idara nyeti ya kliniki tangu mwaka 2016.

Akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Kliniki, JKCI amesimamia rasilimali watu na vifaa katika vitengo vya famasia, uhandisi wa vifaa tiba, huduma za uchunguzi wa picha, uchunguzi wa moyo bila upasuaji, maabara ya uchunguzi wa kisayansi na ya patholojia, na huduma za ustawi wa jamii.

Pia alikuwa na jukumu la kusimamia maduka yote ya dawa na vifaa tiba vya hospitali, kuandaa mipango ya mwaka ya ajira, mafunzo, vifaa na bajeti kwa kuzingatia mkakati wa taasisi.

Dk Kimanbo alihakikisha miongozo ya huduma za kliniki na ubora inatengenezwa, kuidhinishwa na kutekelezwa kwa ufanisi. Kuratibu utekelezaji wa sera na mipango kwa mujibu wa mipango iliyopitishwa.

Alisimamia bajeti na matumizi kwa idara zote zilizotajwa. Kufuatilia utendaji wa idara na kuchukua hatua za kuboresha huduma.

Pia alikuwa na jukumu la kusaidia kuandaa mpango mkakati wa biashara wa idara kwa kuzingatia mkakati wa taasisi. Kufuatilia na kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa mipango ya kimkakati, bajeti na malengo ya idara.

Pia aliratibu na kusimamia shughuli za kliniki za ndani (IPP) na kliniki ya kimataifa ya taasisi. Kuweka malengo ya utendaji kwa wafanyakazi wote na kuhakikisha kila mmoja ana mpango wa kazi.

Alisimamia na kufanya tathmini ya watumishi, pamoja na kutambua mahitaji yao ya maendeleo ya kazi na mafunzo. Kusaidia kuandaa nyaraka za zabuni kulingana na mahitaji ya idara.

Pia Dk Kimambo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 amekuwa Mwenyekiti wa mkutano mkuu wa wataalamu wa moyo barani Afrika, (Heart Team Africa Cardio Tan Conference).

Kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2022 akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni alisimamia mchakato wa zabuni wa taasisi kuhakikisha unakwenda vizuri. Kupitisha mapendekezo ya kitengo cha ununuzi na kuidhinisha mikataba.

Kukagua maombi ya marekebisho au nyongeza katika mikataba inayoendelea. Kuidhinisha nyaraka za zabuni na mikataba. Kuangalia utekelezaji wa sheria ya ununuzi wa umma (PPA 2011 na PR 2013) pamoja na kuwasiliana na mamlaka husika kwa masuala yaliyo katika mamlaka ya bodi.

Kipindi cha mwaka 2016 mpaka sasa Dk Kimambo ameendelea kuwa daktari bingwa akiwahudumia wagonjwa wa nje na wa ndani kwa wodi za kawaida, ICU na CCU.

Kuwapa ushauri wagonjwa wanaohitaji huduma za moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, kutoa mafunzo endelevu ya kitabibu, kusimamia na kutathmini picha za echocardiography.

Novemba 2011 mpaka Mei 2012 alifanya kazi katika kituo cha Christian Medical Centre - Vellore, Tamil Nadu, India kama daktari wa Idara ya moyo kama sehemu ya mafunzo ya ubingwa wa magonjwa ya moyo.

Alijikita zaidi katika kutumia vifaa mbalimbali kutambua magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kushiriki katika matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa CCU na kliniki za wagonjwa wa nje na kufanya maamuzi muhimu katika hali za dharura.

Machi hadi Septemba mwaka 2011 alikuwa katika mafunzo kwa vitendo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland huko Bergen, Norway kama daktari anayebobea katika magonjwa ya moyo akijifunza mambo mbalimbali ikiwemo kusaidia maabara za upasuaji wa moyo na upandikizaji wa betri za moyo ‘pacemaker’.

Mwaka 2016 mpaka sasa amekuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI na Mkurugenzi wa huduma za kliniki na Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni.

Pia Dk Kimambo amewahi kufanya kazi Hospitali ya Taifa Muhimbili kuanzia mwaka 2013 katika idara ya magonjwa ya moyo kama daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kabla hajahamishiwa JKCI Aprili 2016.

Dk Kimambo amewahi kufanya kazi katika Hospitali ya Ligula – Mtwara kuanzia Desemba 2004 hadi Aprili 2012 kama Daktari wa Mkoa na Mratibu wa Mpango wa Ukimwi kwa niaba ya Clinton Foundation na alihamishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Pia amewahi kufanya kazi katika idara ya magonjwa ya ndani kama sehemu ya mafunzo Muhimbili kati ya mwaka 2010 hadi 2012.

Dk Kimambo alifanya kazi kama daktari mtarajiwa katika Hospitali ya Bugando kwa kipindi cha mwaka mmoja 2003 – 2004.

Alipata shahada ya udaktari wa tiba katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam kati ya mwaka 2003 - 2007

Shahada ya uzamili katika tiba (MMed) aliipata katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam kwa mwaka 2007 hadi 2010.

Dk Kimambo pia alipata shahada ya uzamili ya sayansi katika tiba za moyo (MSc Cardiology) kati ya mwaka 2010 hadi 2013 kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam.

Mwaka 2021 hadi 2023 alitunukiwa shahada ya uzamili ya uangalizi wa wazee (MSc Care of Elderly) kutoka katika Chuo Kikuu cha Wales Trinity Saint David, kilichopo nchini Uingereza.