Janabi aingia rasmi WHO, aahidi mageuzi ya afya

Muktasari:
- Muhula wake utaanza Juni 30, 2025 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo na anaweza kuteuliwa tena kwa muhula mmoja zaidi.
Dar es Salaam. Profesa Mohamed Janabi, ameapishwa rasmi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, huku akiahidi kuboresha afya za watu wa Afrika.
Profesa Janabi amekula kiapo hicho leo, Mei 28, 2025 ikiwa ni siku 11 tangu alipochaguliwa Mei 18, 2025 wakati wa kikao maalumu cha ana kwa ana cha kamati ya kanda ya WHO ya Afrika na bodi hiyo ya utendaji kilichofanyika huko Geneva, Uswisi.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC), Dk Ntuli Kapologwe amesema uapisho huo umefanyika leo katika mkutano mkuu wa 78 wa WHO.
“Alikuwa ni mkurugenzi wa kanda mteule Mei 18 baada ya kuchaguliwa kwenye kikao cha bodi cha WHO na leo amethibitishwa rasmi na kupewa mikoba yote,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Kapologwe, WHO ilitoa taarifa awali kuwa Profesa Janabi angeanza kazi rasmi Juni mwaka huu baada ya kuapishwa.
Taarifa iliyotolewa leo na WHO imeeleza kuwa bodi kuu ya shirika hilo limemteua Profesa Janabi kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO kufuatia uteuzi wake uliofanywa wakati wa kikao maalum cha kamati ya kanda.
“Natoa pongezi zangu za dhati kwa Profesa Mohamed Yakub Janabi, pamoja na serikali na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuteuliwa kwako na Bodi Kuu kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus na kuongeza;
“Tunashukuru kwa uongozi wako na uzoefu wako tunapofanya kazi kwa pamoja kukabiliana na changamoto tunazokutana nazo, na kuiimarisha taasisi yetu ili iwe thabiti zaidi, endelevu na yenye ufanisi zaidi, tukitumia mgogoro wa sasa kama fursa.”
Profesa Janabi ametoa shukrani na kuahidi kuongeza juhudi za kuboresha afya ya watu wa Kanda ya Afrika.
“Ni kwa unyenyekevu mkubwa na kwa hisia ya dhima kubwa ninakubali heshima ya kuhudumu kama Mkurugenzi mpya wa Kanda ya Afrika. Nimeheshimiwa sana na ninashukuru kwa imani na uaminifu mlioweka kwangu,” amesema Profesa Janabi na kuongeza;

“Kuimarisha msingi wa kazi za WHO katika kanda ni kipaumbele kikuu kwangu. Kwa kulinganisha kila hatua tunayochukua na vipaumbele vya nchi, tunaweza kufanikisha matokeo yenye athari ya kudumu na yanayobadilisha maisha.”
Profesa Janabi ni daktari bingwa wa moyo, mtaalamu wa mikakati ya afya na mwanadiplomasia wa afya ya kimataifa, ambaye amejitolea maisha yake kuimarisha mifumo ya afya, kuendeleza huduma za haki, na kushirikiana katika uvumbuzi ili kuboresha matokeo ya kiafya barani Afrika.
Profesa Janabi ataongoza kazi za WHO katika kusaidia Nchi Wanachama 47 wa Kanda ya Afrika katika juhudi zao za kuboresha afya na ustawi wa watu.
Kwa kushirikiana na wadau, WHO barani Afrika inafanya kazi katika maeneo mbalimbali kutoka katika kuimarisha mifumo ya afya, kuzuia magonjwa hadi kukabiliana na dharura kwa ajili ya kukuza, kulinda na kutoa huduma za afya kwa wote.

Muhula wake utaanza Juni 30, 2025 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo na unaweza kuteuliwa tena kwa muhula mmoja zaidi. Anachukua nafasi ya Dk Matshidiso Moeti, ambaye aliongoza WHO Kanda ya Afrika tangu mwaka 2015.
Uchaguzi huo umeitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo Mtanzania Dk Faustine Ndugulile, aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo Agosti 27, 2024, aliyefariki dunia Novemba 27, 2025 wakati akipatiwa matibabu nchini India.