Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvutano wa Tanzania na Malawi umemalizwa hivi

Muktasari:

  • Aprili 23, 2025 ilitangaza kuzuia mazao kutoka nchi za Afrika Kusini na Malawi kuingia katika mipaka ya Tanzania hadi hapo hatua zitakapochukuliwa kwa nchi hizo kuruhusu mazao yetu kuingia katika masoko yao.

Dar es Salaam. Baada ya mvutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Malawi uliodumu kwa siku kadhaa, hatimaye nchi hizo zimemaliza tofauti zao kupitia mkutano wa mawaziri waliokutana Dodoma jana.

Baada ya kikao hicho cha Mei 2, 2025, kilichoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Malawi, Nancy Tembo, nchi hizo zilitoa tamko la pamoja kuashiria kumaliza hali hiyo iliyokuwa ikiathiri biashara baina yao.

Mawaziri wengine waliohudhuria mkutano huo ni wa Biashara, Habari, na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ambaye alikutana na mwenzake Sam Kawalenga, ambao walikuwa wakitunishiana misuli katika siku za hivi karibuni.

Aprili 23, 2025, Wizara ya Kilimo, ilitangaza kuzuia mazao kutoka nchi za Afrika Kusini na Malawi kuingia katika mipaka ya Tanzania hadi hapo hatua zitakapochukuliwa na nchi hizo kuruhusu mazao yetu kuingia katika masoko yao.

Kufuatia zuio hilo, Serikali za Malawi na Afrika Kusini ziliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo za Tanzania, ili kutafuta suluhisho la zuio husika. Siku mbili baadaye, Waziri Bashe aliondoa zuio hilo.

Kusainiwa kwa tamko la pamoja ni uthibitisho wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi kwa bidhaa mbalimbali, ikiwemo mazao ya kilimo, kulingana na mikataba na miongozo ya kikanda na kimataifa iliyopo.

Lengo la mkutano wa pamoja wa mawaziri lilikuwa kujadili amri ya udhibiti wa bidhaa (uingizaji na uuzaji nje ya nchi) (biashara) (marufuku), iliyotolewa Machi 13, 2025 na Serikali ya Jamhuri ya Malawi, ambayo ilipiga marufuku uingizaji wa baadhi ya bidhaa nchini humo.

“Majadiliano yalisisitiza dhamira ya pamoja ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kushughulikia masuala yaliyopo ya kibiashara,” limeeleza tamko hilo lililosainiwa na Balozi Kombo pamoja na Waziri Tembo.

Aidha, tamko hilo limeeleza kuwa pande zote mbili zilitambua uhusiano wa kihistoria na kindugu pamoja na urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Malawi. Wamewapongeza marais wa nchi zote mbili, Rais Samia Suluhu Hassan na mwenzake Lazarus Chakwera, kwa uongozi wao wa mfano na mwongozo katika masuala yote ya ushirikiano wa pande mbili na kikanda.

Ujumbe wa nchi zote mbili umepongeza mahusiano mazuri ya pande mbili yaliyopo kati ya nchi hizo, huku ukisisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili, kwa kutambua umuhimu wa kuzingatia mifumo ya kikanda na kimataifa katika utekelezaji wa ushirikiano wa kibiashara.

Zaidi ya hayo, ujumbe wa nchi hizo mbili umekubaliana kuandaa taratibu za pamoja za uendeshaji kuhusu viwango vya afya na usafi wa mimea na wanyama (Sanitary and Phytosanitary Standards) kwa mujibu wa miongozo ya kikanda na kimataifa.

Malawi ilithamini uamuzi wa Tanzania wa kuondoa notisi ya marufuku ya uingizaji wa mimea na bidhaa za mimea kutoka Malawi iliyotolewa  Aprili 23, 2025. Hivyo, ikaahidi kutoa waraka wa kiutawala kwa mamlaka husika ili kuwezesha uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Malawi kuanzia tarehe ya taarifa hiyo.

Kwa kuzingatia maamuzi ya kikao cha sita cha Tume ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi kilichofanyika kuanzia Februari 24 hadi 27, 2025 mjini Lilongwe, Malawi, pande zote mbili zilihakikisha tena dhamira yao ya kukamilisha mahitaji ya kisheria kwa ajili ya kusaini Mkataba wa Utaratibu Rahisi wa Biashara (Simplified Trade Regime Agreement) na kutekeleza mkataba huo baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani za kisheria ifikapo Mei 30, 2025.

Pande zote mbili zilitamka dhamira ya kutekeleza maazimio ya mkutano huo kwa manufaa ya wananchi wa Malawi na Tanzania.

Baada ya mkutano kumalizika, Waziri Bashe alichapisha taarifa iliyoambatana na picha katika ukarasa wake wa mtandao wa X, akielezea kuwa mkutano huo umezaa matunda muhimu katika uchumi na kwa wakulima wa nchi hizo mbili.

“Saini ya tamko hili ni hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara, hasa katika sekta ya kilimo, kwa kuzingatia mikataba ya kikanda na kimataifa. Ushirikiano huu ni ushahidi wa diplomasia ya kiuchumi inayolenga maendeleo ya wakulima wetu,” alisema Bashe.


Kauli ya Jafo

Leo, Mei 3, 2025 Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, akizungumza katika Jukwaa la Kiuchumi Mkoa wa Arusha, amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa, hasa kwa upande wa biashara kwa kutanua masoko.

Serikali ya Tanzania imekutana na nchi ya Malawi kumaliza changamoto iliyokuwa imejitokeza na kusababisha zuio la uingizaji wa bidhaa za kilimo baina ya nchi hizo mbili.

Kutokana na sababu hiyo, Serikali imewataka wafanyabiashara nchini waliokuwa wakifanya biashara nchini humo waendelee kufanya biashara zao kwa uhuru ili kuongeza uchumi wa Taifa.

“Nataka niwaambie ndugu zangu, jana tulikuwa na kikao Tanzania na wenzetu wa Malawi kuondoa mambo yote yaliyokuwa yanaonekana ni changamoto. Kama hapa Arusha kuna wafanyabiashara wanaofanya biashara na Malawi... nendeni mkafanye biashara kwa upana unaotakiwa, tutengeneze fedha, nchi isonge mbele,” amesema Dk Jafo.