Walimu waliohamishwa kutoka sekondari kwenda msingi kulipwa

Muktasari:
- Mpango wa kuwahamisha walimu kutoka sekondari kwenda msingi ulianzishwa katika uongozi wa awamu ya tano chini ya hayati John Magufuli.
Dodoma. Walimu waliohamishwa kutoka shule za sekondari na kupelekwa shule za msingi wanaidai Serikali Sh865.93 milioni na imeahidiwa italipa.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainabu Katimba amesema jumla ya fedha iliyohitajika kwa ajili ya uhamisho wa walimu kwenye mpango huo ilikuwa ni Sh2.08 bilionio ambapo Sh1.22 zimelipwa.
Katimba ametoa majibu hayo bungeni leo Jumatatu Mei 5,2025 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe.
Katika swali lake mbunge huyo amehoji ni lini Serikali italipa madeni ya walimu wa shule za sekondari waliohamishiwa shule za msingi.
Naibu Waziri amesema Serikali katika kuboresha ikama ya walimu wa shule za msingi nchini imekuwa ikihamisha walimu kwa kuzingatia ikama ya halmashauri husika.
“Kwa kipindi cha mwaka 2017 hadi 2025, walimu 1,914 wamehamishwa kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi, Serikali itaendelea kulipa madeni ya uhamisho wa walimu kadiri ya upatikaji wa fedha,” amesema Katimba.
Februari 2018, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilitangaza baadhi ya walimu wa masomo ya sanaa kutoka shule za sekondari wakapelekwa shule za msingi ili kukidhi mahitaji.
Akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, kilichopo mkoani Iringa, Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alisema hakuna madhara kwa walimu kuhamishwa kutoka sekondari kwenda kufundisha msingi, isipokuwa wanatakiwa kuangalia viwango vyao vya mishahara.
Hayati Magufuli alisema baadhi ya nchi za Scandinavia kuna maprofesa ambao wanafundisha hadi shule za chekechea na wanalipwa mishahara mikubwa kuliko wanaofundisha vyuo vikuu.