Aliyemtisha Padri Kitima siku chache kabla ya kushambuliwa akamatwa

Muktasari:
- Watu wawili wanashikiliwa kwa mahojiano juu ya tukio la kushambuliwa na kitu butu kichwani kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima ambaye kwa sasa amelazwa Hospitali ya Aga Khan akipatiwa matibabu
Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetangaza kumshikilia na kumuhoji, Dk Frey Edward Cosseny aliyemtisha kupitia mitandao ya kijamii, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.
Dk Cosseny aliandika ujumbe wa kumtisha Padri Kitima na siku mbili baadaye akashambuliwa. Ujumbe huo aliutoa Aprili 28, 2025 usiku ukisomeka:
“Mwambieni Kitima iko siku ataingia kwenye 18 hatokaa asahau Tanzania muacheni ajifanye mwanasiasa. Mfikishieni message siku si nyingi atapata anachokitafuta dawa yake iko jikoni atakuja kuozea jela.”
Kukamatwa kwake kumeripotiwa na Jeshi hilo, ikiwa siku chache zimepita baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa kuliagiza jeshi hilo kumtafuta na kumuhoji mtuhumiwa huyo aliyeandika kwenye mitandao ya kijamii siku za Kitima zinahesabika.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta kwa haraka, yule mtu aliye-tweet kwenye mitandao ya kijamii kwamba, ‘siku za Kitima zinahesabika’. Mtu huyu atafutwe haraka, ahojiwe ametumwa na nani, na hatua kali za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo, kwa watu wote watakaobainika kuhusika katika tukio hili,” aliagiza Bashungwa, Mei 2, 2025.
Mtuhumiwa huyo anakuwa wa pili kutiwa mbaroni ikiwa siku tano zimepita tangu Padri Kitima kushambuliwa Aprili 30, 2025 kwenye makazi yake Kurasini jijini Dar es Salaam yalipo makao makuu ya baraza hilo na hadi sasa amelazwa Hospitali ya Aga Khan akiendelea kupatiwa matibabu.
Tangu kutokea kwa tukio hilo linalovuta hisia tofauti kuanzia kwenye mitandao yakijamii, kumekuwa na matamko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa dini, kiserikali na wanadiplomasia wakilaani tukio hilo wakitaka wahusika kushughulikiwa.
Leo Jumatatu, Mei 5, 2025 akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa na wameanza kumuhoji.
"Natoa taarifa rasmi, tumemkamata na tunamuhoji, Frey Edward Cosseny (51) mkazi wa Dodoma na Mbezi Beach Makonde Dar es Salaam, kufuatia chapisho lake la vitisho dhidi ya Padri Charles Kitima ambalo kwa mujibu wa ufuatiliaji alilitoa na kulichapisha mitandaoni siku chache kabla ya kutokea kwa tukio lilomuhusisha pande Kitima," amesema Kamanda Muliro.
Amesema upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa pamoja na ufuatiliaji kwa kushirikiana na mamlaka zingine za dola.
"Taarifa hii ni mwendelezo wa ufuatiliaji unaofanywa na Jeshi la Polisi katika tukio hili la Padri Kitima kuhusiana na kila jambo ambalo limejitokeza, na huyu ni mtu wa pili ambaye tunaendelea kumuhoji kwa chapisho lake lililokuwa linaashiria vitisho kabla ya tukio lenyewe kutokea," amesema Muliro.
Jana Jumapili, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) lilisema shambulio dhidi ya Padri Kitima, licha ya kumuumiza yeye, pia baraza hilo limeshambuliwa na heshima ya Taifa imejeruhiwa.
Kauli hiyo ilitolewa katika salamu za TEC zilizotolewa na Makamu wa Rais wa Baraza hilo, Askofu Eusebius Nzigilwa katika misa ya kumsimika Askofu wa Jimbo Jipya Katoliki la Bagamoyo, Askofu Stephano Musomba.
Hilo lilikuwa tamko la pili la TEC, baada ya tukio la kushambuliwa kwa Padri Kitima huku ukitolewa wito wa uchunguzi wa haraka.
“Tunatafakari na kujiuliza ni nini hasa kinachoshambuliwa kwa tukio kama lile. Je, anashambuliwa mtu, taasisi au Taifa,” amehoji na kufafanua kuwa maeneo matatu yameshambuliwa na kujeruhiwa.
“Shambulio lile halikuwa la watu waliotaka kumpora mali au fedha, bali lilikuwa ni shambulio la watu waliotaka kumpora uhai wake, uhuru na haki yake ya kuishi, kusema na kutenda kadiri ya dhamiri, imani na wito wake aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Askofu Nzingilwa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda.
Watano wadakwa Kigamboni
Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amesema wanawashikilia watu watano wanaotuhumiwa kwa makosa ya usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya bangi gunia 60, maeneo ya Kibada Kigamboni katika Mkoa wa Kipolisi Temeke.
Watuhimiwa hao walikamatwa na dawa hizo zikiwa zimehifadhiwa kwenye magunia kupakiwa ndani ya tenki la lori lenye mwonekano wa kubeba mafuta.
"Baada ya kulipekua tulikuta likiwa limepakia gunia hizo za bangi, watuhumiwa waliokamatwa ni Nassan Danga 'Masumbuko' na wenzake wanne akiwemo mwanamke aliyefahamika kwa jina la Upendo Mgonja wote watafikishwa mahakamani kupitia mamlaka nyingine za kisheria," amesema Muliro
Muliro amesema Jeshi hilo limemkamata mtu anayefahamika kwa jina la David Zephania Sanga (38), ambaye zamani alikuwa mfanyakazi wa taasisi ya bima kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kituo cha Polisi Kigamboni.
"Wezi wamemuibia vifaa vya magari mawili yaliyokuwa yamehifadhiwa ndani kwake, baada ya Jeshi la Polisi kufanya ufuatiliaji ilibanika vifaa alivyotaja ikiwemo bamba za mbele na nyuma, saiti mira na betri alivyodai vimeibiwa na wezi baada ya kuruka ukuta alikuwa amevificha na kuja kutoa taarifa za uongo akiwa na lengo la kudanganya kampuni ya bima ili ajipatie fedha," amesema.