Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mifugo kutumika kupata mikopo

Muktasari:

  • Serikali imesema mpango wa utambuzi na chanjo ya mifugo, unalenga kudhibiti wizi na kuongeza thamani ya mifugo nchini.

Simiyu. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wa Serikali kuanzisha mpango wa utambuzi na mifugo, pamoja na mambo mengine, unalenga kuwawezesha wafugaji kuitumia mifugo yao kama dhamana ya kupata mikopo katika taasisi za fedha.

Sambamba na hilo, amesema mpango huo unaohusisha pia chanjo kwa ajili ya mifugo yote, unalenga kudhibiti wizi na kuongeza thamani ya mifugo nchini.

Kauli hiyo ya Rais Samia inakuja katika kipindi ambacho, Tanzania inatajwa kuwa nchi ya kwanza kwa wingi wa mifugo, lakini sekta hiyo inachangia asilimia sita pekee katika uchumi.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizindua mpango wa chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa kwa mwaka 2024/2025- 2028-2029 katika viwanja vya Nanenane Bariadi Mkoani Simiyu leo Juni 16, 2025.

Kuanzishwa kwa mpango huo wa chanjo na utambuzi wa mifugo, amesema utawezesha kuongeza mchango wa sekta hiyo kwa uchumi wa Taifa.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumatatu Juni 16, 2025 alipowahutubia wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, katika mkutano wa hadhara, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.

Dhamira ya Serikali kuanzisha mpango wa utambuzi wa mifugo na chanjo, amesema ni kusaidia kudhibiti wizi na kuongeza thamani ya mifugo ikiwemo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.

“Kwa hali ya sasa ya mifugo kutotambulika kunasababisha utajiri walionao wafugaji kutotambulika na hivyo kuwakosesha manufaa yanayopatikana kutokana na mifugo yao kutotambulika,” amesema.

Baada ya kuitambua, amesema itakuwa rahisi mfugaji kuitumia mifugo yake kuweka dhamana katika taasisi za fedha na kupewa mkopo.

Katika mpango huo wa chanjo, amesema Serikali itagharimia uwekaji wa hereni kwenye mifugo yote na chanjo za kuku, hivyo wafugaji watazipata bure.

“Lengo ni kuweka kanzidata ya Taifa ya mifugo, kwa sasa tunakisia lakini tukijua idadi kamili tutafanikiwa,” amesema Rais Samia.

Ameambatanisha ujumbe wake huo na kile alichoeleza, licha ya wingi wa rasilimali za mifugo zilizopo nchini, mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa ni asilimia sita pekee.

Zitakapofanyika jitihada za uwekezaji, amesema katika sekta husika, itakuza mchango huo.

Amesema mchango mdogo wa sekta hiyo unatokana na kutotambulika na kutochanjwa kwa mifugo, kwa kuwa wafugaji wengi wanafuga kwa ufahari wa kuwa na ng’ombe wengi.

“Tulipoanza jitihada ndogo za kushughulikia sekta hii, mauzo ya mazao ya mifugo yameanza kuifaidisha nchi,” amesema.

Ili kufikia lengo linalokusudiwa, amesema Serikali imelenga kutoa chanzo na utambuzi wa mifugo na katika utekelezaji wa hilo Sh216 bilioni zimeandaliwa.

Katika mpango huo wa miaka mitano, amesema wanalenga magonjwa ya mifugo yenye athari kimkakati ikiwemo homa ya mapafu ya ng’ombe, sotoka ya mbuzi na kondoo na mdondo kwa kuku.

Gharama za uchanjaji wa mifugo, amesema zitachangiwa nusu kwa Serikali na nyingine kwa wafugaji wenyewe ili kuwapunguzia mzigo wa bei.

“Maana yake tumeanza kutoa ruzuku kwa wafugaji, tukianza kwenye chanjo,” amesema.

Kwa mujibu wa Rais Samia, juhudi ndogo zilizofanywa katika kuiboresha sekta ya mifugo, mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 692 mwaka 2021 hadi 14,701 zenye thamani ya Dola za Marekani 61.4 milioni.

Amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na binafsi katika kuzalisha viuatilifu, chanjo na dawa za mifugo.

“Kampuni zote za ndani na wanazalisha chanjo zote na nimesikia mipango yao wanayokwenda kufanya ili Tanzania ijitosheleze kwa uzalishaji wa chanjo haya ni mambo makubwa sana,” amesema.

Uzalishaji wa chanjo nchini, amesema unatoa uhakika wa usalama wake kwa kuwa wakati zinaagizwa nje ya nchi hakukuwa na uhakika wa usalama.

Amesema utambuzi wa mifugo umeanza mkoani Simiyu kwa sababu ni namba tatu kwa wingi wa mifugo nchini, hivyo anatarajia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kwingineko.

“Natambua changamoto zinazowakabili wafugaji nchini hususan suala la malisho na maji, nikuhakikishie Serikali inakwenda kufanyia kazi,” amesema.

Mkuu huyo wa nchi, amesema maeneo ya malisho yatakapotengwa yanapaswa kuendelezwa ili kuhakikisha kunakuwa na malisho ya mwaka mzima.

Amewataka wafugaji kuanza kufanya uendelezaji wa maeneo yanayotengwa kwa ajili ya malisho ili yawafae wakati wa kiangazi.

“Tujiepushe kutenga fedha kwa ajili ya kulipa faini za kulipa faini ya kulisha mifugo katika hifadhi za misitu au wanyamapori na badala yake tutumie fedha hizo kuendeleza maeneo ya malisho,” amesema.

Ameitaka wizara husika kuongeza uzalishaji wa mbegu za malisho na kutoa elimu ya upandaji wake kwa kuwa dhana hiyo ni mpya nchini.

Rais Samia amesema mifugo kwa kiasi kikubwa ni ya asili na inachukua muda mrefu kukua na kufikia uzito unaostahili kupelekwa soko na kwamba wizara inajipanga kuboresha mbali za mifugo.

“Sasa ninyi wafugaji muitikie programu hii ili badala ya kumtunza ng’ombe kwa miaka zaidi ya miwili hajafika kilo 290 sasa umfuge kwa miezi tisa akupe kilo zaidi ya 200 na hiyo inawezekana tukifuata uwekezaji,” amesema.

Amesema kampeni ya chanjo ya mifugo inaenda sambamba na ugawaji wa vifaa vya chanjo ikiwemo majokofu, pikipiki na vishikwambi vya kutolewa chanjo katika halmashauri zote nchini.


“Nielekeze Tamisemi kusimamia na kuhakikisha vifaa hivi vinafungwa na kuhakikisha kampeni hii inatekelezwa ipasavyo na kuwa na mafanikio yanayotarajiwa,” amesema.

Amesema wataalamu 3,800 wanashirikishwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo na mpango uliopo ni kutoa ajira za muda mfupi kwa wataalamu 7,000 kwa ajili ya wataalamu walioko nje ya soko la ajira.

Jukumu wanalokabidhiwa, amesema linalenga kuhakikisha mifugo inahudumiwa vema na isitokee wazalishaji wa chanjo walalamikiwe kwa sababu ya uchanjaji usiostahili.


Alichokisema Waziri

Akizungumza utambuzi wa mifugo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema hilo ni tukio la kihistoria kwani ndiyo mara ya kwanza linafanyika tangu uhuru wa nchi na zaidi ya nusu ya gharama za jambo hilo, zinatolewa na Rais Samia.

Amesema Serikali imeridhia kuendelea kuitambua na kuichanja mifugo, kadhalika itasimamia kuhakikisha utekelezaji wake ili kuwafanya wafugaji wanufaike na shughuli zao.

Sambamba na hilo, ameeleza chanjo zote zitatoka kwa wazalishaji wa ndani.

Katika hotuba yake, Dk Ashatu amesema Agosti 8, mwaka 2024, Rais Samia aliwakabidhi vijana wa mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), kiasi cha Sh1.1 bilioni kwa ajili ya uwekezaji katika unenepeshaji wa mifugo.

Amesema tayari vijana 106 wamepatiwa ekari 1,700 katika ranchi ya Kagoma wilayani Karagwe na wameshanunua ng’ombe mara mbili na kuwauza na kazi wanayofanya sasa ni kuwaita vijana wengine waendelee.

Wafugaji

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mrida Mshota ameiomba Serikali ipime na kurasimisha maeneo ya wafugaji ili kuondoa migogoro kati yao na mamlaka hasa za maliasili.

“Tunaomba maeneo ya wafugaji yapimwe na kurasimishwa kwa wafugaji kwa sababu tumebaki nyuma kwa muda mrefu..tuna mifugo mingi sana zaidi ya milioni 39 lakini ukienda kwenye  vijiji tulichelewa sana kwenye mpango wa matumizi ya ardhi,” amesema Mshota.

Amesema yakipimwa yataondoa changamoto nyingi nchini, pia ameomba wafugaji wachimbiwe vizimba kwa ajili ya kunyeshewa mifugo yao akidai, ikifanyika hivyo, migogoro ya wafugaji kuingilia maeneo ya wakulima itakwisha.

Hata hivyo, Rais Samia alisema Serikali itafanyia kazi maombi yote ya kiongozi huyo wa wafugaji.