Rais Samia azindua ofisi ya RC Simiyu, aahidi neema kwa wakulima

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu akivuta kitambaa kuashiria ufunguzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu lililopo Bariadi leo Juni 16, 2025.
Muktasari:
- Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, ambayo awali ilikuwa eneo la Somanda, imehamishwa katika jengo jipya la utawala lililopo katika Mji wa Kiserikali wa Nyaumata.
Simiyu. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua na kulifungua rasmi jengo la ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh6.5 bilioni, huku akiahidi neema kwa wakulima wa zao la pamba.
Uzinduzi wa jengo hilo umefanyika leo Juni 16, 2025, wakati wa ziara ya mkuu huyo wa nchi, inayoendelea mkoani Simiyu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, ambayo awali ilikuwa eneo la Somanda, imehamishwa katika jengo jipya la utawala lililopo katika Mji wa Kiserikali wa Nyaumata.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Rais Samia, Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Simiyu, Erick Mapande amesema pamoja na ofisi za idara mbalimbali, jengo hilo la kisasa pia lina kumbi za mikutano ukiwemo ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuchukua watu 500 kwa wakati mmoja.

“Mradi huu umetekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ilianza Mei, 2019, awamu ya pili ilianza Februari, 2022 na awamu ya tatu na ya mwisho umeanza Juni 2022; hadi sasa mradi umekamilika, bado vitu vichache kama uzio ambao utatekelezwa kwenye awamu inayofuata,” amesema Mapande.
Ametaja faida kadhaa zinazotokana na utekelezaji wa mradi huo ikiwemo mazingira bora ya kazi na huduma kwa watumishi na wananchi wanaofika katika ofisi hizo.
“Fursa za ajira ya kudumu na za muda, mafunzo kwa wanafunzi wa fani ya ujenzi kutoka vyuo mbalimbali nchini, fursa ya biashara kwa wauzaji wa vifaa vya ujenzi na wajasiriamali na makusanyo ya kodi na ushuru kwa watoa huduma ni miongoni mwa faida za kiuchumi zilizotokana na utekelezaji wa mradi huu,” amesema Mapande.
Akimkaribisha Rais Samia kuzindua mradi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema mradi huo ni kati ya miradi kadhaa ya maboresho ya miundombinu ya ofisi katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
“Tulipoingia madarakani, ulitoa maelekezo ya kuboresha miundombinu katika mikoa yote 26 nchini (Bara), ikiwa ni jukumu la utekelezaji wa suala zima la utawala bora; na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya majengo yote 26 ya mikoa ni takriban Sh91.17 bilioni,” amesema Mchengerwa.
Kilimo cha pamba
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali imejipanga kuimarisha na kupandisha hadhi ya zao la pamba kama ilivyofanya katika mazao ya korosho na kahawa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua na kufungua viwanda viwili vya kuongeza thamani ya mazao, kikiwemo kiwanda cha kuchambua pamba na kingine cha kutengeneza mabomba ya maji, mkuu huyo wa nchi ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika jitihada za kuboresha na kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
“Nimefurahishwa kuona wazawa wanawekeza kwa nguvu kubwa. Hili ni jambo la kujivunia kwa sababu linatoa siyo tu ajira, bali pia kukuza uchumi wa mikoa yetu,” amesema Rais Samia.
Amesema pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati kama ilivyo korosho na kahawa, hivyo Serikali inaandaa mikakati itakayopandisha hadhi ya zao hilo katika soko la ndani na nje ya nchi.
“Kazi yetu Serikali ni kuweka mazingira, kutunga na kutekeleza sera zitakazosaidia kupandisha hadhi na thamani ya mazao yetu kwa kuziongezea thamani badala ya kuuza mazao ghafi. Tumeanza na korosho na kahawa. Hata mbaazi ambayo zamani tulitumia kama mboga, sasa ipo kwenye soko la dunia. Sasa tunakwenda kwenye pamba,” amesema Rais Samia.
Amesema mageuzi katika sekta ya kilimo siyo tu yataongeza kipato na uchumi wa wakulima, bali pia yatawezesha Taifa kuingiza fedha nyingi za kigeni kwa kuuza bidhaa iliyoongezwa thamani.
Amewaomba wakulima nchini kuunga mkono juhudi za Serikali katika mabadiliko yanayofanyika katika sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa hatua zote zinalenga kuwanufaisha.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema uwekezaji katika sekta ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, ikiwemo pamba, utaongeza fursa za ajira kwa vijana na hivyo kupanua mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Azindua kiwanda cha mabomba, pamba
Katika hatua nyingine, Rais Samia amezindua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji na uchakataji wa zao la pamba cha MOLI Oil Mills kilichopo Bariadi mkoani Simiyu.
Rais Samia amezindua kiwanda hicho kinachomilikiwa na Gungu Silanga leo Jumatatu, Juni 16, 2025 ambapo amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa Simiyu.

Pia, amesema pamba inayozalishwa ndani ya nchi kutumika hapa nchini katika kuzalisha bidhaa zingine badala ya kuisafirisha nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo awali.
“Tunafahamu hapa Simiyu wanategemea zao la pamba katika kukuza uchumi, na hapa nimshukuru sana Silanga kwa kufanya uwekezaji huu mkubwa ambao, unakwenda kuongeza thamani ya pamba.
Kwa upande wake Silanga ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amemshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira bora na salama kwa uwekezaji na kwamba, hatua hiyo imeongeza ari kwa wawekezaji wazawa.

Amesema mazingira yaliyowekwa na Serikali yameendelea kufungua milango ya uwekezaji na kwamba, hatua hiyo inakwenda kuibadilisha Tanzania kwa kuvutia wawekezaji wengi zaidi.