Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia awasili kanda ya ziwa kwa ziara ya Simiyu, Mwanza

Muktasari:

  • Rais Samia atafanya ziara ya siku saba mkoani Mwanza na Simiyu kuanzia Juni 15 hadi 21, 2025 na atazindua miradi mbalimbali ukiwamo wa Daraja la JPM maarufu kama Kigongo - Busisi lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni.

Mwanza. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Mwanza, tayari kwa ziara ya siku saba katika mikoa ya Mwanza na Simiyu.

Ndege aliyopanda mkuu huyo wa nchi, imetua Uwanja wa Ndege wa Mwanza leo Juni 15, 2025 saa 9:30 alasiri na amepokewa na kusalimaina na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi.

Rais Samia ameendelea na safari kwenda mkoani Simiyu huku njiani akipata fursa ya kusalimiana na wananchi waliojitokeza kumlaki.

Akiwa Simiyu, Rais Samia anatarajiwa kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Sh522 bilioni.

Miongoni mwa mradi mkubwa atakaouwekea jiwe la msingi akiwa mkoani Simiyu, ni mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unakadiriwa kugharimu Sh440 bilioni.

Rais Samia atamalizia ziara yake mkoani Simiyu Juni 19, 2025 kisha atarejea mkoani Mwanza atajapozindua Daraja la JPM maarufu kama Kigongo – Busisi, lililojengwa kwa gharama ya Sh700 bilioni, kisha ataendelea na ziara yake Mwanza hadi Juni 21, 2025.

Daraja hilo ni refu kuliko yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati na la sita barani Afrika, lina urefu wa kilometa 3.2 na linakatisha katika Ziwa Victoria, likiunganisha eneo la Kigongo wilayani Misungwi na eneo la Busisi, Wilaya ya Sengerema.

Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo lenye njia nne pamoja na njia za watembea kwa miguu kila upande, kutarahisisha shughuli za usafirishaji kati ya mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza, Kigoma na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na DRC kwa kumaliza kero ya kutumia muda mrefu  kuvuka eneo la Kigongo – Busisi kwa kutumia vivuko.

Uwepo wa daraja hilo, pia, utaokoa maisha ya wagonjwa kutoka mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera wanaokimbizwa kwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ambao baadhi maisha yao yalikuwa hatarini kutokana na kusubiri muda mrefu kuvuka eneo hilo kwa kutumia vivuko.

Kwa sasa, muda wa wastani wa kuvuka eneo la Kigongo – Busisi kwa kutumia kivuko ni kati ya dakika 45 hadi saa nzima kutegemeana na wingi wa magari na idadi ya vivuko vinavyotoa huduma.

Mara nyingi, huduma ya kuvusha magari na abiria kwa vivuko eneo hilo, inatolewa na vivuko vya Mv Mwanza na Mv Misungwi vinavyotumia wastani wa dakika 30 hadi 45 kuvuka kutoka ama Kigongo kwenda Busisi au kinyume chake.


Wananchi wazungumza

Wakizungumza wakiwa uwanja wa ndege, wakazi wa Mkoa wa Mwanza wamesema sasa wanaamini kuwa Daraja la JPM linazinduliwa Juni 19, 2025 baada ya kushuhudia Rais Samia akiwasili na kuwasalimia kwa kuwapungia mikono.

“Nimekuja kushuhudia ni kweli Rais Samia atafika? Nimemuona, sasa najiandaa kwenda kushuhudia uzinduzi wa daraja la Busisi,” amesema Flora John, mkazi wa Pasiansi mkoani Mwanza.

Zainabu Maulid, mkazi wa Furahisha jijini Mwanza, amesema ujio wa Rais Samia umemuaminisha kuwa sasa atatumia daraja hilo kwenda na kurudi Geita anapofanya biashara ya dagaa wa kukaanga.

“Mimi biashara yangu kubwa ni dagaa wa kukaanga, ujio wa Rais umeniaminisha kweli anaenda kuzindua Daraja la Busisi na sasa masuala ya kuhangaika na vivuko yanaenda kuwa historia, nitakwenda Geita na kurudi Mwanza,” amesema Maulid.

Naye, Moses Michael ameshukuru Rais Samia kurudi tena Kanda ya Ziwa, akieleza kanda hiyo imekuwa na bahati ya kutembelewa na viongozi wa kitaifa ambao mara kadhaa wanachochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Mwanza tuna bahati ya kutembelewa na Rais Samia, Rais wa Tanzania…hii ni kama mara ya tatu akija Mwanza tangu aapishwe kuwa Rais. Ni bahati sana kwetu wanaMwanza,” amesema Michael.