Rais Samia kufanya ziara mikoani, Msumbiji na Comoro

Muktasari:
- Rais wa Tanzania, anatarajia kufanya ziara katika mikoa na nchi mbili kwa nyakati tofauti.
Dodoma. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara mikoa ya Simiyu na Mwanza pamoja na nchi za Msumbiji na Comoro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 11, 2025, Msigwa amesema akiwa mikoa hiyo, Rais Samia atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Amesema Juni 15 hadi 18, 2025 atakuwa kwenye Mkoa wa Simiyu kwa kutembelea wilaya zote za mkoa huo takribani nne na kisha Mwanza ambapo itadumu hadi Juni 21, 2025.
Msigwa amesema akiwa Mwanza, Rais Samia atazindua daraja kubwa la Kigongo Busisi ambalo ni miongoni mwa madaraja makubwa yaliyopata kutokea barani Afrika.
Msigwa amesema akiwa Mwanza Juni 21, 2025 Rais Samia atashiriki katika tamasha la kitamaduni na kuwataka wananchi kuhudhuria kwa wingi katika ziara zake.
Pia amesema Rais Samia amealikwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru ya nchi za nchi za Msumbiji na Visiwa vya Comoro.
Aidha, Msigwa amesema wakati Tanzania inaelekea katika uchaguzi mkuu Oktoba 2025, mihemko ya uhamasishaji usiofaa imekuwa mingi kwenye mtandao ya kijamii hivyo kuwaonya vijana kutojihusisha nayo.
Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya kuwapo watu katika mitandao ambao wamekuwa wakiandika chini ya jumbe za watu No reform, no election.
Msigwa amesema sehemu kubwa ya wanaojihusisha na vitendo hivyo ni vijana walio vyuoni lakini kupitia vipindi vya televisheni na mitandao ya jamii elimu imekuwa ikitolewa kuhusu matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Tamaduni na Michezo, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la wizara hiyo katika mji wa kiserikali Mtumba jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
“Nawaombeni Watanzania tuzingatie, elimu ya matumizi ya mitandao ya kijamii. Lakini Serikali imejenga uwezo wa udhibiti wa matendo yasiyofaa katika mitandao ya kijamii. Na ndio hapa ninapokuja kuzungumzia Sheria ya Makosa ya Mtandao,” amesema.
Amesema wengi wanaofanya hivyo ni wanafunzi na kuwahakikisha watawapata watu wote wanajihusisha na vitendo hivyo kama sio leo basi ni siku zijazo kwa kuwa jinai huwa haifi.
“Naomba kutumia mkutano huu kuwaomba watu na vijana wote na walioko mitaani tutumie mitandao ya kijamii kwa manufaa. Tutumie mitandao ya kijamii kujifunza, kujielimisha, kufanya biashara na kuunganishwa wenyewe kwa wenyewe,” amesema.
Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wametendea haki kwanza muda wao kwa kuwa vijana wengi sasa wanapoteza muda mwingi kwenye mitandao kufanya vitu vya hovyo, badala ya kufanya vitu ambavyo vingewasaidia.
“Kwa wanafunzi kwenye shule umeenda kusoma, kupata ufaulu, ukifanya makosa tutakupata, sheria inakataza kutukana, kufanya uchochezi, kuzusha taharuki, kudhalilisha. Tumeanza kuona kwenye mitandao watu wanafanya,” amesema Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Sasa naomba niwaambie hakuna atakayefanya makosa haya akabaki salama, tutampata litakuwa ni suala la muda tu, hatutakupata leo, tutakupata kesho tutakupata keshokutwa tutakupata wiki ijayo tutakupata mwakani, jinai haifi,” amesema.