Rais Samia asimulia uwekezaji bandarini ulivyobadili msimamo Benki ya Dunia

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amesimulia uwekezaji wa bandari ulivyoivutia Benki ya Dunia kutaka kutoa mkopo ambao awali, iligoma kuutoa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema maboresho na uendelezaji uliofanywa katika sekta ya bandari, umeifanya Benki ya Dunia (WB) iliyogoma kuikopesha Tanzania kwa shughuli hiyo, ijitokeze baadaye na kutaka kuikopesha.
Mkuu huyo wa nchi, amesema hatua ya WB kuja baadaye na kuonyesha utayari wa kutoa mkopo kwa Tanzania kwa ajili ya uendelezaji wa bandari, imetokana na kuona kuwa Taifa lenyewe limeiendeleza vema sekta hiyo.
Katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali imeiboresha sekta ya bandari kwa uwekezaji, kadhalika kuingia ushirikiano na sekta binafsi, ikiwemo Kampuni ya DP World inayoendeleza na kuendesha bandari ya Dar es Salaam.
Uwekezaji na ushirikiano huo wa sekta binafsi na umma bandarini, umechochea ongezeko la mapato, ufanisi na hata kuifanya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikusanye Sh325.3 bilioni kwa kipindi cha miezi mitano pekee, kama ilivyowahi kuelezwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumanne Juni 10, 2025 alipohutubia hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya Serikali, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesimulia mwaka 2023 Serikali iliomba mkopo WB kwa ajili ya kuendeleza bandari, lakini taasisi hiyo ya fedha ilikuja na masharti lukuki ikionyesha kwanini haitaweza kuikopesha Tanzania kwa shughuli hiyo.
Baada ya kuona Serikali imeanza kuiboresha na inakusanya fedha kutokana na sekta hiyo, amesema benki hiyo ikajitokeza yenyewe bila kufuatwa, ikitaka kuikopesha Tanzania Dola za Marekani 500 milioni (zaidi ya Sh 1.302 trilioni) kwa ajili ya uendelezaji wa bandari.
“Mbossa (Plasduce-Mkurugenzi Mkuu wa TPA), akaja mbio kwangu, mama… nikamwambia mh! Tulia kwanza usiharakishe. Hawa wameshaona kitu hawa, kaa nao zungumza nao ujue, wana kitu gani haswa, wasione kwamba tunaendelea sasa wenyewe 500 hii ikaja ikatutokea puani.
Nikamwambia una fedha ya kutosha ya kufanya uendelezaji, anza mwenyewe. Ukikwama tutaangalia, tunakwenda huko au tunakwenda wapi,” amesema.
Rais Samia amesema imewezekana kufanya hivyo, kwa sababu nchi ina fahari ya kufanikisha mambo yake yenyewe bila utegemezi na kwamba hata wakopeshaji wanakufuata, badala ya kuweka masharti lukuki.
Akizungumza na Mwananchi Ikulu Dar es Salaam baada ya gawio, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbosa amesema mabadiliko yaliyofanyika katika uendeshaji wa bandari ndiyo siri ya mafanikio.
Mabadiliko hayo, amesema yamesaidia kupunguza gharama za uendeshaji zilizokuwa zikitumika awali kwa asilimia 46.
Kabla ya kuingia kwa wawekezaji matumizi ya kawaida ikiwemo kununua mitambo, vifaa zaidi yalikuwa yakitumia Sh1.1 trilioni zilikuwa zikitumika ambazo sasa zimeshuka hadi Sh537 bilioni.
“Huu ni upungufu wa zaidi ya asilimia 46 na hiyo ni kwa sababu eneo kubwa ambalo linaendeshwa na wawekezaji sasa wao ndiyi wanabeba gharama zote na hii ndiyo sababu tulikuwa tukiwaambia wananchi wawekezaji hawa wana mtaji kwa sababu wao wanaweza kubeba gharama ambazo tulikuwa tukibeba awali,” amesema.
Amesema fedha ambayo ilikiwa ikitumika awali sasa inapelekwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo kupanua bandari iliyopo Mtwara, ujenzi wa matenki ya mafuta zaidi ya Sh600 bilioni, Bandari ya Mbambabay zaidi ya Sh70 bilioni sambamba na Kemondo Bukoba na huduma nyingine.
“Sasa na si gawio tu na kodi kubwa tunatoa na hili linatokana na mabadiliko tuliyofanya. Siri ya kuendelea kuchangia gawio hili ni mabadiliko ya kiutendaji ambayo tumefanya na tunayoendekea kufanya,” amesema Mbosa.