JP Magufuli sio daraja tu, ni ufunguo wa kiuchumi

Moja ya alama kuu za juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu na kukuza uchumi, ni Daraja la JP Magufuli, ambalo awali liliitwa Kigongo Busisi. Ujenzi wa daraja hili umekamilika kwa asilimia 100 na sasa linakwenda kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 19, 2025.
Mabadiliko ya jina la daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 yana uhusiano wa moja kwa moja na historia ya Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati Dk John Magufuli.
Mitazamo ya wengi ilikuwa kufariki kwa Hayati Magufuli, kungezima ndoto ya kukamilika kwa mradi huo, unaogharimiwa kwa Sh716.3 bilioni ambazo zote zimetolewa na Serikali.
Hata hivyo, aliyeipa uhai ndoto hiyo ni Rais wa Serikali ya awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan ambaye muda mfupi baada ya kuapa kuwa Rais, alijipambanua kuiendeleza miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake, huku akianzisha mipya kwa ahadi ya kuendelea kuijenga Tanzania.
Daraja la JP Magufuli ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati, ambayo Rais Samia si tu anaiendeleza kwa kuakisi ndoto ya Hayati Magufuli, bali pia analenga kuwaondolea changamoto ya miundombinu Watanzania hasa wakazi wa Kanda ya Ziwa kutoka eneo moja kwenda lingine.
Historia ya daraja na Hayati Magufuli
Katika ziara yake Desemba 31, mwaka 2020 kutembelea mradi huo, Dk Magufuli, aliwaambia wakazi wa eneo hilo kuwa anayo historia na daraja hilo, tangu wakati ambao hakuwa na wadhifa wa urais.
“Siku moja niliondoka Mwanza kwenda Busisi kuposa, nimefika pale kwa Mzee mmoja ni Askari Magereza anaitwa Mathias Mbiza, nikamaliza kuposa na mahali tukapatana, wakati wa kurudi Kivuko kilikuwa MV Geita au Sengerema.”

Anaongeza, “Kikawa kimeharibika na kilikuwa kinafanya hivyo kila siku, nilikuwa na pikipiki yangu XL 125 Honda, kwa hiyo kulikuwa na mitumbwi walikuwa wanavusha kwa pesa, kila mara kivuko kilipoharibika watu walipakiwa kwenye mitumbwi”.
Anasema alisogea karibu na eneo hilo na wavushaji walimtaka kuingia kwenye mtumbwi na pikipiki yake, alipofikiria moyo ulikataa, wakati huo kulikuwepo na familia na baskeli yao walipakiwa.
“Mimi nikazunguka Kamanga, nilipofika Mwanza ule Mtumbwi ukawa umezama na ukaua watu 11, hivyo ninaifahamu na ndiyo maana nilipofanikiwa kuwa Waziri wa Ujenzi mawazo yangu yalikuwa niokoe maisha ya watu wa hapa,” anasema.
Samia akatimiza ndoto, amekamilisha kazi
Rais Samia aliingia madarakani pamoja na mambo mengine, mradi huo ulikuwa sehemu ya ile aliyoiangazia kuhakikisha inakamilika.
Juhudi zilizofanywa na Serikali, zimewezesha kazi ziendelee kufanyika usiku na mchana na hatimaye ujenzi wa daraja umekamilika na wananchi wanasubiri kuzinduliwa tu.
Draja hilo linaunganisha barabara kuu ya Usagara - Sengerema - Geita katika Ziwa Victoria hivyo, kulifanya daraja hilo kuwa la kipekee.
La sita kwa urefu Afrika
Daraja la JP Magufuli limetajwa kuwa refu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati, huku likishika nafasi ya sita kwa bara la Afrika.
Hilo lilithibitishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara, Joseph Haule alipokagua ujenzi wa mradi huo mkoani Mwanza.
Katika orodha ya madaraja marefu, linaloongoza ni 6th October lililopo nchini Misri lenye urefu wa kilomita 20.5.
“Kama mnavyoona Tanzania sasa tunazidi kupaa, tumeona madaraja mengine mengi makubwa na mazuri yakichukua rekodi lakini sasa daraja hili ndilo litakalovunja rekodi nchini, Afrika Mashariki na Kati,” alisema.
Mengine marefu ni Third Mainland la Nigeria (kilomita 11.8), Suez Canal la Misri (kilomita 3.9), Kisiwa cha Msumbiji (kilomita 3.8), na Dona Ana la Msumbiji (kilomita 3.67), kisha JP Magufuli linafuata.
Manufaa makubwa kiuchumi
Utekelezwaji wa mradi huo, siyo tu utaunganisha pande mbili za wakazi wa maeneo ya jirani, bali pia linafungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii.
Mradi huo pia, utapunguza gharama za usafirishaji kwa kuwa kwa sasa, kivuko cha Kigongo-Busisi kinabeba abiria na bidhaa kuvuka Ziwa Victoria, jambo linalosababisha msongamano mrefu na ucheleweshaji.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, takriban magari 1,600 huvuka kwa kivuko hicho kila siku, huku abiria zaidi ya 2,000 wakikabiliwa na changamoto ya kungoja kwa muda mrefu.
Kwa kukamilika kwa daraja hilo, gharama za usafirishaji zinatarajiwa kupungua kwa asilimia 25 hadi 30, huku muda wa kusafiri kati ya mikoa hiyo ukipungua kutoka zaidi ya saa mbili hadi dakika chache.
Daraja hilo pia litaunganisha maeneo ya uzalishaji wa mazao kama dhahabu, pamba na samaki kutoka mkoa wa Geita na masoko ya Mwanza, ambayo ni kitovu cha biashara cha Kanda ya Ziwa.
Takwimu za Benki ya Dunia mwaka 2023, zinaonesha mradi huu unatarajiwa kuongeza thamani ya biashara kati ya mikoa hii kwa zaidi ya asilimia 40 katika kipindi cha miaka mitano baada ya kukamilika.
Ujenzi wa daraja hilo, umeajiri zaidi ya wafanyakazi 700 wa ndani, wengi wao wakiwa vijana wa kitanzania. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), ajira hizo zimechangia kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa maeneo ya Kigongo na Busisi.
Pia, ripoti inakadiria kwamba ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zitokanazo na mradi huo zinaweza kufikia zaidi ya 5,000 baada ya kukamilika, kutokana na kuanzishwa kwa shughuli za kibiashara kama migahawa, huduma za usafiri na biashara ndogondogo.
Utalii ni faida nyingine ya daraja hilo kwa kuwa Ziwa Victoria ni kivutio kikubwa cha watalii, mradi huo unatarajiwa pia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea mkoa wa Mwanza na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha idadi ya watalii katika Kanda ya Ziwa iliongezeka kwa asilimia 10, huku matarajio ya ongezeko zaidi yakiwa ni asilimia 20 baada ya daraja kukamilika, kutokana na urahisi wa usafiri wa barabara.
Ulega awapa kicheko makandarasi
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema daraja hilo lililojengwa na kampuni ya China Civil Engineering (CCECC) licha ya kuwa la kwanza Afrika Mashariki na kati likiwa na urefu wa Kilomita tatu na urefu wa mita 17 kutoka usawa wa ziwa, pia ni kivutio na fahari kwa Tanzania.
Ulega amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha ndoto hiyo inakamilika kwani, wakati huo anaingia madarakani lilikuwa limetekelezwa kwa asilimia 25 pekee.
Amesema faida kubwa ambayo Taifa limeipata kupitia mradi huo ni wataalamu wazawa kushiriki kuanzia hatua ya kwanza hadi kukamilika kwake, na kuchota ujuzi mbalimbali ikiwemo teknolojia ya ujenzi wa madaraja makubwa na usimamizi wa miradi hiyo.
Amesema Serikali itaanza kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa ya kimkakati makandarasi hao wazawa waliovunwa kwenye miradi mbalimbali badala ya kutegemea kampuni za kigeni.
"Wataalamu wazawa walifanya ushiriki kuanzia hatua ya mwanzo ya ubunifu, huko mbele ya safari tukiwa na miradi mikubwa kama huu watapata nafasi kwa sababu wamepata elimu na utaalam wa kutosha," amesema Waziri Ulega na kuongeza;
"Kwa mfano tunaye Mhandisi Kaswaga (Katelula) ambaye ni ofisa wa mradi huu amefanya kazi kuanzia mwanzo mpaka mwisho na pia anasimamia madaraja ya Simiyu na Pangani ni miongoni mwa wataalamu wazawa tunaowategemea. Huyu na wenzake wataaminiwa na kupewa miradi kwa sababu ipo mingi inayoendelea na inayokuja."