Rais Samia aagiza usimamizi ulipaji kodi, atahadharisha misaada ya wahisani

Muktasari:
- Rais Samia amesema hakuna nchi inayoendeshwa bila wananchi wake kulipa kodi, hata wahisani wanaosaidia, nao wanategemea kodi za wananchi wao.
Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara kulipa kodi ili nchi ijiendeshe kwa mapato yake ya ndani bila kutegemea misaada ya wahisani, ambao amedai kuwa sasa wana masharti mengi.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 16, 2025 mara baada ya kuzindua jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu, Rais Samia amesema hakuna nchi inayoendeshwa bila wananchi wake kulipa kodi, hata wahisani wanaosaidia nao wanategemea kodi za wananchi wao.
“Hao wanaoendelea huko na wakatusaidia, ni pesa za walipa kodi wao…wamejenga, zimebaki wanatusaidia, lakini tutaomba mpaka lini? Hatuna haja ya kuomba.
“Wakati mwingine tunafanya kufuru ndugu zangu. Tanzania hii Mungu katupa madini, katupa bahari, katupa maziwa, katupa ardhi nzuri, katupa kila kitu, lakini bado tumejikunja hivi tunangojea mtu mweupe aje achimbe, achukue apeleke kwao, kiduchu atupe, hapa alafu tunaomba kule alikopeleka. Tunaomba wakati ile pesa ilitoka huku kwetu, hatuna haja ya kufanya hivyo,” amesema Rais Samia.
Ametolea mfano wa mwanaume mzuri ni yule anayeendesha nyumba yake vizuri na kusimama vizuri kwenye nyumba yake, akifafanua kwamba hata Serikali lazima ikusanye kodi ili iendeshe nchi yake vizuri.
Azungumzia madeni
Rais Samia amesema hivi sasa Serikali imepeleka huduma mbalimbali zikiwemo za maji, afya na umeme kwa fedha za ndani huku akieleza kwamba hata kama imekopa, ina uwezo wa kulipa.
Amesema Serikali ilikuwa na fedha, imezitawanya kwa kufanya miradi mbalimbali nchini kwa makusanyo ya ndani, akitolea mfano miradi sita anayoizindua leo Simiyu, kwamba imejengwa kwa fedha za ndani, kasoro mmoja wa ambao ni kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji.
Mkuu huyo wa nchi amesema nchi nzima miradi inaendelea, kuna fedha za mikopo, misaada lakini zipo zinazokusanywa ndani.
“Sasa hivi tuna uwezo, tumepeleka maji nchi nzima, tuko kama tulivyotumwa na ilani kwa fedha za ndani na kama tumekopa tunaweza kulipa, tumekopa kuharakisha utekelezaji lakini kwa sababu tunalipa ni fedha zetu,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa: “Tumejenga vituo vya afya…mashine inayotupima Tanzania leo tukikupeleka India na Marekani, utapimwa na mshine hiyo hiyo ambayo Tanzania ipo. Matibabu ya kisasa, umeme kila mahali na tunapeleka umeme vijijini na kote, watu wazalishe mradi kidogo unachokipata changaia rudisha serikalini kupitia mapato ili nchi iweze kusonga mbele.”
“Kwa hiyo, tumefanya mengi kwa sababu tunakusanya ndani, ndiyo tunakopa lakini kwa miradi mikubwa, lireli lile hatutoweza kujenga wenyewe, lazima tuwabembeleze tukopesheni tulijenge, halafu reli likizalisha, tunarudisha fedha zako. Niwaombe sana TRA, jitahidini sana kukusanya mapato kwa njia rafiki,” amesema.
Ataja madhara ya misaada
Wakati akiwataka TRA kukusanya kodi kwa njia rafiki, Rais Samia ametoa angalizo kwa mamlaka hiyo kutowafumbia macho wafanyabiashara watakaokaidi kulipa kodi kwa makusudi, akisema ili nchi ijivunie na kujiamini, lazima ikusanye chakwake.
“Ninachotaka kuwaambia wanangu wa TRA ni kwamba mwanadamu anayejivuna na anayejiamini ni yule mwenye chake...unacho chako unajipangia matumizi unavyotaka. Ukitegemea mtu akupe, ukitegemea mtu akukopeshe…hujakaa vizuri, hali haijawa, anakuja kukwambia mbele za watu ‘deni langu, hujanilipa pesa zangu, nakudai’ Uanaume wako upo hapo? amehoji Rais Samia.
Ameendelea kusema: “Ukitegemea msaada, wale wanaopewa msaada dunia nzima sasa ipo juu chini, vita, ugomvi, vurugu, chumi zimeshuka hawafanyi vizuri kama tunavyofanya hapa.”
Kiongozi huyo wa nchi, amewataka wanaofanya tafiti wakafanye tafiti Ulaya na Marekani, akieleza sasa hivi hawafanyi vizuri kama Tanzania inavyofanya vizuri kiuchumi.
“Sisi hapa hata ndani, Kanda yetu ya East Africa (Afrika Mashariki), Tanzania tunafanya vizuri sana, niwaombe sana watoto wangu, ndugu zangu TRA, twendeni tukakusanye, tukusanye kirafiki,” amesema.
Amewataka kutowafanya wafanyabiashara maadui kwa kuwafungia maduka na kuwanyang’anya vitendea kazi vyao, badala yake wazungumze kujua wana uwezo wa kulipa, kiasi gani na kwa wakati gani, lakini kutowafumbia macho wadaiwa sugu.
“Lazima niseme hapa, kuna masugu, lazima tufanye hivyo...kuna wengine wana viburi, lazima tufanye hivyo. Kwa hiyo, inapobidi tutafanya hivyo lakini kwa kawaida isiwe ndiyo mwenendo wetu, tuwaite, tukae nao, tuzungumze nao tujue tatizo lake ni nini,” amesema Rais Samia.
Aipongeza TRA
Rais Samia amewapongeza TRA kwa kukusanya mapato ambayo yamewezesha kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa majengo ya TRA Simiyu.
“Niwapongeze, zamani ukisikia TRA kila mtu alitaka kwenda TRA kwa sababu ukikaa TRA miezi mitatu, sita wewe umenona, suti nzuri umeng’ara na hivyo…lakini sasa ni TRA ya kukusanya kwa ajili ya nchi yetu, hilo nawapongeza sana kwa sababu yote tunayoyafanya,” amesema.
Amesema uwepo wa majengo hayo umeboresha hali ya utendaji kazi kwa kuwa licha ya majengo kuwa mazuri, yana vitendea kazi vya kisasa, mifumo madhubuti inayowapa urahisi wa kufanya kazi wafanyakazi hao.
Amesema ameongeza wafanyakazi zaidi ya 1800 wa TRA ili kuboresha utendaji kazi ambao pia Serikali imewaongezea kiwango cha makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/26 ikiwa ni jitihada za kuwaboreshea hali nzuri ya kufanya kazi, maslahi yao na wao waendeleze kazi.
“Na sina wasiwasi mnaweza kufikia kwa sababu toka nimeshika dhamana hii, nimekuwa nikiangalia mwenendo wa makusanyo ya TRA kila mwaka, mnapanda mnapanda mnapanda na asilimia tuko kwenye 98, 99 baadhi ya mikoa kidogo ndio wapo 97, kwa hiyo nina hakika tutakwenda zaidi,”
Amesema kuna mikoa wamepita zaidi ya asilimia 100 wakiwabeba wenzao, hivyo ana uhakika kiwango cha makusanyo kilichoongezwa kitafikishwa kwenye mwaka ujao wa fedha.
Jengo la TRA Simiyu
Awali, akitoa taarifa kwa Rais Samia, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema jengo hilo lenye ghorofa tatu, lilianza kujengwa mwaka 2023 na kukamilika mwaka huu, kwa gharama ya Sh9.483 bilioni na lina uwezo wa kuchukua watumishi 200 pamoja na kutoa huduma mchanganyiko ikiwemo mabenki na kumbi za mikutano.
“Kwa hiyo ni moja kati ya jengo la kisasa kabisa na miongoni mwa majengo yanayyoendelea kujengwa kwa mwaka huu wa fedha unaoisha ambayo yamegharimu Sh116 bilioni, yapo mikoa yote 33 na wilaya,” amesema Mwenda.
Amesema jengo hilo litatoa huduma bora kwa walipa kodi ambao matatizo yao ya kikodi yatatatuliwa, pia linaenda kuongeza hamasa kwa watumishi kwakuwa watakaa sehemu nzuri na kuwa na morali ya kazi ya hali ya juu hivyo watafanya vizuri zaidi.
“Lakini hili jengo linaenda kuongeza ulipaji kodi. Mkoa wa kikodi wa Simiyu kwa mwaka huu ambao unaisha ulipaswa kukusanya Sh22 bilioni lakini mpakhivi tunapozungumza wameweza kukusanya Sh25 bilioni na hii kwa sababu wamehamasika sana,” amesema.
Amesema majengo hayo ambayo yanajengwa nchi nzima kwa muda wa miezi 11 kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2025, TRA Bara na Visiwani wamekusanya Sh28.861 trilioni badala ya Sh27.841 trilioni iliyopaswa kukusanywa, sawa na asilimia zaidi ya 103.