Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgogoro wa Israel, Iran utakavyoiathiri Tanzania kiuchumi

Wakati hali ya sintofahamu ikitanda Mashariki ya Kati kufuatia mashambulizi kati ya Israel na Iran, dunia inashuhudia mtikisiko wa kiuchumi unaogusa karibu kila kona ya masoko ya fedha, bidhaa, usafiri wa anga, na hata mifumo ya uzalishaji wa bidhaa.

Tanzania nayo haijabaki salama, hasa ikizingatiwa utegemezi wake mkubwa katika bidhaa zinazotoka eneo hilo, lakini uzoefu wa namna ambavyo migogoro ya ulimwengu imekuwa ikiathiri uchumi wa Taifa hili kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara, mzozo huu unaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa bei ya mafuta duniani, kuibua wasiwasi wa mfumuko wa bei, na kusababisha taharuki kwenye masoko ya mitaji.

Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imepanda hadi Dola za Marekani 74.60 kwa pipa, ikiwa ni ongezeko la karibu asilimia 7 ndani ya siku chache tu tangu Israel kuzindua shambulio la kushtukiza dhidi ya Iran.

“Eneo la Mlango wa Hormuz ni muhimu kwa usafirishaji wa karibu theluthi moja ya mafuta yote yanayosafirishwa kwa meli duniani,” anasema Hamzeh Al Gaaod, mchambuzi wa masuala ya uchumi wa dunia kutoka TS Lombard. “Iwapo Iran itafunga mlango huo, bei inaweza kupaa hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa – na hiyo ni habari mbaya kwa nchi zinazoagiza mafuta kama Tanzania.”

Mlango wa Hormuz unaunganisha Bahari ya Arabia na Bahari ya Hindi, na upana wake mdogo unalifanya kuwa rahisi kushambuliwa wakati wa vita. Mbunge mashuhuri wa kihafidhina nchini Iran, Esmail Kosari amenukuliwa na shirika la habari la IRINN akisema serikali yao inafikiria kufunga mlango huo – hatua ambayo tayari imeibua hofu kubwa sokoni.

Kulingana na hali hiyo, Tanzania inapaswa kuchukua tahadhari za mapema ili kuzuia athari kubwa za kiuchumi. Serikali inaweza kufikiria kuimarisha akiba ya mafuta, kuangalia upya kodi ya mafuta ili kulinda wananchi dhidi ya ongezeko la gharama, na kuchochea uzalishaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Lakini kilicho wazi ni kwamba katika dunia iliyounganishwa kwa karibu kibiashara, cheche za vita Mashariki ya Kati zinaweza kuwa moto mkubwa kwa uchumi wa dunia — Tanzania ikiwa ni miongoni mwa waathirika wa kwanza.


Tahadhari mfumuko wa bei

Akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26, Waziri wa Fedha, Dk Mwingulu Nchemba alisema ukusanyaji na utumiaji wa Sh56.4Trilioni unaweza kuathiriwa na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza na hivyo kusababisha kutofikiwa kwa shabaha na malengo ya bajeti miongoni mwake ni majanga ya asili na migogoro ya kimataifa.

Mgogoro huo ambao huenda ukawa na athari kubwa katika mifumo ya usambazaji ya ulimwengu, unatokea wakati ambao Tanzania inaendelea na maumivu ya athari za vita kati ya Russia na Ukraine lakini pia kibano cha kodi cha Rais wa Marekani, Donald Trump.

Itakumbukwa kwamba vita kati ya Russia na Ukraine ilipoanza Februari 24, 2022, Tanzania ilikabiliwa na hali ngumu kiuchumi kama vile kupaa kwa bei ya mafuta, bidhaa za chakula hasa ngano na mbolea.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Thobias Swai anasema Tanzania iko hatarini kupatwa na athari za mzozo huo hasa kutokana na utegemezi wake kwa mafuta kutoka Mashariki ya Kati.

“Mafuta tunayoyatumia Tanzania kwa kiwango kikubwa yanaagizwa kutoka ukanda huo. Hivyo, endapo bei ya mafuta itapanda kwa kiwango kikubwa, gharama za uzalishaji, usafirishaji na huduma zitapanda pia. Hii inaweza kuchochea mfumuko wa bei na kuathiri ustawi wa kiuchumi,” anasema.

Aidha, Dk Swai anaonya kuwa hali hiyo inaweza pia kuathiri thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani, hali inayoweza kuongeza gharama ya kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje.


Masoko yatikisika

Soko la hisa la Marekani limeshuka; S&P 500 na Nasdaq Composite zilipungua kwa asilimia 1.1 na 1.3 mtawalia. Ulaya pia haikusalimika – DAX ya Ujerumani, CAC 40 ya Ufaransa, na FTSE 100 ya Uingereza zote zimeshuka, huku wawekezaji wakielekeza mitaji yao kwenye dhahabu na kampuni za ulinzi kama BAE Systems na Lockheed Martin, ambayo hisa zake zimepanda.

Hali hii inaashiria mwelekeo wa dunia kutafuta “maeneo salama” ya uwekezaji, na kusababisha kuporomoka kwa masoko ya hatari kama vile hisa na fedha za nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni.


Athari sekta ya usafiri wa anga

Mashirika makubwa ya ndege kama Emirates, Qatar Airways na Etihad Airways yamesitisha baadhi ya safari zake kuelekea na kutoka Iraq, Lebanon, Iran na Jordan. Iran na Iraq pia zimefunga anga zao kwa muda – hatua inayohatarisha safari nyingi kati ya Asia na Ulaya, zinazopita Mashariki ya Kati.

“Hili lina athari kwa safari za kibiashara, utalii na hata upatikanaji wa bidhaa kwa wakati,” alisema mchambuzi mmoja wa usafiri wa kimataifa.

Hata hivyo, wakati dunia ikifuatilia kwa karibu hali ya kijeshi kati ya Israel na Iran, wasomi wengine wanasema huenda kusiwa na changamoto kubwa kwani hali bado inaweza kudhibitika ikiwa pande zote zitaketi meza ya mazungumzo.

Mhadhiri mwingine wa uchumi wa Udsm (jina limehifadhiwa kwa ombi), anasema: “Siamini kuwa Iran ni nchi yenye silaha za nyuklia. Kama ingekuwa hivyo, Israel isingethubutu kuivamia. Marekani inaitumia Israel kama njia ya kulazimisha Iran irejee mezani kwenye mazungumzo.”

Ameongeza kuwa: “Athari kubwa hutokea pale vita vinapoendelea kwa muda mrefu. Lakini kwa sasa, ni mapema mno kutabiri hasara ya muda mrefu. Tunachoshuhudia ni mshtuko wa muda mfupi kwenye masoko.”


Nini hatma ya uchumi wa dunia?

Wachambuzi wa kimataifa wameonya kuwa endapo mzozo huu utadumu, benki kuu duniani zitakosa nafasi ya kuchukua hatua madhubuti za kisera kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.

“Magavana wa benki kuu wako kwenye mpango wa kupunguza viwango vya riba. Lakini mshtuko wa bei za nishati unaweza kuwalazimisha kusubiri tena,” alisema Al Gaaod.

Hata hivyo, matarajio ya wengi ni kuwa mzozo huo hautachukua muda mrefu na kwamba ushawishi wa kidiplomasia utarejesha hali ya utulivu.