Maandalizi Sabasaba yafikia asilimia 85, maguta, malori marufuku uwanjani.

Muktasari:
- Kampuni zaidi ya 5,000 zimethibitisha kushiriki katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DiTF) huku maandalizi yakiwa yamefikia asilimia 85.
Dar es Salaam. Wakati maandalizi ya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yakiwa yamefikia asilimia 85, walioegesha malori karibu na uwanja huo wametakiwa kuyatoa kuanzia sasa.
Pia, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amezitaka taasisi za Serikali kuongeza kasi katika uandaaji wa mabanda yao ili maonyesho yanapoanza wawe wamekamilisha.
Ametoa kauli hiyo leo, Juni 23, 2025 wakati akikagua maandalizi ya maonyesho ya Sabasaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28 mwaka huu ambapo kampuni zaidi ya 5,000 zimethibitisha kushiriki maonyesho hayo.
Akizungumza baada ya kumaliza kufanya ukaguzi, Mapunda amesema maonyesho hayo yana hadhi ya kimataifa hivyo haipendezi malori kupaki katika maeneo ya uwanja huo wa Julius Nyerere na kusababisba usumbufu.
“Kampuni za usafirishaji, hatuhitaji kuona lori lolote likipaki katika eneo ambalo linakaribiana na viwanja vya maonyesho ya sabasaba. Maonyesho haya ni ya kimataifa yanahitaji viwango vya kimataifa si busara mtu kuja kupaki gari lake na kuanza kutengeza gari lake au kupaki kusubiri kwenda bandarini,” amesema Mapunda.
Akijibu maagizo hayo, mmoja wa madereva, Linus Samson amesema wameyapokea.
“Tutaangalia namna ya kuwa tunaegesha magari haya kama alivyosema lakini wanapaswa kutambua kuwa sehemu za maegesho hazitoshi,” amesema Samson.
Mbali na agizo hilo pia aliyataka mashirika ya serikali kuongeza kasi ya maandalizi ya mabanda yao.
“Wakiendelea hivi kwa tukafika Julai 3 siku ya uzinduzi rasmi na mabanda yao yakawa hayana hadhi inayostahili, Wajifunze kwa kampuni binafsi namna wanavyoenda kwa kasi katika uandaaji wa mabanda yao, kwani hadi siku ya uzinduzi tayari maonyesho yanakuwa yameanza,” amesema Samson.
Akizungumzia utofauti wa maonyesho haya na mengine, Mapunda amesema mwaka huu kutakuwa na usafiri maalumu ndani ya uwanja kwa ajili ya watembeleaji na ubebaji wa mizigo.
“Tumeweka utaratibu mzuri wa usafiri wa watu na mizigo, tofauti na miaka ya nyuma mafuso na maguta ndani ya uwanja hayatakuwapo kuna utaratibu wa kuchukua bidhaa za wateja kwenda nje ya uwanja na hadi nyumbani pia utaratibu wa kuingiza uwanjani mizigo ya waonyeshaji umewekwa,” amesema.
Pia kutakuwa na usafiri wa ndani ya uwanja kwa ajili ya watembeleaji wasioweza kutumia muda mwingi kutembea.
Wale wanaoona tabu kutembea kutoka banda moja hadi lingine sasa hivi tutakuwa na usafiri umeandaliwa ikiwemo magari ya umeme unaenda mabanda yote unayotaka. Pia Kutakuwa na usafiri wa kuwaleta watu wenye mabanda na kuwarudisha nyumbani kwao hivyo kuonda ulazima wa waonyeshaji kuwa na magari,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuitaka Dart kuangalia namna inavyoweza kuleta usafiri wa magari ya haraka kati ya Posta hadi Mbagala Rangi Tatu na Mbagala Rangi Tatu hadi Gerezani ili kuweka urahisi kwa watembeleaji kufika eneo hilo.
Katika hilo, Ofisa Habari wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), William Gatandu amesema walikuwa wakizungumza na mtoa huduma kuangalia kama mabasi yatatosha kwani si busara kupeleka mabasi katika njia hiyo wakati maeneo mengine hayatoshi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo yaBiashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis amesema jadi sasa washiriki zaidi ya 5,000 kutoka ndani na nje ya nchi huku nchi 23 zikiwa zimethibitisha kushiriki.
“Kwa upande wa nchi za Afrika ya Mashariki kama Burundi na Uganda bado tunapokea washiriki na tuna imani hadi Juni 28, 2025 kampuni zitakuwa zimeongezeka,” amesema Latifa.
Akizungumzia kuzuiwa kwa maguta na malori ndani ya uwanja wakati wa maonyesho, Latifa amesema Shirika la Posta limejipanga kuhakikisha kunakuwa na usafiri ndani ya uwanja na waonyeshaji kupitia programu maalumu.
“Hii itakuwa rahisi na salama na watu Watakasafirishiwa kutoka mtaani hadi uwanjani,” amesema.
Haya yanasemwa wakati ambao Mwananchi imeshuhudia mashirika na kampuni mbalimbali zikimalizia mabanda yao kwa ajili ya maonyesho haya.
Wakati wao wakimalizia, baadhi ya watu tayari wameanza kupita kutafuta ajira huku kicheko kikiwa kwa mafundi na wapambaji wakiendelea kufurahia fedha.