Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sabasaba mpya ya saa 24 kujengwa kwa ubia

Katika harakati za kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa kisasa, Serikali ya Tanzania inatarajia kutumia zaidi ya Sh948.5 bilioni kubadilisha sura ya Uwanja wa Maonyesho wa Mwalimu Julius Nyerere maarufu kama Sabasaba.

Uwanja huu ambao kwa miongo kadhaa umehifadhi historia ya maonyesho ya biashara ya kimataifa, sasa unatazamwa kwa jicho jipya jicho la mageuzi, maendeleo na ustawi wa kisasa.

Mradi huo wa kimkakati wa ushirikiano unatarajiwa kutekelezwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Ofisi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kupitia wabia mbalimbali walioalikwa kuchangamkia fursa hiyo.

Utekelezaji wake unalenga kuifanya Sabasaba kuwa kitovu cha kisasa kinachovutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Miundombinu ya hali ya juu itajengwa, ikiwa ni pamoja na majengo ya biashara ya kimataifa, maeneo ya burudani ya kisasa, hoteli za nyota tano, vituo vya teknolojia na ubunifu, pamoja na maeneo ya wazi kwa ajili ya shughuli za kijamii, sanaa na utamaduni.

Aidha, mpango huo mkubwa utachochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza fursa za ajira, kuwainua vijana kiuchumi, na kuhimiza ubunifu wa kizazi kipya. Sabasaba mpya haitabaki kuwa tu mahali pa maonyesho ya msimu, bali itakuwa mahali pa kudumu pa shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Hamisi anasema sababu ya maboresho hayo ni uwanja huo kwa sasa umepitwa na wakati, hivyo kuna haja ya kuufufua kwa viwango vya kimataifa.

“Uwanja wetu umepitwa na wakati, tunatambulisha mpango mkakati wa kuuendeleza ili kuvutia wawekezaji wenye nia ya dhati. Tunawaomba wawekezaji kujitokeza huku kwani mradi huu unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani 322 milioni (Sh948.5 bilioni) na unatarajiwa kukamilika kabla ya mashindano ya AFCON,” anasema.

Anasema mradi huo utahusisha ujenzi wa kumbi za kisasa, hoteli, maeneo ya burudani, makazi, mifumo ya ulinzi wa kidijitali, mawasiliano na taa za kisasa kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea.

Kupitia maboresho hayo, sasa wananchi watapata nafasi ya kuutumia uwanja huo kwa saa 24 kwa wiki nzima bila kungoja tu maonyesho ya Sabasaba.

“Kutakuwa na shopping malls (maduka makubwa), majengo ya biashara na hoteli zitakazowezesha watu mbalimbali kukaa pale, pia, utakuwa kivutio kikubwa kwa uchumi wetu,” anasema. 

Latifa anasema uchambuzi wa kina utafanyika ili kupata mwekezaji bora wakiwemo wale watakaowasilisha mapato ya manufaa kwa TanTrade, muhtasari wa nia ya uwekezaji, pamoja na uwezo wa kiusimamizi na kiteknolojia.

“Mradi huu tunatamani uanze hata kesho. Muda wowote mwekezaji atakapopatikana, utekelezaji utaanza mara moja,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa PPP, David Kafulila anasema Serikali pekee haiwezi kumudu kugharamia mradi huu mkubwa hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni jambo la lazima.

“Ni gharama kubwa na tunahitaji wadau wa sekta mbalimbali kuwekeza katika mradi huu wa kipekee,” anasema.

Kafulila anawataka wananchi kuondokana na dhana kuwa uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya umma ni kuuza mali ya umma na badala yake wazoee kuona sekta za umma zikiendeshwa na sekta binafsi.

“Si kuuza uwanja, bali ni njia ya kuleta faida kubwa kwa jamii na taifa,” amesema. 

Anawataka wawekezaji wenye nia kufanya maandalizi ya kina na kuwasilisha nyaraka muhimu kama nakala za usajili, wasifu wa kampuni, na ushahidi wa uwezo wa kifedha ili kushiriki katika mchakato wa uteuzi.

Mradi huo wa kuendeleza uwanja Sabasaba pia unatarajia kutoa fursa mpya za ajira, kuimarisha mapato ya serikali na kupanua wigo wa biashara za ndani na za kimataifa. 

Matarajio ya wafanyabiashara

Mmoja wa wafanyabiashara jijini hapa, Silauli Nkinga anasema suala hilo limechelewa kwani uwanja huo ungekuwa umeingiza fedha nyingi ikiwa hili lingefikiriwa tangu zamani.

“Unajua mbali na sabasaba uwanja ule huwa hauna kazi, uwanja ni kama unafungwa zinabaki ofisi za Tantrade peke yake, unaweza kuona ni fedha kiasi gani ambazo zingeweza kupatikana, hata kama wanakodisha kumbi katika siku za kawaida lakini haiwezi kuleta fedha nyingi kama eneo hili lingekuwa linatumika kimalifu,” anasema Nkinga.

Anasema uwekezaji huo ni vyema uangalie zaidi namna ya kuwezesha bidhaa za Tanzania ikiwemo mazao ya kilimo yanayozalishwa ili kuongeza tija kwa wakulima.

Maneno yake yanaungwa mkono na Elizabeth Mambo ambaye ni mfanyabiashara, anasema kuwapo ikiwa maboresho hayo yatakamilika inaweza kuwa moja ya njia ya wafanyabiashara wadogo kupata masoko ya kimataifa kwani Tantrade hushughulika na masoko hayo.

“Tantrade huwa inaratibu masoko ya kimataifa sasa wanapokuwa na soko la kisasa katika ofisi zao inasaidia wafanyabiashara wadogo kupata soko la uhakika, nina imani kuwa kutakuwa na eneo kwa ajili yao na ningetamani mradi huu ufanyike kwa haraka ili tunufaike nao,” anasema.

Anasema anaamini ujio wa mradi huu utakuwa ni fursa kwa Watanzania wote hususani vijana ambao wanatafuta fursa za ajira huku wengine wakiwa ni wahitimu wa vyuo lakini hawana sehemu za kujiingizia kipato.

“Kama ambavyo huwa msimu wa sabasaba kwa vijana kunufaika na fursa ajira za muda sasa hizi zitakuwa ni endelevu, tutamkomboa kijana wa kitanzania na kumfanya atoke katika makundi mabaya na ajiingizie kipato cha halali,” anasema Elizabeth.

Wachumi wamulika

Mchambuzi wa Uchumi, Dk Donath Olomi anasema jambo hilo litakwenda kusaidia ukuaji wa uchumi huku akiunga mkono matumizi ya PPP katika utekelezaji wake.

Anasema wakati mwingine matumizi ya PPP haimaanishi kuwa serikali haina fedha ya kutekeleza mradi husika bali ina mambo mengi ambayo inapaswa kutekelezwa ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya, miundombinu na elimu.

Mwanazuoni huyo anasema kuwekeza kwa ubia pia inaweza kupata matokeo tarajiwa kwani ukishirikiana na mtu anayejua biashara anakuja na utalaamu, mbinu nzuri za uendeshaji ambazo zitakuwezesha kupata faida ya kile ulichokusudia kufanya.

“Hata katika usimamizi wanakuwa wapo vizuri, ikifika wakati wa kuchagua bodi wanakuwa wanajua ipi wanayohitaji, wanataka iwaje, Mkurugenzi apatikane kwa namna gani ili kufanikisha kile mnachokihitaji,” anasema Dk Olomi.

Maneno yake yaliungwa mkono na mchambuzi wa uchumi, Oscar Mkude anayesema utumiaji wa PPP katika utekelezaji wa mradi huu utasaidia kupunguza utegemezi kwenye fedha za Serikali na kuiacha itumike katika mambo mengine.

Hata hivyo, anataka kuwapo mkazo kuhakikisha miradi ya ubia iliyoanzishwa inatekelezwa kwa wakati ili kujenga imani ya wawekezaji na siyo kusubiri muda mrefu kabla ya kuanza utekelezaji baada ya kusainiwa kwa mkataba husika.

Akizungumzia maboresho hayo, anasema kama nchi inapohitaji kujenga kituo cha kimataifa cha kibiashara ni vyema kuangalia namna mradi huo utakavyochagiza shughuli za kiuchumi.

“Tunaweza vipi kutumia eneo hilo kuangalia namna linavyoweza kuchagiza malengo yetu ya kiuchumi kwani unaweza kujenga eneo kama lakini kama huna msingi wa ndani unaweza kujikuta unatumika kama kituo cha nchi nyingine kuuza bidhaa zake katika soko lako,” anasema.

Anasema ikiwa nchi inayoleta bidhaa lengo lake ni kuwa mzalishaji kama malengo ya tanzania yalivyo yanaweza kuua ndoto za nchi hivyo ni vyema kile kinachokwenda kufanyika kifungamanishwe na Dira ya Maendeleo 2050.

“Ukijenga kituo hakikisha unajenga uwezo wa kuzalisha bidhaa na kusaidia ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo za kilimo, angalia namna kile unachokifanya kinaendana na malengo yako, kama ambavyo tunakwenda kuzindua DIra 2050 hivyo ni vyema kuhakikisha tunachofanya kinaunga mkono malengo yetu,” anasema.