Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Sh948.5 bilioni kubadili uwanja wa maonyesho Sabasaba

Muktasari:

  • Katika uwekezaji huo mpya, viwanja hivyo sasa vitakuwa vikitumika saa 24 kila siku ikiwa ni baada ya kumbi za kisasa, hoteli, maeneo ya burudani, makazi, mifumo ya ulinzi wa kidijitali, mawasiliano na taa za kisasa kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea.

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh948.5 bilioni zinatarajiwa kutumika katika kuubadili Uwanja wa Maonyesho wa Mwalimu Julius Nyerere, maarufu Sabasaba na kuufanya kuwa kitovu cha kisasa cha biashara, burudani na uwekezaji.

Lengo la kufanya hivyo ni kuongeza kiuchumi wa Taifa huku ikihamasisha mashirika, taasisi na wawekezaji binafsi kushiriki katika kuuboresha uwanja huo wa kihistoria unaokaribia kufikisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, Juni 16, 2025 wakati wa kutambulisha mradi wa kimkakati wa kuubadili uwanja huo kati ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Ofisi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Hamisi amesema sababu ya maboresho hayo ni uwanja huo kwa sasa kuonekana umepitwa na wakati, hivyo kuna haja ya kuufufua kwa viwango vya kimataifa.

“Uwanja wetu umepitwa na wakati, tunatambulisha mpango mkakati wa kuuendeleza ili kuvutia wawekezaji wenye nia ya dhati. tunawaomba wawekezaji kujitokeza, kwani mradi huu unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 322 (Sh948.5 bilioni) na unatarajiwa kukamilika kabla ya mashindano ya Afcon (Fainali za mataifa ya Afrika (Afcon),” amesema.

Amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa kumbi za kisasa, hoteli, maeneo ya burudani, makazi, mifumo ya ulinzi wa kidijitali, mawasiliano na taa za kisasa kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea.

Kupitia maboresho hayo sasa wananchi watapata nafasi ya kuutumia uwanja huo kwa saa 24 kwa wiki nzima bila kungoja tu maonesho ya Sabasaba.

“Kutakuwa na shopping malls, majengo ya biashara na hoteli zitakazowezesha watu mbalimbali kukaa pale, pia utakuwa kivutio kikubwa kwa uchumi wetu,” amesema.

Latifa amesema uchambuzi wa kina utafanyika ili kupata mwekezaji bora wakiwemo wale watakaowasilisha mapato ya manufaa kwa TanTrade, muhtasari wa nia ya uwekezaji, pamoja na uwezo wa kiusimamizi na kiteknolojia.

“Mradi huu tunatamani uanze hata kesho. Muda wowote mwekezaji atakapopatikana, utekelezaji utaanza mara moja,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PPP, David Kafulila amesema Serikali pekee haiwezi kumudu kugharamia mradi huu mkubwa hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni jambo la lazima.

“Ni gharama kubwa na tunahitaji wadau wa sekta mbalimbali kuwekeza katika mradi huu wa kipekee,” amesema.

Kafulila pia amewataka wananchi kuondokana na dhana kuwa uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya umma ni kuuza mali ya umma na badala yake wazoee kuona sekta za umma zikiendeshwa na sekta binafsi.

“Si kuuza uwanja, bali ni njia ya kuleta faida kubwa kwa jamii na Taifa,” amesema.

Aliwataka wawekezaji wenye nia kufanya maandalizi ya kina na kuwasilisha nyaraka muhimu kama nakala za usajili, wasifu wa kampuni, na ushahidi wa uwezo wa kifedha ili kushiriki katika mchakato wa uteuzi.

Mradi huo wa kuendeleza uwanja Sabasaba pia unatarajia kutoa fursa mpya za ajira, kuimarisha mapato ya Serikali na kupanua wigo wa biashara za ndani na za kimataifa.